VIDEO: Salamu za Ney wa Mitego, Roma Mkatoliki zatikisa mkutano Bavicha

Monday December 9 2019

 

By Mwandishi Wetu, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Wasanii wa muziki wa kizazi kipya nchini Tanzania, Ney wa Mitego na Roma Mkatoliki wameibua shangwe katika mkutano wa Baraza la Vijana la Chadema (Bavicha) baada ya wenzao kuwasilisha salamu zao, kueleza sababu za kutofika.

Salamu za wakali hao wa Bongo Fleva zilitolewa na wasanii wa filamu nchini,  Shamsa Ford na Geogratius Shija walioalikwa katika mkutano huo wa kuchagua viongozi wa Bavicha unaofanyika katika ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam leo Jumatatu Desemba 9, 2019.

Shangwe zilianza baada ya katibu mkuu wa Bavicha,  Julius Mwita kuwatambulisha wasanii hao wa filamu ili wawasalimu wajumbe 371 wa mkutano huo pamoja na wageni mbalimbali wakiwemo wa vyama vya siasa vya CCM, TLP, CUF, ACT-Wazalendo na Chauma.

“Ukiona wasanii kama mimi niko upinzani ujue ni kazi kweli. Nimeamua kuwa upande huu kwani wengine wako kule na wanatamani wasanii wote wawe kwao,” amesema Shija.

Huku akishangiliwa Shija amesema, “nimepewa salamu na Ney wa Mitego niwafikishie, alitamani sana kufika hapa lakini ametoka tamasha la Fiesta saa 12 asubuhi, sasa amelala lakini anawasalimia sana.”

Tamasha la Fiesta lilifanyika jana Jumapili Desemba 8, 2019 katika uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.

Advertisement

Kwa upande wake Shamsa amesema ana salamu kutoka kwa Roma Mkatoliki aliyeko nchini Marekani, “alitamani sana kuwepo hapa lakini ameshindwa na kunipa salamu zake nizifikishe.”

Huku akishangiliwa na wajumbe wa mkutano huo, Shamsa amesema kwake upinzani ni mapenzi kama walivyo wasanii wengine kuunga mkono vyama vingine.

“Kila mmoja anapaswa kuheshimu matakwa ya mwingine. Nakipenda sana Chadema ndiyo maana kipindi kile nilibaki peke yangu, wengine walinikimbia.”

“Nashukuru sana kupata mwaliko, kikubwa nawatakia uchaguzi mwema. Mtuletee kiongozi mzuri asiyepelekeshwa,” amesema Shamsa.

Msanii huyo amewaomba wanawake wanaogombea nafasi mbalimbali kujiamini.

Wanaowania uwenyekiti  wa Bavicha ni John Pambalu, Dorcas Francis na Mathayo Gekul

Advertisement