Rais wa zamani Burundi afungwa maisha

Rais wa zamani wa Burundi, Pierre Buyoya

Muktasari:

Rais wa zamani wa Burundi, Pierre Buyoya, ambaye kwa sasa ni mwakilishi maalum wa Umoja wa Afrika nchini Mali, amehukumiwa kifungo cha maisha jela baada ya kupatikana na hatia ya kumuua mrithi wake mwaka 1993, kwa mujibu wa uamuzi wa mahakama ambao AFP imeona nakala yake.

Nairobi, Kenya (AFP).Rais wa zamani wa Burundi, Pierre Buyoya, ambaye kwa sasa ni mwakilishi maalum wa Umoja wa Afrika nchini Mali, amehukumiwa kifungo cha maisha jela baada ya kupatikana na hatia ya kumuua mrithi wake mwaka 1993, kwa mujibu wa uamuzi wa mahakama ambao AFP imeona nakala yake.

Buyoya alipatikana na hatia ya "shambulio dhidi ya kiongozi wa nchi" kutokana na ushiriki wake katika mauaji ya rais aliyechaguliwa kidemokrasia, Melchior Ndadaye, katika mapinduzi yaliyoiingiza nchi hiyo katika vita vya ndani.

Mbali na Buyoya, maofisa 18 wa vyeo vya juu jeshini na raia waliokuwa karibu na kiongozi huyo, wamepewa adhabu kama hiyo.

Watu wengine watatu walihukumiwa kwenda jela kwa miaka 20 kwa "kushiriki" katika uhalifu huo, huku waziri mkuu wa zamani, Antoine Nduwayo, akiachiwa huru.

Ni washtakiwa watano tu kati ya watuhumiwa hao waliokuwepo mahakamani, na waliosalia walihukumiwa bila ya kuwepo. Mmoja wa watuhumiwa aliiambia AFP kwa sharti la kutotajwa jina kuwa wanasheria wao hawakutaarifiwa kuhusu kuwepo kwa hukumu.

Kwa sasa Buyoya ni mwakilishi wa Umoja wa Afrika nchini Mali na mtu anayeheshimika barani Afrika na nje.

Buyoya, ambaye anatoka mbari ya Kitutsi, aliingia madarakani mwaka 1987 kwa msaada wa jeshi. Aliachia madaraka mwaka 1993, wakati Ndadaye, ambaye ni Mhutu, alipochaguliwa kuwa rais. Lakini Ndadaye aliuawa miezi minne baadaye katika jaribio la mapinduzi lililoongozwa na wanajeshi wa Kitutsi wenye msimamo mkali.

Mauaji hayo yalifuatiwa na miaka kadhaa ya vita vya wenyewe kwa wenyewe baina ya makundi ya kimbari, vita ambavyo vilisababisha watu wanaokadiriwa kufikia 300,000 kuuawa.

Buyoya alirejea madarakani baada ya mapinduzi, na kuongoza kati ya mwaka 1996 na 2003.