Wapinzani ‘watilia shaka’ milioni 19 kujiandikisha uchaguzi Serikali za mitaa

Monday October 21 2019

 

By Waandishi Wetu, Mwananchi [email protected]

Dodoma/Dar. Siku mbili baada ya Serikali kutangaza kuwa wananchi milioni 19.6 wamejiandikisha katika daftari la wapiga kura kwa ajili ya kushiriki uchaguzi wa Serikali za Mitaa, yameibuka maoni tofauti kuhusu idadi hiyo iliyotangazwa.

Wakati baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa nchini wametilia shaka idadi hiyo, wengine wamesema siku tatu zilizoongezwa zilichangia kwa kiasi kikubwa idadi hiyo kuongezeka.

Wakizungumza na Mwananchi jana kuhusu idadi ya wananchi hao watakaoshiriki uchaguzi huo utakaofanyika Novemba 24, baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa vya upinzani wamesema takwimu hizo haziendani na kasi ya uandikishaji kwa maelezo kuwa mwitikio wa wananchi ulikuwa mdogo.

Awali uandikishaji wapiga kura ulianza nchini kote Oktoba 8 na kupangwa kufanyika kwa siku saba, lakini ulimalizika Oktoba 17 baada ya Waziri wa Tamisemi, Seleman Jafo kuongeza muda wa siku tatu.

Wakati baadhi ya viongozi hao wa vyama vya upinzani wakiwa na shaka na takwimu hizo, Waziri Jafo amesema hakuna takwimu za kupikwa kwa sababu zilikusanywa katika vituo vya uandikishaji na kulikuwa na mawakala wa vyama vya siasa waliokuwa wakisimamia kazi hiyo.

Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Vincent Mashinji alisema jana kuwa haiamini idadi hiyo kuwa ndiyo waliojiandikisha kwa sababu haiendani na hali halisi ya jinsi kazi hiyo ilivyoendeshwa.

Advertisement

“Sio kweli hapakuwa na mwamko mkubwa wa kujiandikisha, kama Tume yaTaifa ya Uchaguzi yenyewe hadi sasa ina watu milioni 22 waliojiandikisha, wao wamefikiaje idadi hiyo? Hiyo ni kufurahisha watu na kuvuruga uchaguzi, shughuli za uandikishaji hazijaendana na mazingira husika,” alisema Dk Mashinji.

Si yeye tu aliyekuwa na shaka kwani CUF nao walikuwa na mtazamo kama huo.

Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uenezi wa CUF, Abdul Kambaya alisema takwimu hizo hawawezi kuziamini moja kwa moja kutokana na mazingira ya uandikishaji yalivyokuwa.

Alisema kinachowapa shaka ni baada ya kukataliwa mawakala wao kuwepo katika vituo vya kujiandikisha ili waweze kuona idadi ya watu.

“Hiyo idadi ni namba tu, hali halisi ilikuwa inaonekana na ndiyo maana waliongeza hizi siku tatu, sisi hiyo idadi waliyotaja kwa kweli hatuna imani nayo,” alisema Kambaya.

Lakini si kila mmoja aliyekuwa na mtazamo huo, kuna waliozungumzia umuhimu wa uchaguzi huo.

Makamu Mwenyekiti wa Taifa wa Chauma, Kayombo Kabutale alisema ukombozi unaanzia katika Serikali za Mitaa, vitongoji na vijiji, hivyo ni muhimu watu wengi kujitokeza kujiandikisha, kupiga kura na kugombea nafasi mbalimbali za uongozi.

“CCM ni watu wa kupika sana takwimu, kama ni kweli waliojiandikisha ndio hao basi vizuri. Ingawa tuliwaona waandikishaji wanawafuata watu mitaani kujiandikisha,” alidai Kabutale.

Alisema viongozi wa ngazi ya serikali za mitaa na vitongoji ni muhimu katika Taifa kwa sababu wanaishi karibu na watu na hivyo inarahisisha mawasiliano kwao.

Mwenyekiti wa chama cha NLD, Tozi Matangwa alidai idadi ya watu waliojiandikisha iliongezeka kutokana na wafanyakazi kushinikizwa kujiandikisha na kupiga kura kwa kuhofia wasipofanya hivyo wangepoteza ajira zao.

“Hivi karibuni Rais aliwaonya watendaji, ambao maeneo yao wamejiandikisha watu wachache kuwa atawachukulia hatua kali, matokeo yake kila kiongozi alianza kushinikiza wafanyakazi kujiandikisha, ambao walikuwa wanahofia kupoteza ajira zao na ndio maana imepatikana idadi ya waliojiandikisha 19 milioni wanayodai,” alisema.

“Ninawaomba wananchi waende wakapige kura wasikatishwe tamaa na shinikizo mbalimbali bali wachague viongozi wanaowataka.

“Naiomba serikali wasiwashinikize watu kupiga kura, nchi yetu inaendeshwa kwa demokrasia, unapomlazimisha mtu anakata tamaa matokeo yake siku ya kupiga kura watakaojitokeza ni wachache,” alisema Matangwa.

Mkurugenzi wa Mambo ya Nje, Itifaki na Mawasiliano wa Chadema, John Mrema alisema jambo la kwanza wanatakiwa kuweka majina hadharani kwenye vituo ili waone idadi ya watu 19 milioni.

Alisema idadi ya watu 19 milioni waliojiandikisha wanataka kuiona kwenye kupiga kura na pia Serikali iwaeleze wananchi imekusanya vipi hadi kupata hiyo takwimu kwa kuwa siku tatu walizoongeza wananchi wajiandikishe ni vigumu kupata idadi hiyo kutokana na maeneo mengine kwenye vitongoji kutokuwa na simu wala intaneti.

Mrema alidai wana mashaka na takwimu hizo ukizingatia kuwa hivi karibuni Waziri wa Tamisemi, Jafo alisema kuwa Mkoa wa Dar es Salaam waliojiandikisha ni asilimia sita na alitolea mfano kwenye mtaa wake waliofikia umri wa kujiandikisha ni 6,552 na waliokuwa wamejiandikisha walikuwa 1,400.

“Wanaposema Mkoa wa Dar es Salaam waliojiandikisha ni asilimia 84 wametoa wapi kama mtaani kwangu waliojiandikisha ni idadi ndogo sana, kwenye mitaa mingine najua itakuwa hivyo hivyo,” alisema Mrema.

Alisema takwimu za serikali tuna mashaka nazo hivyo tunaomba waweke takwimu zilizo sahihi.

Kwa upande wake, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama cha Mapinduzi, (NEC) Angela Akilimali alisema idadi hiyo iliyotangazwa na Waziri Jafo ni sahihi japo lengo ilikuwa kufikisha watu 22 milioni.

“Kwa idadi hiyo tumepiga hatua kwa sababu tumefikisha asilimia 85 wakati uandikishaji uliopita tulikuwa na asilimia 65 pekee ya Watanzania waliojiandikisha kwa hiyo ni mafanikio makubwa,” alisema.

Habari imeandikwa na Sharon Sauwa, Pamela Chilongola na Asna Kaniki

Advertisement