Sababu RC Mbeya kuwacharaza bakora wanafunzi 14

Muktasari:

  • Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Albert Chalamila amewacharaza bakora wanafunzi 14 wa Shule ya Sekondari Kiwanja wanaodaiwa kuchoma moto mabweni mawili ya shule hiyo saa kadhaa baada ya kukutwa na simu za mkononi.

Chunya. Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Albert Chalamila amewacharaza bakora wanafunzi 14 wa Shule ya Sekondari Kiwanja wanaodaiwa kuchoma moto mabweni mawili ya shule hiyo saa kadhaa baada ya kukutwa na simu za mkononi.

Chalamila amechukua uamuzi huo leo Alhamisi Oktoba 3, 2019 alipotembelea shule hiyo akiwa ameongozana na kamati ya ulinzi na usalama ya Mkoa.

Pia,  ametoa maagizo kwa Jeshi la Polisi kuhakikisha wazazi wa wanafunzi waliokutwa na simu na kuhusishwa na tukio hilo wanalipa Sh1 milioni kila mmoja kwa ajili ya ukarabati wa mabweni hayo.

Oktoba Mosi, 2019 mabweni hayo yaliyokuwa yakikaliwa na wanafunzi 150 yaliteketea kwa moto huku wanafunzi hao wakidaiwa kuhusika.

Hadi leo mchana, wanafunzi watano wanashikiliwa na polisi kati ya 19 waliokamatwa siku ya tukio.

Mkuu wa shule hiyo, Elly Mnyarape amesema Septemba 30, 2019 mchana walifanya msako na kukuta baadhi ya wanafunzi wana simu, kwamba zilikamatwa simu 26, “Usiku wa kuamkia Oktoba Mosi mabweni yaliteketea kwa moto.”