Shambulio la kigaidi laua watu 38 Burkina Faso

Ouagadougou. Shambuliao la kigaidi limeua watu 38 na kujeruhi wengine 63 karibu na mgodi wa dhahabu, waziri wa ulinzi wa Burkina Faso, Moumina Cherif Sy amesema.

Waziri Sy aliyetembelea eneo shambulio lilitokea katika jimbo la mashariki ya mji mkuu wa Ouagadougou amesema maafisa wa uokozi wangali wanawatafuta wachimba migodi wengine ambao bado hawajulikani walipo.

Kampuni ya Canada ya Semafo inayosimamia kazi za mgodi huo, imeeleza kuwa mabasi yake matano yaliyokuwa yanawasafirisha wafanyakazi kuelekea kazini yalishambuliwa na wanamgambo wasiojulikana wa makundi ya wafuasi wa itikadi kali za kidini yanayoendesha shughuli zake kaskazini na mashariki ya Burkina Faso.

Taifa hilo la Afrika Magharibi linalofahamika kwa utulivu, limekuwa likipambana na mashambulizi ya kigaidi yaliyowasababisha maelfu ya watu kukimbia makazi yao tangu mwanzoni mwa mwaka huu.