RIPOTI MAALUMU: Wahadzabe waomba Katiba itamke kuhusu mahitaji yao-2

Muktasari:

Katika toleo lililopita tuliona jinsi jamii ya Wahadzabe inavyonufaika kwa kutunza mazingira na kutumia fedha wanazozipata kwa elimu na afya huku wakiwa na utaratibu wa kulinda misitu yao. Endelea...

Pili Goodo, mratibu wa vijana wa ulinzi wa jamii ya Wahadzabe anasema ili kusimamia maeneo ya misitu yasiharibiwe askari wa vijiji walitafutwa.

“Hawa kazi yao ni kuangalia ‘beacon’ zisiharibiwe, miti isikatwe, kupambana na majangili,” anasema na kuongeza kuwa kila askari hulipwa Sh80,000 kwa mwezi kwa kazi hii ya kulinda misitu.

Mwenyekiti wa Bodi ya Elimu wa Wahadzabe, Ezekiel Philipo anasema asilimia 25 ya fedha (sawa na Tsh4milioni kila baada ya miezi sita) huwekwa kwenye elimu.

“Yaani kutokana na huu utunzaji wetu wa misitu, sasa watoto wa Kihadzabe wanasoma bure, kuanzia shule ya msingi na hata wanapoingia sekondari wanapewa mahitaji muhimu,” anasema.

Anasema fedha hizo zinawasaidia wanafunzi kupanga vyumba karibu na shule, kununua vitanda, magodoro na kujikimu kwa chakula. “Wakati mwingine zinatumika kujenga vyumba vya madarasa na kusaidia masuala mengine ya elimu,” anasema Philipo.

Mkurugenzi wa halmashauri ya Mbulu, Hudson Kamoga anawashukuru watu wa Carbon kwa kuwapa elimu jamii ya Wahadzabe kutunza misitu na kufaidika na mamilioni hayo kila mwaka.

Anasema kuna kiasi cha fedha kinachotengwa kwa ajili ya shughuli za utunzaji wa misitu zinazofanywa na halmashauri hiyo.

Mwanafunzi wa sekondari

Ni saa tatu asubuhi, nipo Kijiji cha Domanga, Kata ya Yaeda Chini wilayani Mbulu, jua likiwa kali na joto kiasi, naingia katika familia ya mtoto wa miaka 15, Paulo Simon.

Ananikaribisha katika makazi yao, yenye nyumba tatu; mbili zilizoezekwa kwa nyasi juu mpaka chini na moja imejengwa kwa udongo na kuezekwa kwa nyasi.

Paulo, mwanafunzi wa kidato cha kwanza wa sekondari ya Yaeda Chini yupo likizo fupi ya mwezi wa tisa na ndiyo maana nimebahatika kumkuta nyumbani.

Ananitambulisha familia yao ya watu tisa, mama yake, bibi yake na ndugu zake sita.

Paulo ni mtoto pekee anayesoma katika familia yao, anasema anajiona mwenye bahati kwa sababu kwa jamii ya Wahadzabe ni nadra kusoma.“Nilisomeshwa shule ya msingi na Kanisa la Tanzania Assemblies of God (TAG) walikuja na kutufanyia usaili, kisha nikachaguliwa na kwenda kusoma Moshi, (Moshi International School),” anasema na kuongeza kuwa alipomaliza shule ya msingi, alichaguliwa sekondari ya Yaeda Chini na kuanza kidato cha kwanza mwaka huu.

Kijana huyo anayeishi katika mazingira ya kimaskini, nguo zake zikiwa zimechanika alikuwa akizungumza kwa Kiingereza wakati wote wa mazungumzo yetu.

Licha ya hali yake ngumu kiuchumi, Paulo anayepata huduma za elimu kutokana na fungu linalotengwa kutoka katika mradi wa uhifadhi mazingira unaotekelezwa na kampuni ya Carbon Tanzania, alishika nafasi ya kwanza kati ya wanafunzi 53 katika mtihani wake wa muhula wa kwanza.

Paulo, ambaye anatamani kuwa daktari wa moyo atakapomaliza masomo ana ujumbe kwa Rais wa Tanzania Dk John Magufuli. “Ninajua kuwa Rais wa nchi hii ni Magufuli, tunaomba akipata muda aje atutembelee na kusikiliza shida za Wahadzabe.”

Paulo anasema anafahamu kuwa Rais Magufuli ana mambo mengi lakini anatamani japo afike eneo hilo na kusikiliza shida zao na kujionea kwa macho yake mazingira yao. “Hata mtoto mdogo kama mimi najua kuwa Carbon inaratibu sisi kupata fedha ambazo ndizo tunatumia katika elimu na afya, lakini tungependa tumwambie mambo yetu mengine Rais,” anasema.

Paulo anasema ndoto yake ni kuwa daktari wa moyo na kuwahudumia watu wa jamii ya Wahadzabe.

Si Paulo pake yake anayetaka kumuona Rais Magufuli akitembelea jamii ya Wahadzabe, hata Pachal Greyson na mlinzi wa jadi wa eneo la Domanga alikuwa na haya kwa Rais.

“Rais afike hapa ajionee jinsi hali ya jamii ya Wahadzabe ilivyo. Sisi tunaishi katika mazingira hatarishi,” anasema.

Paschal anasema anapokuwa doria, mara kadhaa hunusurika kushambuliwa na majangili wanaowinda katika maeneo hayo.

“Silaha tunazotumia ni za jadi tunazotengeneza wenyewe, yaani upinde na mshale, wakati majangili wanatumia bunduki, baruti, tochi na filimbi kufanya ujangili,” anasema.

Paschal, ambaye ni askari wa doria chini ya mradi wa Carbon wa kuhifadhi mazingira anasema mara kadhaa wanawaacha majangili wafanye uharibifu kwa sababu wanashindwa kuwamudu.

“Siwezi kupambana na jangili mwenye bunduki wakati mimi nina mshale,” anasema.

Anasema wanatumia mbinu nyingi kuua wanyama kama twiga, pofu na swala, kwa mfano wanatumia filimbi na tochi yenye mwanga mkali kuwachanganya wanyama na kisha kuwakata kwa panga.

Paschal anaongeza kuwa wakati mwingine majangili wanaweka sumu kwenye maji ili wanyama wakija kunywa wafe.

“Hii ni hatari hata kwetu sisi Wahadzabe kwa sababu tunategemea maji hayohayo wanayotumia wanyama,” anasema.

Paschal anasema mradi wa Carbon unawawezesha vijana kufanya doria ili kuangalia iwapo kuna uharibifu wa mazingira ikiwamo kukatwa misitu na baadaye kutoa taarifa katika serikali ya kijiji.

“Mara kadhaa tunawatisha majangili wanaovamia misitu na kuua wanyama, lakini wakati mwingine wanatuzidi nguvu na tunawaacha wakiondoka na mnyama,” anasema.

Paschal ni mmoja wa vijana wengine 42 walioajiriwa kama askari wa doria wa uhifadhi wa mazingira katika vijiji vitatu vya Domanga, Yaeda Chini na Mongo wa Mono.

Mwingine anaibuka na kitu kipya kabisa, anazungumzia Katiba.

Pili Goodo, mratibu wa askari wa jadi katika Kijiji cha Domanga anamuomba Rais Magufuli abadili Katiba ya nchi na itamke wazi kuhusu mahitaji ya Wahadzabe.

“Tayari tuna haki miliki ya kimila ya kumiliki ardhi yetu ya Wahadzabe ambayo tuliipata tarehe 18/10/2019, kwa hiyo tuna haki ya kulinda mazingira yetu,” anasema.

Anasema The Nature Conservancy ndiyo waliwasaidia kupata hati ya kimila ya ardhi yao.

“Lakini tunataka tupate mwakilishi ambaye atawasilisha mahitaji yetu bungeni,” anasema.

Pili anasema wanafahamu yupo mbunge wa eneo hilo, lakini akiwepo mwakilishi wa Wahadzabe atawasilisha mahitaji yao kwani inaonekana wamesahaulika kabisa.

“Sisi Wahadzabe tunaelekea kutoweka, tunategemea matunda, mizizi na asali na wanyama wa porini kama vyakula vyetu vikuu, lakini hivi vitu sasa vinapotea? Sisi pia tunapotea?” anasema

Mradi wa uhifadhi wa mazingira unaowapatia mamilioni jamii ya Wahadzabe unafanya kazi katika eneo la hekta 32,000 na umezuia ukataji wa miti zaidi ya 18,700.

Itaendelea