Tumuenzi Nyerere kwa kutekeleza aliyoyaagiza

Muktasari:

“Mwalimu Nyerere hadi anafariki hakuwa na mali, lakini tuangalie wagombea wetu hivi sasa wakipata madaraka, baada ya muda mfupi anakuwa na mali ya kufuru, Mwalimu hakuwa hivi,”

“Kiongozi wa kuchaguliwa lazima achaguliwe na watu wenyewe kwa hiyari, kwa uhuru na haki, ama sivyo mtatawaliwa na viongozi madikteta ambao watu watakuwa hawana kauli katika nchi yao wenyewe.”

Hiyo ni nukuu ya hayati Mwalimu Julius Nyerere aliyoinukuu Mwenyekiti wa asasi ya kuenzi fikra sahihi za baba wa Taifa, Dk Muzzamil Kalokola alipozungumza na Mwananchi Jijini Tanga kuhusiana na kumbukizi ya miaka 21 ya Tanzania bila ya Nerere.

Mwenyekiti huyo ambaye amesema alifanya kazi kwa karibu na Mwalimu Nyerere, alisema wakati Watanzania wakimkumbuka katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu, kuna haja ya vyombo vinavyohusika kusimamia uchaguzi, wapiga kura na wagombea kutafakari kwa kina na kufanyia kazi kwa vitendo usia huo wa hayati Nyerere.

Dk Kalokola ambaye pia ni kada wa CCM ambaye alikuwa akizungumzia ni wapi Tanzania ilipojikwaa, alisema baada ya kuzika maelekezo ya azimio la Arusha, mwongozo wa mwaka 1981 wa CCM na kanuni za uchaguzi zilizotumika wakati wa uhai wa Mwalimu Nyerere.

Anasema wakati wa Mwalimu nafasi za kuchaguliwa hazikuwa lele mama kama ilivyo sasa, bali watu walipelekwa vyuoni kupikwa kwanza ndipo wakabidhiwe madaraka.

Anasema hali hiyo ilisaidia kuwa na viongozi waadilifu waliokuwa na hofu ya Mungu na hawakuthubutu kujilimbikizia mali kama ilivyo sasa.

“Lakini baada ya kuzika azimio la Arusha lililoasisiwa na Nyerere kwa madai linaleta mambo ya ujamaa, Bunge na mabaraza ya madiwani yamekuwa kama mahala pa watu kupambania wapate nafasi hizo ili watajirike kwa kupata posho, mishahara mikubwa na kiinua mgongo baada ya muda wao kumalizika.

Dk Kalokola ambaye pia ni mchumi, anasema kwa bahati mbaya wanasiasa wengi hivi sasa hupanda majukwaani kujinadi eti wanamuenzi Nyerere kusudi tu wapate kura za wananchi.

“Lakini ukichunguza kwa kina, hakuna kitu kama hicho,” anasema Dk kalokola.

“Mwalimu Nyerere hadi anafariki hakuwa na mali, lakini tuangalie wagombea wetu hivi sasa wakipata madaraka, baada ya muda mfupi anakuwa na mali ya kufuru, Mwalimu hakuwa hivi,” anasema.

Anasema baadhi ya wanasiasa baada ya Nyerere kufariki dunia, wameliamua kuvunja miiko aliyoiacha ya kukataa raslimali za Taifa kutoroshwa nchi za nje huku Watanzania wakibaki masikini.

“Hata sera ya ubinafsishaji imekuja kuharibu uchumi wa Tanzania kwa sababu wawekezaji wanatumia kanuni ya kupeleka nje fedha za kigeni jambo ambalo ni kosa kubwa kiuchumi kwa sababu mwisho wa yote shilingi yetu inaporomoka,” anasema daktari mchumi huyo.

Anasema Tanzania ilishapata sifa kubwa nje kutokana na msimamo wa baba wa Taifa wa kutokubali ukoloni mamboleo ambao ulirejea Tanzania kwa mlango wa nyuma wa uwekezaji.

Tusikubali muungano uvunjike

Akizungumzia suala la Muungano na namna Mwalimu alivyouasisi, Dk Kalokola anasema alikuwa na maana kubwa.

Hivyo ameasa yeyote atakayefanikiwa kuchukua madaraka Oktoba 28, asithubutu kuuvunja.

Anasema Muungano ndiyo tunu pekee iliyoachwa na Nyerere inayoing’arisha Tanzania dunia.

“Tanzania itafanya kosa kubwa kama itakubali kuuvunja muungano kwa maslahi ya wachache,” alisema.

Anasema hata atakayefanikiwa kuwa Rais baada ya Oktoba 28, asifanye makosa ya kumteua Waziri wa Muungano ambaye atakuwa hana ufahamu mzuri uhusiana na Muungano.

Anasema wizara hiyo ni nyeti anapaswa kuongozwa na waziri mwenye hekima,busara na subira kama alivyokuwa akifanya Mwalimu Nyerere.

Azungumzia Ilani za vyama na sera za uwekezaji nchini.

Kada huyo anasema amefuatilia sera za wagombea urais wote wa Jamahuri ya Muungano wa Tanzania na kusikia wakijinadi kwamba watawaleta wawekezaji kuwekeza katika sekta mbalimbali ikiwamo viwanda.

Anasema kama wanataka kumuenzi baba wa Taifa ni vyema waelekeze nguvu zao katika kuwawezesha Watanzania kujikita kwenye uwekezaji wa sekta mbalimbali vikiwamo viwanda kwa kuwalea na kuwakuza.

“Marehemu Reginald Mengi ni zao la baba wa Taifa kwa sababu aliwezesha vyombo vya fedha kutoa mikopo iliyo na masharti rafiki hatimaye akaibuka kuwa mwekezaji wa ndani katika sekta ya viwanda, madini na tasnia ya habari kupitia kampuni zake za IPP … tupate rais atakayefuata nyayo za baba wa Taifa mwenye sera ya kuwainua wawekezaji wa ndani zaidi kuliko kukaribisha wa nje,” anasema Dk Kalokola.

Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC)

Kada huyo wa CCM ameitaka Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kuacha kushughulika na wagombea wanaokosea kwa namna moja ama nyingine kwenye ujazaji wa fomu badala yake iwaibue na kuwapa adhabu wale wanaojipa sifa zisizo zao za ukweli ili kuwahadaa Watanzania waweze kuwachagua. “NEC inafanya makosa kwa vitu visivyo vya msingi, baba wa Taifa aliruhusu sifa kubwa ya mgombea wa ubunge na udiwani ajue kusoma na kuandika kwa sababu hiyo si ajira bali ni uwakilishi, lakini sasa wapo wagombea ambao wanajipa sifa zisizokuwa zao ili kuwahadaa wakipga kura,” alisema Dk Kalokola.

Anasema anafahamu kwamba NEC imesheheni wataalamu wa sheria lakini anashangaa kuona wanakiuka kifungu namba 107 “A”(2) “E”kinachokataza kutumia mambo ya kiufundi kuwanyima haki wagombea au wapiga kura.