Uchaguzi 1970 waja na sura mpya, Mwinyi apewa wizara

Friday March 20 2020

 

By William Shao, Mwananchi

Siku sita baada ya Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 30 mwaka 1970, Rais wa Tanzania, Mwalimu Julius Nyerere, aliteua Baraza jipya la Mawaziri.

Ndani ya Baraza hilo, kulikuwa na sura sita mpya zilizoingia. Mawaziri karibu wote waliokuwa katika baraza lililopita walichaguliwa tena kurejea bungeni na kuteuliwa kuwa mawaziri tena, isipokuwa Stephen Mhando aliyechaguliwa jimboni Tanga.

Mhando alikuwa waziri wa kwanza wa Mambo ya Nje, wizara ambayo iliundwa mwaka 1964.

Mmoja wa mawaziri wapya aliyeteuliwa ni John Mhavile ambaye aliteuliwa kuongoza Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo Mijini.

Mhavile aliyekuwa mzaliwa wa Ilembula wilayani Njombe, alichaguliwa kuwa mbunge wa Njombe Kaskazini. Awali alikuwa Katibu Mkuu wa Vyama vya Ushirika Tanganyika.

Mwingine alikuwa ni Jacob Namfua aliyeteuliwa kuwa Waziri wa Habari na Utangazaji.

Advertisement

Namfua alikuwa mmoja wa mawaziri wapya ambao Mwalimu Nyerere aliwateua kuwa wabunge na kisha akamteua kuwa waziri.

Kabla ya uchaguzi, Waziri Namfua alikuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Uchumi na Mipango ya Maendeleo.

Mwingine mpya alikuwa Dk Wilbert Chagula aliyepewa dhamana ya kuongoza Wizara ya Maendeleo ya Maji na Umeme. Historia inamwelezea Chagula kuwa hadi Julai 1970, alikuwa Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, pia alikuwa mbunge wa kuteuliwa na Rais.

Alizaliwa mwaka 1926 katika Kijiji cha Mondo mkoani Shinyanga, Tanganyika. Miaka miwili baadaye mwaka 1972 aliteuliwa kuwa Waziri wa Uchumi na Mipango ya Maendeleo.

Israel (Isaeli) Elinawinga aliyekuwa mzaliwa wa Hai, Kilimanjaro, aliteuliwa kuwa Waziri wa Nchi, Wizara ya Mambo ya Nje.

Kabla ya wadhifa huo, alikuwa Mkuu wa Chuo cha Tanu cha Kivukoni ambacho baadaye kiliitwa Chuo cha Siasa cha Kivukoni.

Elinawinga aliteuliwa kushika wadhifa wa wizara hiyo na kuchukua nafasi ya Stephen Mhando ambaye kabla ya uchaguzi wa mwaka 1970 ndiye aliyekuwa waziri wa wizara hiyo.

Sheikh Ali Hassan Mwinyi aliteuliwa kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais. Baadaye, katika mabadiliko ya Baraza la Mawaziri la mwaka 1972, Mwinyi aliteuliwa kuwa Waziri wa Afya na baadaye, mwaka 1975 akateuliwa kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani.

Waziri mwingine aliyeteuliwa ni Edward Moringe Sokoine. Uteuzi huo ulikuja baada ya kushinda uchaguzi katika Jimbo la Masai alikopita bila kupingwa. Aliteuliwa kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais.

Kabla ya uteuzi huu, Sokoine alikuwa Waziri Mdogo (Naibu Waziri) wa Mawasiliano, Uchukuzi na Kazi baada ya uteuzi uliofanyika Agosti 1967.

Kwa hiyo, miongoni mwa mawaziri wote wapya walioteuliwa kwenye uteuzi wa Novemba 5, 1970, Jacob Namfua na Dk Wilbert Chagula hawakugombea ubunge kwenye uchaguzi huo wa 1970.

Kwa sababu hiyo, ili waingie katika baraza la mawaziri ilikuwa lazima wateuliwe na Rais wawe wabunge kabla ya kuwa mawaziri.

Katiba ilimpa Rais mamlaka ya kuteua wabunge 10 kuingia katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Wengine wote, isipokuwa Mwinyi ambaye alitoka Zanzibar walichaguliwa kuingia katika Bunge.

Hata hivyo, mawaziri wawili walibadilishiwa wizara zao ambao ni pamoja na Paul Bomani ambaye awali alikuwa Waziri wa Mambo ya Uchumi na Mipango ya Maendeleo, akateuliwa kuwa Waziri wa Biashara na Viwanda.

Alichukua nafasi ya Abdulrahman Babu aliyeteuliwa kuwa Waziri wa Mambo ya Uchumi na Mipango ya Maendeleo.

Mwaka huo ziliundwa pia wizara mbili. Moja ya Wizara ya Maliasili na Utalii ambayo waziri aliyeteuliwa alikuwa Hasnu Mwita.

Nyingine ilikuwa Wizara ya Maendeleo ya Maji na Umeme iliyoongozwa na Dk Chagula.

Baraza zima la mawaziri lililoapishwa Ijumaa ya Novemba 6, 1970 lilikuwa na Makamu wa Kwanza wa Rais, Sheikh Abeid Amani Karume. Mwingine alikuwa ni Makamu wa Pili wa Rais, Rashidi Mfaume Kawawa.

Wengine ni Waziri wa Kilimo na Ushirika, Derek Bryceson. Yeye alikuwa mkulima, lakini awali aliteuliwa kuwa Waziri wa Afya na Masuala ya Wafanyakazi.

Kwa wakati huo alikuwa na umri wa miaka 37. Bryceson aliingia nchini Tanganyika kwa mara ya kwanza mwaka 1952 akitokea Kenya.

Alipata elimu yake katika Chuo Kikuu cha Cambridge nchini Uingereza na alikuwa katika kikosi cha Jeshi la Anga la Uingereza wakati wa Vita Kuu ya II ya Dunia.

Kwa mara ya kwanza aliingia serikalini mwaka 1957 akiwa Waziri Msaidizi wa Kazi za Starehe na baadaye Juni 1959, akawa Waziri wa Machimbo ya Madini na Biashara, mwaka 1960 akaingia katika Serikali ya Mwalimu Nyerere. Tofauti na Wazungu wenzake waliokuwa katika Serikali ya Mwalimu Nyerere, Bryceson alikuwa mjumbe wa kuchaguliwa wa Legco kutoka Dar es Salaam (Kaskazini).

Waziri mwingine aliyeapishwa ni Waziri wa Fedha, Amir Habib Jamal ambaye ni Mhindi pekee aliyekuwa katika Serikali ya kwanza ya Tanganyika, na baadaye Tanzania, na aliendelea kuwapo katika awamu mbalimbali za serikali za Mwalimu Nyerere kwa miaka mingi baada ya Uhuru.

Jamal aliingia katika serikali hiyo ya kwanza akiwa na umri wa miaka 38 akiwa Waziri wa Njia (mawasiliano), Simu na Majengo.

Yeye alizaliwa nchini Tanganyika na kupata elimu yake mkoani Mwanza na Dar es Salaam kabla ya kwenda Chuo Kikuu cha Calcutta nchini India ambako alifuzu masomo ya uchumi mwaka 1958.

Kabla ya kuchaguliwa kuingia serikalini, Jamal alikuwa mfanyabiashara na Mkurugenzi wa Kampuni ya Habib & Company Ltd.

Juni 1959 ndipo alipoingia serikalini kwa mara ya kwanza alipoteuliwa kuwa Waziri wa Tawala za Miji na Majengo katika serikali ya muda ya Tanganyika. Uteuzi huo ulitokana na uchaguzi wa kura tatu mwaka 1958.

Job Malecela Lusinde aliteuliwa kuwa Waziri wa Mawasiliano, Uchukuzi. Awali Lusinde alikuwa Waziri wa Serikali za Mitaa na Utawala.

Aliyeteuliwa kuwa Waziri wa Elimu ya Taifa ni Chedieli Yohane Mgonja, mshindi wa uchaguzi wa ubunge wilaya ya Pare, ambaye kati ya mwaka 1965 na 1967 alikuwa Waziri wa Maendeleo na Utamaduni na ambaye kwa wakati huo aliweka rekodi ya kuwa waziri kijana kuliko wote Tanzania.

Mgonja ambaye mwaka 1967 aliteuliwa kuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Raisi (Mambo ya Nje) na mwaka 1968 akateuliwa kuwa Waziri wa Elimu, alikuwa ndiye Waziri aliyetoa tamko la serikali ya Tanzania kuitambua Jamhuri ya watu wa Biafra iliyojitenga na Nigeria mwishoni mwa miaka ya ‘60.

Hadi wakati wa uchaguzi wa 1970 Mgonja alikuwa Waziri wa Elimu. Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi aliteuliwa Said Ali Maswanya, Mnyamwezi kutoka Tabora. Alichaguliwa kuingia bungeni kupitia Jimbo la Kahama.

Alikuwa waziri wa tano kuteuliwa kushika wadhifa wa Waziri wa Mambo ya Ndani.

Lawi Nangwanda Sijaona aliteuliwa kuwa Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii. Yeye alichaguliwa kuwa mbunge wa Lindi.

Peter Abdallah Kisumo aliteuliwa kuwa Waziri wa Nchi, Wizara ya Tawala za Mikoa na Maendeleo Vijijini.

Aboud Jumbe aliteuliwa kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wakati Edward Moringe Sokoine akiteuliwa kuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais.

Mawaziri wote, isipokuwa Jacob Namfua ambaye alikuwa mkoani Kilimanjaro katika maziko ya ndugu yake, waliapishwa na Rais Nyerere jioni ya Novemba 6, 1970 katika hafla iliyofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam ambayo ilidumu kwa muda usiozidi dakika 45.

Katika hafla hiyo waliapishwa pia Makatibu Wakuu wapya watatu walioteuliwa na Rais. Makatibu hao ni Julius Sepeku, Frederick Lwegarulila na Godfriend Kileo.

Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi, Chifu Adam Sapi Mkwawa na Jaji Mkuu, Philip Telford Georges, ni miongoni mwa waliohudhuria hafla hiyo.

Katika safu hii kesho, tutasoma jinsi Mwalimu Nyerere alichokisema kwa wale waliomnyima kura

Advertisement