Waziri Biteko akabidhi leseni 11 vikundi 10 vya wachimba dhahabu Wilayani Nzega

Waziri wa Madini, Doto Biteko akikabidhi leseni ya uchimbaji madini ya dhahabu kwa mwakilishi wa moja ya vikundi 10 vilivyo kabidhiwa leseni.

 


Muktasari:

Waziri Biteko ajigamba kufanya kazi na kuongeza mapato ya madini bila kupiga kelele, asema hatokubaliana na mtu atakayejaribu kurudisha  nyuma kasi yake.

Nzega. Waziri wa Madini Doto Biteko amesema ataendelea kuzungumza kwa namba (takwimu) badala ya maneno huku akitamba kuwa wizara yake itavuka malengo ya makadirio ya makusanyo ya fedha zilizopangiwa na wizara yake kukusanya ambayo ni Sh475 bilioni katika mwaka wa 2019/20.

Waziri huyo ameeleza kuwa dalili za kufikia lengo hilo zimeshaonekana kufuatia kukusanya Sh205 bilioni kwa kipindi cha miezi mitano.

Biteko aliyasema hayo wilayani Nzega wakati akikabidhi  leseni 11 kwa vikundi 10 vya wachimbaji wadogo wa madini ya dhahabu.

Biteko amesema uthubutu wake na viongozi wenzake wa wizara nzima ndio unaopelekea kuiweka sekta ya madini kwenda mwendo mdundo  huku akiahidi yeyote anayetaka kurudisha nyuma mwendo huo hatokubaliana nae.

 “Madini haya si yangu mimi wala ya Rais John Magufuli, ni madini ya Watanzania na sote tunawajibu wa kuyalinda, kazi yangu ni kusimamia maekezo ninayopewa na rais  ni  kuhakikisha sekta hii inachangia kwenye pato la taifa kama inavyostahili.

“Narudia tena, anae stahili sifa katika haya yote yanayofanyika kwenye madini sio Mimi Doto Biteko, anaye stahili sifa na pongezi zote ni Rais John Pombe Magufuli kwani yeye ndiye anaye elekeza na mimi ni msimamizi tuu wa kutekeleza yale anayo yaagiza.”. amesema Biteko.

Biteko amesema amekuwa akipata simu kadhaa za wananchi wakimpa taarifa za utoroshaji wa madini lakini huwa anachukizwa  na vitendo vya uchonganishi kutokana na baadhi ya watu kutoa taarifa za uongo.

Katika hafla hiyo Biteko alikabidhi leseni kwa vikundi 10 ambavyo ni  Msilale Miners Group, Jimbo la Nzega Vijijini, Undomo Miners Group, Hapa Kwetu Group, Umoja wa Wachimbaji Mwanshina, Mkombozi Mining Group, Imalamakoye Miners Group, Salama Miners, Makalanga Minerals Group na Nzega Miners Association.