Samia ataka wananchi kujiandikisha kwa wingi, kuchagua viongozi wenye maadili

Wednesday October 9 2019

 

By Sharon Sauwa, Mwananchi [email protected]

Dodoma. Makamu wa Rais nchini Tanzania, Samia Suluhu Hassan amewataka Watanzania kuchagua viongozi wa Serikali za mitaa wenye maadili na watakaowaletea maendeleo.

Uandikishaji wa wapiga kura kwa ajili ya uchaguzi huo umeanza jana Jumanne Oktoba 8, 2019 na utafanyika kwa siku saba.

Akizungumza leo Jumatano Oktoba 9, 2019 baada ya kujiandikisha kupiga kura katika  Shule ya Msingi  Kilimani mjini Dodoma, Samia amewataka  Watanzania kujitokeza kwa wingi kujiandikisha.

Samia aliyejiandikisha katika mtaa wa Salimin uliopo kata ya Tambuka Reli jijini Dodoma, amewataka wananchi kutumia haki yao ya msingi ya kikatiba kuwachagua viongozi wenye maadili.

 “Watanzania mjitokeze kwa wingi kujiandikisha (orodha ya wapiga kura) na kupiga kura katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa,” amesema.

Awali, mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk Binilith Mahenge amesema idadi ya vituo katika mkoa wa Dodoma ni 3,679 na hadi jana watu  156,000 walikuwa wamejiandikisha katika orodha ya wapiga kura.

Advertisement

“Idadi hiyo ya jana ni kwa sababu ni siku ya kazi na wengi wako maofisini kwa hiyo wasingeweza kushiriki. Tunategemea siku ya Jumamosi ambayo ni mapumziko idadi itakuwa kubwa,” amesema Mahenge.

Advertisement