Rais Magufuli atoa Sh600 milioni ujenzi kituo cha afya Bunju

Wednesday February 05 2020
pic magufuli

Dar es Salaam. Rais  wa Tanzania, John Magufuli ametoa Sh600 milioni za ujenzi wa kituo cha afya kitakachojengwa katika zahanati ya Bunju A  wilayani Kinondoni, Dar es Salaam.

Hayo yameelezwa  leo Jumatano Februari 5, 2020 na mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam,  Paul Makonda aliyeeleza kuwa ujenzi huo utakamilika Mei, 2020.

Makonda amesema wanaipandisha hadhi zahanati  hiyo kuwa kituo cha afya ili wananchi wapate huduma bora.

Amesema kiongozi mkuu huyo wa nchi ametoa fedha hizo baada ya kuona wananchi wa  Bunju A, Mabwepande, Tegeta na MbwenI wanakumbana na changamoto wanapotaka kufanyiwa upasuaji.

Amesema wengi hulazimika kufunga safari kwenda Hospitali ya Rufaa Mwananyamala, kwamba wapo baadhi walipoteza maisha wakiwa njiani.

Amebainisha kuwa watakaotibiwa hao na kuonekana wana shida zaidi wataandikiwa rufaa kwenda Mwananyamala.

Advertisement

"Nilitoa ahadi ya kutafuta fedha kwa ajili ya kuboresha huduma za afya katika wilaya hii,  nashukuru rais ametupatia Sh6 milioni na tunategemea ndani ya miezi mitatu majengo mapya matano yatakamilika,  hivyo kuanzia Juni, 2020 tunatarajia kituo hiki cha afya kuanza kufanya kazi," amesema Makonda.

Amesema katika kuhakikisha huduma zinakuwa bora zaidi wataongeza wauguzi na madaktari 58. Kwa sasa waliopo hawazidi 10.

 

Mganga Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Samwel Laizer amesema fedha hizo zitatumika kujenga jengo la upasuaji, la wanawake, la kulaza wagonjwa wanawake kwa wanaume pamoja na jengo la X ray.

Laizer amesema katika zahanati hiyo wanawake wakijifungua huwa hawapatiwi huduma za dharura ikiwemo upasuaji na kuongezewa damu baada ya kupoteza damu nyingi  wakati wa kujifungua.

"Kituo cha afya kikikamilika huduma hizo zitapatikana pia tutakuwa na jengo la watoto wachanga waliozaliwa njiti watapatiwa huduma hapahapa hivyo tutapunguza vifo vya mama na mtoto," amesema Laizer.

Amesema katika wilaya hiyo mwaka 2019 akina mama waliofariki wakati wanajifungua walikuwa 84 na watoto wachanga 180.

Advertisement