Ujenzi barabara ya Makongo Juu, Madale wazinduliwa

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda akizungumza na wakazi wa Makongo Juu katika hafla ya uzinduzi wa barabara ya eneo hilo.

Muktasari:

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Tanzania, Paul Makonda amesema barabara ya Makongo Juu itajengwa kwa kiwango la lami kwa muda wa mwaka mmoja.

Dar es Salaam. Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Tanzania, Paul Makonda amesema barabara ya Makongo Juu itajengwa kwa kiwango la lami kwa muda wa mwaka mmoja.

Mkuu huyo wa Mkoa pia alizindua ujenzi wa barabara ya Madale yenye urefu wa kilomita sita, utakaofanyika kwa mwaka mmoja na nusu, akibainisha kuwa kukamilika kwa ujenzi wa barabara hizo kutaondoa kero kwa wananchi, kupunguza foleni kwenda katikati ya Jiji.

Ujenzi wa barabara ya Makongo Juu yenye urefu wa kilomita 4.5 utagharimu Sh8.9 bilioni zinazojumuisha malipo  fidia na uhamishaji na miundombinu ya maji na umeme.

Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Daniel  Chongolo pamoja na watendaji wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroad) ni miongoni mwa walioshuhudia uzinduzi huo. Kampuni ya Jasco ndio inajenga barabara hiyo.

"Poleni sana wakazi wa Makongo Juu na watumiaji wa barabara hii, sio  kama fedha hazikuwepo ila mlikosa kiongozi mwenye ushawishi na anayejenga hoja, "amesema Makonda.

Awali, Chongolo amesema kwa kipindi kirefu wakazi wa eneo hilo walikuwa wakitaniwa kwenye mitandao ya kijamii  kuwa mtu atakayeonekana na vumbi anatokea Makongo Juu jambo ambalo hivi karibuni litakuwa historia.