VIDEO: Wanafunzi 39 wanusurika baada ya kupigwa na radi

Mwanafunzi wa darasa la nne Shule ya Msingi Ihumilo wilayani Geita akiwa amelazwa katika hospital ya wilaya hiyo Nzera baada ya kupata mshutuko wa radi.

Muktasari:

  • Wanafunzi 39 wa darasa la nne Shule ya Msingi Ihumilo wilayani Geita wamejeruhiwa baada ya kupigwa na radi wakiwa darasani.

Geita. Wanafunzi 39 wa darasa la nne Shule ya Msingi Ihumilo wilayani Geita wamejeruhiwa baada ya kupigwa na radi wakiwa darasani.

Taarifa iliyotolewa leo Ijumaa Oktoba 18, 2019 na  mganga mkuu wa mkoa wa Geita,  Josephat Simeo inaeleza kuwa wanafunzi 24 wamepelekwa katika hospitali ya wilaya ya Nzera na 15 wamepatiwa matibabu katika zahanati ya Nkome.

Dk Simeo amesema radi hiyo imesababisha watoto kupata mshtuko na kuzimia lakini baada ya kupatiwa huduma ya kwanza wanaendelea vizuri na tayari wanafunzi 36 wameruhusiwa kutoka hospitali.

Mganga mfawidhi wa hospitali hiyo, Kaitila Murusuri amesema aliwapokea wanafunzi 24 saa 2 asubuhi kwamba walikuwa wamepata mshtuko, waliwapatia huduma ya kwanza.

“21 kati yao wameruhusiwa kutoka hospitali, watatu ambao hali zao si nzuri wanaendelea na matibabu,” amesema.

Mmoja wa wanafunzi hao, Neema John amesema aliona mwanga mkali ukipiga darasani na hakujua kilichoendelea hadi alipojikuta amelazwa wodini.