Serikali yatoa Sh1.5 bilioni ujenzi chumba cha upasuaji JKCI

Wednesday September 18 2019
pic jkcu

Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania imesema Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) inatarajia kufungua chumba cha tatu cha upasuaji baada ya asilimia 90 ya wagonjwa wa moyo kupatiwa matibabu ndani ya nchi.

Hadi sasa Sh1.5 bilioni zimeshatolewa kwa ajili ya kununulia vifaa vitakavyofungwa kwenye chumba hicho, huku ikifikiria kujenga jengo jingine kutokana na lililopo sasa kutotosheleza.

Hayo yameelezwa leo Jumatano Septemba 18, 2019 na Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu wakati akizindua kambi ya upasuaji wa moyo iliyoandaliwa na taasisi ya Shajjah Charity Group kutoka nchi za Falme za Kiarabu.

“Serikali imeshatenga Sh1.5 bilioni kwa ajili ya kununua vifaa vitakavyofungwa katika chumba kipya cha upasuaji ili kianze kutoa huduma, tunataka kukamilisha ndoto ya Tanzania kuwa nchi ya utalii wa matibabu, lakini pia tunataka kuipanua JKCI kwa kuwa vyumba havitoshi tunafikiria kubomoa jengo moja hapa karibu tujenge  jingine,” amesema.

Mkurugenzi wa taasisi hiyo, Profesa Mohammed Janabi amesema tayari mipango hiyo imekamilika na vifaa vinasubiriwa ili chumba cha upasuaji kianze kufanya kazi.

“Tunashirikiana na wenzetu wa Bohari ya Dawa (MSD) tumeshaagiza vifaa vipo njiani, hivi karibuni tutafunga na tutatoa huduma kwa wagonjwa wengi zaidi,” amesema.

Advertisement

Akizungumzia kambi hiyo amesema hiyo ni mara ya tatu Islamic Foundation wanafika katika taasisi hiyo kutoa huduma.

“Awali walikuja kuangalia miundombinu wakafanya upasuaji kwa wagonjwa 10 pekee wakizingatia pia kutoa mafunzo ya mbinu za tiba.”

“Lakini tatizo wengi wanakuja wamechelewa lakini tangu wameanza kutoa huduma hapa kwetu mpaka sasa jumla wameshafanya kwa wagonjwa 65 ni mgonjwa mmoja pekee ndiyo alipoteza maisha, kambi ya sasa wameshafanya kwa wagonjwa 28 kati ya 40,” amesema Profesa Janabi.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amesema watoto wasiopungua 500 kutoka mikoa yote wanatakiwa kufanyiwa upasuaji lakini changamoto iliyopo ni uchangiaji wa huduma.

“Nilitoa ahadi JKCI kwamba nitahangaika kutafuta marafiki ili kusaidia watoto 60 mpaka kufikia Desemba na sasa tunaendelea vizuri.”

“Wiki hii nimepata Sh10 milioni kwa mchungaji Mwamposa wiki ijayo tutapata nafasi ya kuja na waumini wake ili ifikapo Oktoba watoto 10 wengine wafanyiwe upasuaji,” amesema Makonda

Advertisement