TANZIA: Injinia Fabiola alivyoacha simanzi

Wednesday March 25 2020

 

By Bakari Kiango, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. “Alikuwa mke mwema, rafiki na mama watoto, ni pigo kubwa kwangu, familia na wanangu,” hayo ni maneno ya Josephat Mushi, mume wa Injinia Fabiola Mushi mwanamke pekee aliyefariki dunia katika ajali ya treni akiwa kazini.

Fabiola (pichani) ni miongoni mwa wafanyakazi watano waandamizi wa Shirika la Reli Tanzania (TRC) waliofariki dunia juzi baada ya treni kugonga kiberenge kati ya stesheni za Mwakiyumbi na Gandagenda katika reli ya Dar –Moshi.

Wafanyakazi wengine waliofariki dunia kutokana na ajali hiyo ni Joseph Komba (meneja msaidizi wa usafirishaji (Kanda ya Dar es Salaam), Philbert Kajuna (mtaalamu wa usalama wa reli), George Urio (dereva wa kiberenge na Ramadhani Gumbo, ambaye ni meneja usafirishaji kanda ya Tanga.

Katika ajali hiyo, wafanyakazi wanne walifariki papo hapo, lakini Kajuna ambaye alikuwa mwanafunzi wa mwaka wa kwanza katika Taasisi ya Teknolojia ya Dar es Salaam (DIT) alifariki akiwa hospitali huku Elizabeth Bona, ambaye ni muongoza treni ndiye majeruhi aliyenusurika katika ajali hiyo.

Mke mwema

Mushi ambaye ni baba wa watoto watatu aliozaa na Fabiola, alisimulia kuhusu mkewe wakati wa shughuli za kuaga miili ya watumishi hao iliyofanyika katika Hospitali ya Jeshi ya Lugalo jijini Dar es Salaam.

Advertisement

Akiwa anatokwa na machozi wakati wa mazungumzo yake na Mwananchi, Mushi alisema, “mke wangu alionyesha njia ya upambanaji katika maisha. Hakuwa mtu wa kuweka kitu rohoni, alikuwa ni mtu wa watu, ni pigo sana kwangu,” alisema Mushi huku akitoa kitambaa mfukoni na kujifuta machozi.

“Fabiola alikuwa anapenda kujiendeleza kielimu, ndiyo maana alifikia mafanikio ya kupata shahada ya uzamili. Ni mtu ambaye alikuwa hakubali kushindwa, akisema jambo fulani anaweza kufanya basi anafanya,” alisimulia.

Maelezo hayo ya Mushi yalifanana na waliokuwa wanafunzi wenzake na Fabiola katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) katika fani ya uhandisi mitambo mwaka 2004 - 2008 walipohitimu.

“Alikuwa ni mchapakazi, anajituma na mtu asiyetishika na kitu, kwangu alikuwa ni mtu anayenivutia darasani. Katika darasa letu tulikuwa wanafunzi 20 kati hao wasichana tulikuwa wawili, mimi na Fabiola.

“Rafiki yangu alikuwa jasiri sana, nilikuwa namtumia kama mwalimu kwa sababu alikuwa mwenye mipango ya muda mrefu. Nakumbuka mwaka 2008 akiwa mjamzito na alipojifungua wiki moja baadaye tulifanya naye mtihani wa mwisho na alipata ufaulu mzuri,” alisema Dk Pendo Bigambo ambaye walisoma pamoja na Fabiola.

Wilbard Gandu alisema Fabiola na Dk Bigambo ni wanawake pekee waliokuwa wakisomea kozi ya uhandisi mitambo chuoni katika darasa la wanaume 18.

“Wanawake hawa waliweza kumudu vyema kozi hizi tukiwa chuoni wakati huo. Ni nadra sana kwa wanawake kusomea kozi hii lakini Fabiola na Dk Pendo waliweza na walifanya vizuri kwenye masomo yao,” alisema Gandu.

Mkurugenzi wa Idara ya Uhandisi na Mitambo wa TRC, Albert Magandi alisema Fabiola ni miongoni mwa wahandisi wanawake waliokuwa na uzoefu mkubwa na alijiunga na shirika hilo mwaka 2008 akitokea chuoni na alikuwa ni mtumishi jasiri kusimamia vyema kazi zake.

Alisema Fabiola alizaliwa Juni 19, 1983 Uru Moshi mkoani Kilimanjaro na mwaka 2016 alihitimu masomo ya Shahada ya Uzamili ya uhandisi mitambo nchini Austria alikokuwa akisoma baada ya kupata ufadhili.

Pigo kubwa

Kaimu mkurugenzi wa uendeshaji wa TRC, Focus Makoye alizungumzia vifo vya wafanyakazi hao kwa mpigo akisema ni pigo kubwa kwa shirika hilo kwa kuwa walikuwa wachapakazi katika utekelezaji wa majukumu yao.

Akimzungumzia Komba wakati akitoa salamu za pole kwa waombolezaji, Makoye alisema mtumishi huyo alikuwa muadilifu na mwenye nidhamu katika utekelezaji wa majukumu na mara kwa mara alionyesha uwezo mkubwa katika utendaji.

“Alikuwa na uwezo mkubwa wa kiungozi, mbunifu na msimamizi bora. TRC imekuwa ikiridhishwa na juhudi za utekelezaji wa majukumu yake,” alisema Makoye.

Mkurugenzi mkuu wa TRC, Masanja Kadogosa alisema katika utumishi wake wa miaka 21 katika shirika hilo hajawahi kuona tukio kama hilo.

Mheshimiwa Naibu Waziri Ujenzi na Uchukuzi, ametuagiza tuunde kamati huru kuchunguza ajali hii.

“Kamati hii itakuwa chini ya Latra (Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri Ardhini) na itafanya kazi kwa siku saba kujua kilichotokea kwa sababu si jambo la kawaida. Latra watasaidiana na watu wengine watakaochukuliwa kutoka sehemu mbalimbali,” alisema Masanja.

Advertisement