Biashara ya kimataifa yaimarika zaidi Tanzania

Wakati biashara baina ya mataifa ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ikipanda na kufika thamani ya dola 10.17 bilioni (zaidi ya Sh23.59 trilioni) Septemba 2022, mauzo ya bidhaa na huduma za Tanzania nje ya nchi nayo yameongezeka mpaka dola 11.94 bilioni (Sh27.7 trilioni) yakilinganishwa na dola 9.73 bilioni (Sh22.58 trilioni) za mwaka ulioishia Novemba 2021.

Taarifa ya tathmini ya kila mwezi ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kwa mwaka ulioishia Novemba 2022, inaonyesha mauzo ya nje ya huduma na bidhaa yalifika dola 11.94 bilioni (Sh27.7 trilioni) yakilinganishwa na dola 9.73 bilioni (Sh22.58 trilioni) za mwaka ulioishia Novemba 2021.

Ongezeko hili la mauzo lililoshuhudia yale ya bidhaa yakipanda kwa asilimia 7.5 na kufika dola 7.24 bilioni yanaelezwa kuchangiwa zaidi na bidhaa zisizo za kilimo.

Katika kipindi hicho, BoT inasema mauzo ya bidhaa hizo zinazojumuisha makaa ya mawe, almasi, chuma na bati, nguo, mbolea na samaki na bidhaa zake, yaliongezeka kwa asilimia 5.7.

Kati ya bidhaa zilizofanya vizuri sana katika kipindi hicho ni makaa ya mawe ambayo mauzo yake yalipanda kutoka dola 13.2 milioni (Sh30.62 bilioni) mpaka dola 141.6 milioni (Sh328.51 bilioni) sawa na ongezeko la asilimia 1,073 katika kipindi hicho.

“Kuimarika kwa usafirishaji wa makaa ya mawe kulitokana na ongezeko la mahitaji ya vyanzo mbadala vya nishati kutokana na kupungua kwa usambazaji wa mafuta ghafi na gesi asilia kulikosababishwa na vita vinavyoendelea nchini Ukraine,” inasema ripoti hiyo.

Sehemu kubwa ya makaa hayo ya mawe, BoT inasema yaliuzwa katika mataifa ya Kenya, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Rwanda na Uganda. Mengine ni Poland, Hong Kong, India na Senegal.

Mauzo mengine mazuri yalikuwa ya almasi yaliyofika dola 63.1 milioni (Sh146.39 bilioni) kutoka dola 8.4 milioni (Sh19.48 bilioni) sawa na asilimia 751 yakichangiwa na kufufuka kwa uzalishaji katika Mgodi wa Williamson Mines maarufu kama Mwadui baada ya kukamilika kwa ukarabati uliofanywa.

Licha ya madini hayo kufanya vizuri katika kipindi hicho, dhahabu ambayo mauzo yake hayakuongezeka kwa kiasi kikubwa, iliendelea kuchangia sehemu kubwa zaidi ya mauzo ya nje. Katika kiasi kilichopatikana, mauzo ya dhahabu yalifika dola 2.82 bilioni (Sh6.54 trilioni), sawa na asilimia 46.5 ya mauzo yote. Mauzo ya dhahabu yalipanda kutoka dola 2.81 bilioni (Sh6.51 trilioni).

Usafirishaji wa mazao katika kipindi hicho uliliingizia Taifa dola 760.9 milioni zilizoongezeka kutoka dola 628.8 milioni zilizopatikana mwaka 2021, yakichangiwa zaidi na korosho, pamba, katani na tumbaku.


Utalii juu

Kwa miaka mitatu mfululizo kabla ya kuibuka kwa janga la Uviko-19, idadi ya watalii wanaoitembelea Tanzania ilikuwa ikiongezeka mpaka kufika 1,510,151 mwaka 2019, lakini ikaporomoka kwa kasi kuanzia mwaka 2020.

Taarifa za BoT zinaonyesha Desemba ndio mwezi ambao Tanzania ilipokea watalii wengi zaidi mwaka huo, walikuwa 160,296. Mwaka 2020 watalii walipungua mpaka 620,867, kisha wakaanza kuongezeka tena na mpaka Novemba mwaka jana, wakafika 1,412,060, idadi karibu na kabla ya Uviko-19.

Sekta ya huduma, BoT inasema ililiingizia Taifa dola 4.24 bilioni Novemba 2019 (Sh9.83 trilioni) ambazo zilipungua mpaka dola 2.54 bilioni (Sh5.89 trilioni) mwaka 2020 kutokana na kupungua kwa watalii.

Mwaka huo, watalii walipungua kwa asilimia 53.5 hivyo kuchangia dola 1.2 bilioni kutokana na hatua zilizochukuliwa na mataifa mengi duniani kufunga usafiri wa anga ili kuzuia maambukizi ya Uviko-19.

Kwa mwaka ulioishia Novemba 2019, Tanzania iliingiza dola 2.51 bilioni (Sh5.82 trilioni), kiasi ambacho kimekaribiwa Novemba 2022 kikifika dola 2.44 bilioni (Sh5.66 trilioni), kikiongezeka takriban mara mbili kutoka mwaka 2021. Mwaka jana, watalii waliongezeka kwa asilimia 53.4, takriban sawa na waliopungua mwaka 2020 kutokana na korona.

Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Humphrey Mushi anasema ni habari njema biashara kuimarika baada ya kuathiriwa na korona kwa takriban miaka minne sasa.

“Ili kubaki katika mstari huo na kupanda zaidi, tunahitaji kuboresha bidhaa zetu na kupunguza gharama za uzalishaji ili vitu tunavyouza nje ya nchi viwe kwenye ushindani,” anashauri Profesa Mushi.

Vilevile, anasema itapendeza iwapo wigo wa bidhaa zinazopelekwa nje utatanuliwa, kwani nchi inapokuwa na vitu vingi vya kuuza ni jambo muhimu, kwani itaweza kustahimili changamoto zitakazojitokeza wakati wowote.

Naye Profesa Haji Semboja wa Chuo Kikuu cha Zanzibar (Suza) anasema tunapaswa kuboresha mifumo ya uzalishaji wa bidhaa.

“Uamuzi ya wawekezaji kuwekeza hutegemea mazingira ya biashara. Kutokuwapo kwa sera za kueleweka za kuwavutia wawekezaji inaweza kuondoa imani yao ya kuwekeza katika nchi hivyo ni muhimu Tanzania ikajiweka vizuri,” anasema.


EAC nako safi

Taarifa iliyotolewa na EAC wiki iliyopita inaonyesha biashara kati ya nchi saba zinazounda EAC imekuwa ikiimarika mwaka hadi mwaka, hali inayochangiwa na kupunguzwa kwa vikwazo vilivyokuwapo.

Kwenye taarifa hiyo, Katibu Mkuu wa EAC, Dk Peter Mathuki amesema mwaka 2019, biashara kati ya mataifa hayo ilikua kwa asilimia 13 na kufika dola 7.1 bilioni (Sh16.47 trilioni), halafu asilimia 15 mwaka 2021 ikiwa na thamani ya dola 9.5 bilioni (Sh22.04 trilioni kabla haijaongezeka mpaka dola 10.17 Septemba mwaka jana sawa na kukua kwa asilimia 20.

Dk Mathuki anasema ufanisi huo umetokana na utayari wa kisiasa miongoni mwa wanachama na kupunguzwa kwa vikwazo vilivyowekwa kukabiliana na janga la Uviko-19 pamoja na makubaliano ya wakuu wa nchi kuondoa vikwazo visivyo vya kikodi, hatua anazoamini zitasaidia kukuza biashara kwa asilimia 40 ndani ya miaka mitano ijayo.

“Jumla ya vikwazo 257 vya biashara vimeondolewa tangu mwaka 2007, hivyo kuongeza biashara ndani ya jumuiya. Bidhaa zilizotengenezwa ndani ya jumuiya zikiwamo samani, nyama na nguo zinatozwa ushuru wa forodha asilimia 35 tangu Julai mosi 2022 ili kuhamasisha uzalishaji wa ndani,” amesema Dk Mathuki.

Katika kipindi hicho, nchi wanachama wa EAC ziliuza bidhaa na huduma zenye thamani ya dola 62 bilioni (Sh143.84 trilioni) duniani kote, huku asilimia 16.4 ikiwa ni baina yao mwenyewe.

Akieleza namna Tanzania inavyoweza kunufaika zaidi na soko la EAC, Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Wanawake Wafanyabiashara Tanzania (TWCC), Mwajuma Hamza anasema ni muhimu wafanyabiashara wakahakikisha wanawekeza kwenye uzalishaji wa bidhaa nyingi kwa ubora unaohitajika.

“Biashara imeongezeka kutokana na mazingira wezeshi, Serikali imeboresha mazingira kati yake na nchi wanachama wa EAC ili tunufaike zaidi na soko hili,” anasema Mwajuma.

Anasema Rais Samia Suluhu Hassan amekuwa akiimarisha mazingira ya biashara kwa kuondoa changamoto kati ya Tanzania na Kenya pamoja na mataifa mengine wanachama.

Mhadhiri Msaidizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Domminic Lukiko anasema Tanzania inaweza kunufaika na soko la EAC kwa kujihakikishia nafasi ya msingi kwenye soko hilo.

“Tuwe na vitu vya msingi tusiruhusu kila kitu kuingia nchini, tunapaswa kuwezeshana kuhakikisha tunazalisha na kusafirisha kwa wingi, hapo ndipo tunapata nafasi nzuri zaidi kwa sababu tutapata fedha za kuwanyanyua watu wetu,” anasema.

Kutokana na nchi nyingi kutojitegemea kwa chakula, Lukiko anasema Tanzania ina nafasi ya kuongeza nguvu kwenye kilimo ili kunufaika zaidi.

Naye Dk Aidan Msafiri ambaye ni mdau wa maendeleo anasema Tanzania italiteka soko la EAC kama kutakuwa hamasa ya kuzalisha na kuuza bidhaa zenye ubora.

“Watu wanapaswa kuelewa uchumi wao upo mikononi mwao na sio kwa Serikali inayotakiwa kujenga mazingira wezeshi, hivyo wabadilike na kuchangamkia fursa,” anasema mchumi huyo.

Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), Dk Yohana Lawi anasema ingizo la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na Sudan Kusini limechangia kuongeza biashara katika mataifa haya.

Mbali na hayo, amegusia suala la kuondolewa kwa vikwanzo vya kibiashara baina ya nchi wanachama, hasa Tanzania na Kenya ambayo ni wafanyabiashara wakubwa kwenye jumuiya hiyo imeongeza biashara.

“Namna tunayoweza kunufaika zaidi ni kuongeza uzalishaji viwandani hata mazao ya kilimo ambayo kwa kiwango kikubwa Tanzania ndio inategemewa kwa chakula. Sudan Kusini, Kenya, DRC na Rwanda wanategemea mahindi kwetu,” anasema Dk Lawi, akisisitiza uimarishaji wa miundombinu hasa ya bandari na reli ili kurahisisha usafirishaji.