VIDEO: Wafungwa 365 waachiwa Morogoro, waeleza walichojifunza

Wednesday December 11 2019

By Lilian Lucas, Mwananchi [email protected]

Morogoro. Wafungwa 365 mkoani Morogoro wakiwemo wanawake watatu wameachiwa huru kwa msamaha wa Rais John Magufuli alioutoa Jumatatu Desemba 9, 2019 katika maadhimisho ya Uhuru wa Tanganyika.

Wafungwa hao ni kati ya 5,533 waliopata msamaha wa Rais Magufuli.

Akizungumza leo Jumatano Desemba 11, 2019 mkuu wa Jeshi la Magereza mkoani Morogoro, Sylivesta Mrema amesema walioachiwa ni waliokuwa wagonjwa, waliokaribia kumaliza vifungo vyao na walioonyesha kujutia makosa waliyoyafanya.

Ametaja Magereza na idadi ya wafungwa walioachiwa ni Kiberege (63), Mahenge (9), Kihonda (49), Mtego wa Simba (31), Kilosa (23), Mbigiri (36), Vijana (10), Wanawake Kingolwira (3), Mkono wa Mara (11), Wami Kuu (26), Idete (57) na gereza la Mahabusu Morogoro (36).

Mkuu wa Gereza la Mahabusu Mkoa wa Morogoro, Zefania Neligwa amesema msamaha huo utasaidia kupungua msongamano wa wafungwa kutokana na kuwepo kwa wafungwa na mahabusu wengi katika gereza hilo.

Baadhi ya wafungwa walimshukuru Rais Magufuli kwa kutoa msamaha huo, wakibainisha kuwa mafunzo waliyoyapata walipokuwa gerezani watayatumia uraiani.

Advertisement

Josam Gabriel  amesema wakati akitumikia kifungo alijifunza ufundi ujenzi na upishi.

“Kiukweli siwezi kusema nimetoka bure nilikuwa fundi ujenzi, nilipokuwa gerezani nimeongeza ujuzi zaidi, nina imani nitaenda kuwa balozi mwema, ninachowaomba wenzangu tusiende kurudia yale tuliyoyafanya awali,” amesema Steven Chambo.

Advertisement