Breaking News

VIDEO: Sumaye ang'oka Chadema, amuachia ujumbe Mbowe

Wednesday December 4 2019

By Ibrahim Yamola, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Waziri mkuu mstaafu wa Tanzania, Frederick Sumaye  amesema kuanzia leo Jumatano Desemba 4, 2019 si mwanachama wa Chadema huku akimuachia ujumbe mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe.

Ametoa kauli hiyo katika mkutano wake na waandishi wa habari uliofanyika leo jijini Dar es Salaam. Aliitisha mkutano huo jana Jumanne Desemba 3, 2019 akieleza kuwa atazungumzia masuala ya kisiasa na uchaguzi wa Chadema unaoendelea.

Kutangazwa kwa mkutano huo kuliibua hisia tofauti kutokana na waziri mkuu huyo wa mwaka 1995 hadi 2005 kupigiwa kura 48 za hapana kati ya 76 katika uchaguzi wa uenyekiti wa Chadema Kanda ya Pwani. Kulingana na taratibu za chama hicho uchaguzi huo utarudiwa.

Sumaye amesema kutokana na yaliyomtokea kwenye uchaguzi huo na yeye kuchukua fomu ya kuwania uenyekiti wa Chadema akipambana na Mbowe haoni haja ya kubaki katika chama hicho.

Amesema katika uchaguzi huo wajumbe wa mkutano walishawishiwa na baadhi ya viongozi walioshiriki kumchukulia fomu za kuwania uenyekiti ili asishinde.

“Nimelazimika kwa kulazimishwa kujiondoa Chadema na kuanzia sasa si mwana Chadema na sijiungi na chama chochote cha siasa. Nitakuwa tayari kutumika na chama chochote ikiwamo Chadema.”

Advertisement

"Nawapenda sana wana Chadema nina imani kubwa sana na nyinyi ninawashukuru kwa ushirikiano mlionipa. Najua wengi wataumia lakini sina jinsi, wengi mtaumia kwa viongozi wenu wa kanda waliofanya haya na mimi nimewasamehe," amesema Sumaye

Sumaye amemtaka Mbowe kuunganisha makundi yaliyotokana na uchaguzi wa ndani wa chama hicho utakaohitimishwa Desemba 18, 2019, akibainisha kuwa wanaomzunguka Mbowe wanakiharibu na kukijengea taswira hasi chama hicho.

Advertisement