Waziri Lugola amtaka RPC mpya wa Morogoro kurudi haraka Kilimanjaro

Sunday September 22 2019

 

By Habel Chidawali,Mwananchi

Dodoma. WAZIRI wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola amemwagiza Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro,Hamis Issah kurudi Mkoani Kilimanjaro ili akamtoe mahabusu Hemed Mbaga ambaye yuko mahabusu kutokana na kubambikiziwa kesi.

Aidha amemwagiza OCD wa Dodoma Mjini, Joas Steven kumpa orodha ya askari ambao wamekuwa wakiwabakizia kesi madereva  bodaboda na bajaji wa Dodoma ili aanze kushughuka nao.

Lugola ametoa agizo hilo leo Septemba 22,2019 katika bonanza lilofanyika uwanja wa shule ya msingi Chang'ombe jijini Dodoma baada ya  kukutana na waendesha bodaboda na bajaji ili kusikiliza kero zao.

Bonanza hilo limeandaliwa na Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) Mkoa wa Dodoma na kushirikisha umati wa watu wakiwemo viongozi na wabunge.

Waziri Lugola amesema Julai  18,2019 Polisi mkoani Kilimanjaro walimkamata Mbaga wakati alipokwenda kuangalia mkusanyiko wa watu kufuatia bodaboda wawili kutelekeza fulushi la bangi.

"Maofisa wa halmashauri walikuwa wanapita hapo kuelekea kwenye makusanyo lakini walikuwa wa kwanza kufika na ndipo Mbaga akaja akitokea nyumbani lakini cha ajabu wakambambikiza kesi na kumweka mahabusu hadi leo," amesema Lugola.

Advertisement

Kwa mujibu wa Waziri, taarifa zilimfikia na akaagiza mtuhumiwa atolewe haraka mahabusu lakini cha ajabu hadi jana alikuwa hajatolewa huku RPC akihamishiwa Morogoro.

Amesema hatavumilia kuona mtu  anashindwa kutimiza wajibu wake wakati Watanzania wanyonge wanaendelea kuumizwa  na polisi wasiowaadilifu na wala rushwa.

"Lakini naagiza kuwa polisi waliohusika wachukuliwe hatua kali bila kuoneana aibu na taarifa nipewe ndipo Kamanda huyu aende katika mkoa aliopangiwa sasa," amesema

Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini,Anthony Mavunde amesema mkoani Dodoma kuna bodaboda wanakamatwa na Polisi wakiwa katika vituo vyao vya kazi na kubambikiziwa kesi bila sababu za msingi na kumwomba Waziri kuingilia kati.

Advertisement