Seth, Rugemalira wasota siku 828 gerezani

Muktasari:

  • Herbinder Seth na James Rugemarila wanaokabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi wanaendelea kusota rumande  kwa siku 828 kutokana na upelelezi wa shauri hilo kutokamilika.

Dar es Salaam. Herbinder Seth na James Rugemarila wanaokabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi wanaendelea kusota rumande  kwa siku 828 kutokana na upelelezi wa shauri hilo kutokamilika.

Washtakiwa hao walifikishwa kwa mara ya kwanza katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Juni 19, 2017 wakikabiliwa na mashtaka 12 yakiwemo ya utakatishaji fedha lakini mpaka sasa upelelezi haujakamilika.

Tangu wafikishwe mahakamani hapo hadi leo Septemba 26, 2019 wamefikisha siku 828, sawa na miaka miwili na siku 98.

Rugemarila,  ambaye  ni Mkurugenzi wa VIP na mmiliki mwenza wa zamani wa IPTL na Sethi, mwenyekiti mtendaji wa PAP, wanadaiwa kutenda makosa hayo jijini Dar es Salaam, Afrika Kusini, Kenya na India.

Leo upande wa mashtaka umedai kuwa upelelezi wa shauri hilo bado haujakamilika.

Wakili wa Takukuru, Leonard Swai ameieleza mahakama hiyo mbele ya Hakimu Mkazi,  Vicky Mwaikambo,wakati kesi hiyo ilipokuja kwa ajili ya kutajwa.

Hakimu Mwaikambo baada ya kusikiliza maelezo hayo ameahirisha kesi hiyo hadi Oktoba 10, 2019 itakapotajwa na washtakiwa wamerudishwa rumande.

Miongoni mwa mashtaka yanayowakabili washtakiwa hao ni kula njama, kujihusisha mtandao wa uhalifu , kughushi, kutoa nyaraka za kughushi.

Pia wanadaiwa kujipatia fedha kwa njia za udanganyifu, kutakatisha fedha  na kusababisha hasara ya Dola za Marekani 22,198,544.60 na Sh309 bilioni

Katika shtaka la kwanza, washtakiwa wanadaiwa  kati ya Oktoba 18, 2011 na Machi 19, 2014 jijini Dar es Salaam walikula njama ya kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu katika nchi za Afrika Kusini, Kenya na India

Katika shtaka la pili la kujihusisha na mtandao, washtakiwa hao kati ya Oktoba 18, 2011 na Machi 19, 2014 jijini Dar es Salaam wakiwa si watumishi wa umma  walitekeleza mtandao wa uhalifu kwa lengo la kujipatia faida.

Katika shtaka la tatu, Seth anadaiwa  Oktoba 10, 2011 katika mtaa wa Ohio jijini Dar es Salaam, akiwa na nia ya ulaghai alighushi fomu namba 14 ya usajili wa kampuni  na kuonyesha yeye ni Mtanzania anayeishi kiwanja namba 887 mtaa wa Mrikau Masaki wakati akijua ni uongo.