Wanaopanga kwenda Zanzibar waombwa wabaki waliko, mgonjwa mwingine wa corona abainika

Muktasari:

Waziri wa Afya Zanzibar, Hamad Rashid amewaomba watu wanaopanga kwenda  Zanzibar baada ya siku tatu kuanzia leo Jumatano Machi 25, 2020 wapumzike walipo ili kuepuka maambukizi ya virusi vya corona.
 

Dar es Salaam. Waziri wa Afya Zanzibar, Hamad Rashid amewaomba watu wanaopanga kwenda  Zanzibar baada ya siku tatu kuanzia leo Jumatano Machi 25, 2020 wapumzike walipo ili kuepuka maambukizi ya virusi vya corona.

Akizungumza na Mwananchi leo Rashid amesema, “nimewaomba ndugu zetu Wazanzibar na wageni baada ya siku tatu kuanzia sasa wapumzike walipo mpaka hali yetu itakapokuwa nzuri lakini hatujazuia ndege wala boti hata usafiri wa ndani.”

Amesema kwa sasa watu wanaoingia Zanzibar wanafikia katika karantini kwa gharama zao wenyewe, “watu 134 wameingia Zanzibar wapo mahotelini na majumbani na wengine zaidi ya 1,000 walitoka Kenya tunawachunguza hali zao. Kuna mtu mmoja tunamfanyia uchunguzi Pemba.”

“Anayetaka kuja siku tatu hizi aje ila atakaa karantini na baadaye atakwenda mtaani. Kila siku tunakutana lakini  baada ya siku tatu kupita tutatoa taarifa nyingine. Kila Alhamisi na Jumatatu huwa tunatoa taarifa kuhusu corona.”

Amesisitiza kuwa baada ya siku tatu watatoa maelekezo kuhusu hatua zaidi zitakazochukuliwa.

Hamad amesema mgonjwa mwingine wa corona amebainika visiwani humo na kufanya idadi yao kufikia wawili.

Amebainisha kuwa mgonjwa huyo ni mke wa mgonjwa wa kwanza wa corona kisiwani humo.