Tundu Lissu ni mwanasiasa wa aina gani?

Mbunge wa Singida Mashariki,Tundu Lissu

Muktasari:

Tundu Lissu ana wasifu mrefu lakini kwa ufupi unaweza kusema ni mwanasiasa na mwanasheria.

Dar es Salaam. Jina la Tundu Lissu kwa kutwa nzima leo Alhamisi limekuwa likisikika kwenye vyombo vya habari na mitandao ya kijamii.

Hilo ni kutokana na Lissu kujeruhiwa kwa risasi nyumbani kwake mjini Dodoma.

Huyu ni Mbunge wa Singida Mashariki kupitia Chadema tangu mwaka 2010.

Mbali na shughuli za siasa, mbunge huyo aliyezaliwa Januari 20, 1968 ni mwanasheria akiwa na shahada mbili za fani hiyo, ya kwanza kutoka Chuo kikuu cha Dar es Salaam na ya pili kutoka Chuo Kikuu cha Warwick, Uingereza.

Kabla ya elimu ya Chuo Kikuu, Lissu alisoma katika Sekondari za Ilboru, Arusha hadi kidato cha nne na Galanos, Tanga kwa kidato cha tano na sita.
Katika taaluma yake ya sheria, amewahi kuwa mwanachama wa Chama cha Wanasheria wa Mazingira (Leat) na kile cha Rasilimali za Dunia (WRI).

Umaarufu wa mbunge huyo ulianzia katika harakati zake za kuwatetea wananchi walioathirika na uwekezaji katika migodi ya madini, suala ambalo lilisababisha mara kadhaa kushtakiwa mahakamani.

Lissu alijiunga na Chadema mwaka 2004 wakati wa harakati za madini katika migodi wilayani Tarime mkoani Mara.

Katika moja ya mahojiano yake na vyombo vya habari alisema aliyempokea Tarime ni Chacha Wangwe, sasa ni marehemu baada ya kumkuta akiwa na kesi 10 za jinai akiwa diwani wa Chadema.

Baada ya hatua hiyo Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alimpigia simu akamwomba amsaidie kisheria kumtetea Wangwe kwa gharama za chama.

Baada ya kushinda kesi hiyo na kuwatoa gerezani watu 366 waliokuwa wanatumikia vifungo, Mbowe alimtaka atafute watu wanasheria wengine ili wajiunge na Chadema, wakati huo yeye alikuwa NCCR-Mageuzi.

Kutokana na harakati za kisheria na kisiasa zinazomfanya apambane na utawala, mara kadhaa mwanasiasa huyo amejikuta mikononi mwa polisi na sasa anakabiliwa na kesi zaidi ya tatu mahakamani.

Hadi sasa ni mwanasheria mkuu wa Chadema na Mnadhimu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni.