Sheikh Mkoa wa Dar ataka viongozi wa dini kutoa azimio kumuunga mkono Magufuli

Muktasari:

Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Mussa Salum amewataka viongozi wa dini kutoa azimio la kuunga mkono jitihada zinazofanywa na Rais wa Tanzania, John Magufuli.

Dar es Salaam. Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Mussa Salum amewataka viongozi wa dini kutoa azimio la kuunga mkono jitihada zinazofanywa na Rais wa Tanzania, John Magufuli.

Amesema miaka minne tangu Magufuli alipoapishwa kuwa Rais amefanya mambo makubwa ambayo hawakuyategemea.

Ametoa kauli hiyo leo Jumatatu Novemba 18, 2019 katika mkutano uliotishwa na mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda uliowakutanisha viongozi wa dini kwa ajili ya kuwaeleza utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo tangu kiongozi mkuu huyo wa nchi aingie madarakani.

“Jamani niwaulize wenzangu haya mambo hamjayafurahia? Kama  mmefurahi kwa nini tusitoke na azimio la kumuunga mkono kwa mambo mema aliyotufanyia hapa nchini.”

“Sema tu kuna vitu hatuwezi kusema kwa sababu ya haya mambo ya demokrasia.  Watu tunataka maendeleo, nidhamu kama hii iendelee tatizo ni hizi nchi zetu ukisema kitu utaambiwa demokrasia,” amesema Sheikh Salum.

Wazo la Alhad Salum  limeungwa mkono na Askofu  wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri (KKKT) jimbo la Dar es Salaam,  Alex Malasusa.

“Katika kusimamia jambo kutakuwa na mishale hasa unapolisimamia kwa haki. Tutaendelea kukuombea  na pale tutakapohitaji kushauriana nawe tutafanya hivyo. Tunashukuru kwa kutupa habari maana tutatoka hapa tukiwa na maarifa mengi,” amesema Malasusa.

Malasusa aligusia hatua zilizochukuliwa kukabiliana na matumizi ya dawa za kulevya kwa vijana jijini Dar es Salaam.