Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Athari za mkono wa Serikali katika safari ya ushirika Tanzania

Muktasari:

  • Tanzania imekuwa na historia ya muda mrefu ya vyama vya ushirika, hususan vya wazalishaji wa mazao mbalimbali, hata hivyo eneo hilo bado lina changamoto lukuki zilizozorotesha ushirika, licha ya kuwepo kwa mafanikio.

Ushirika ni chombo muhimu katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii. Kupitia ushirika, jamii nyingi kwa pamoja zimeweza kufanikisha malengo ya kiuchumi, kupunguza umaskini, na kuongeza ustawi wa kijamii.

Hata hivyo, ili ushirika uwe na mafanikio, ni muhimu kuwa na utawala bora, elimu ya kutosha kwa wanachama na ushirikiano wa dhati. Tanzania imekuwa na historia ya muda mrefu ya vyama vya ushirika, hususan vya wazalishaji wa mazao mbalimbali, hata hivyo eneo hilo bado lina changamoto lukuki zilizozorotesha ushirika, licha ya kuwepo kwa mafanikio.

Miongoni mwa sababu zilizozorotesha ushirika nchini ni pamoja na sheria kandamizi, ikiwemo Sheria ya Ardhi ya Wakoloni ya mwaka 1923, Serikali kuingilia vyama vya ushirika kwa kuanzisha bodi za mazao na siasa kuingizwa kwenye vyama hivyo.

Kwa Tanzania, katikati ya changamoto hizo, vimekuwepo vyama imara na maarufu vya ushirika kama Kilimanjaro Native Coperative Union (KNCU 1933) kwa zao la kahawa, Nyanza Cooperative Union (NCU) kwa zao la pamba, Tandahimba-Newala Coperative Union (Tanecu), Masasi and Mtwara Coperative Union (Mamcu) na Ruangwa, Nachingwea and Lindi (Runali) vyote vya korosho.

Lengo la msingi la vyama hivyo, pamoja na mambo mengine, limebaki ni kutetea masilahi ya wazalishaji wadogo na kuwawezesha kunufaika na mazao yao.

Safari ya ushirika tangu nchi kupata uhuru imekuwa na mabadiliko mengi, miongoni mwake ni mwingiliano wa masilahi na mamlaka nyingine kiasi cha kufanya wazalishaji hao kukosa masilahi waliyotarajia.

Akijadili suala hilo, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi, Beatrice Kimaro, anarejea historia kabla ya ukoloni (kabla ya 1920), kuwa jamii nyingi za Kitanzania zilikuwa na mifumo ya kijamii na kiuchumi, ambayo iliegemea katika ushirikiano wa kijamii.

“Ushirikiano huu haukuwa rasmi kwa namna ya vyama vya ushirika vya kisasa vinavyoendeshwa, bali ulihusisha taratibu za jadi za kugawana rasilimali kama ardhi, maji na nguvu kazi.

“Ushirikiano huu ulitegemea mfumo wa ukoo na familia, ambapo ardhi ilikuwa mali ya jamii nzima na iligawanywa kulingana na mahitaji ya kila familia/kaya.

“Ardhi ndiyo ilikuwa ni mali ya jamii nzima, utawala wa kimila, na ilitumiwa kwa pamoja,” anasema.

Anatoa mfano wa Wachaga ambao walikuwa na mfumo unaoitwa Ng’anda ambapo wakulima walitekeleza mfumo wa kazi za mzunguko.

“Wanafamilia wa ukoo walifanya kazi kwa pamoja kwenye mashamba kama kupanda au kuvuna mazao.

“Njia hii ya usimamizi wa ardhi na kushirikiana ililenga kuhakikisha kuwa kila mmoja katika jamii anapata fursa ya kumiliki na kutumia ardhi kwa usawa na kwa manufaa ya wote,” anasema.

Wakati wa Ukoloni (1920-1960)

Akieleza ilivyokuwa wakati wa ukoloni, Kimaro anasema sera za ardhi na mfumo wa ushirika zilikuwa sehemu muhimu za mpango wa wakoloni kudhibiti uchumi wa wakulima na ardhi ya wenyeji.

“Ardhi iliyoendelea kumilikiwa na jamii kwa kawaida ilianza kuchukuliwa hatua kwa hatua na Serikali za kikoloni kupitia sheria za ardhi ambazo ziliwekwa ili kuhakikisha kwamba malighafi za kilimo, kama vile kahawa na pamba, zinapatikana kwa ajili ya viwanda vya kikoloni,” anasema.

Ni katika kipindi hicho cha miaka ya 1920, anasema mfumo rasmi wa vyama vya ushirika ulianzishwa ili kutoa jukwaa kwa wakulima kuuza mazao ya biashara kwa pamoja ili kufaidisha viwanda vya wakoloni.

“Kwa mfano, Kilimanjaro Native Cooperative Union (KNCU 1933), ilianzishwa kusaidia wakulima wa kahawa wa Kilimanjaro kuuza mazao yao, lakini kiliundwa zaidi kwa masilahi ya ukoloni.

“Wakoloni walichukua ardhi yenye rutuba na kuhamasisha uzalishaji wa mazao ya biashara, huku wakulima wadogo wakiwa na jukumu la kuzalisha mazao hayo kwenye ardhi zao za kijamii (kihamba),” anasema.

Anaitaja Sheria ya Ardhi ya mwaka 1923 iliyoweka ardhi ya wenyeji chini ya usimamizi wa Serikali ya kikoloni, na hivyo kupunguza mamlaka ya jamii na koo katika usimamizi wa ardhi zao za jadi.

“Vilevile, Sheria ya Ushirika ya mwaka 1932 ilikuja kuweka rasmi mfumo wa vyama vya ushirika kwa lengo la kurahisisha usimamizi wa wakulima, hasa katika uzalishaji wa mazao ya biashara kama kahawa na pamba,” anasema.

Kuzorota kwa vyama vya ushirika

Akijadili sababu za kuzorota ushirika nchini, Dk Ng’wanza Kamata anasema baada ya Tanganyika kupata uhuru mwaka 1961, ilitungwa Sheria ya kudhibiti mazao ya 1962.

“Sheria hiyo iliiruhusu Serikali kuunda bodi za mazao na ushirika ukiwapo,” anasema.

Anasema kazi ya bodi za mazao ikawa ndio mnunuzi na muuzaji wa mazao ya mkulima na kuyatafutia soko nje.

“Kwa hiyo ikabadilisha nafasi ya ushirika kutoka kuwa wakusanyaji na wauzaji wa mazao yao wenyewe moja kwa moja wakawafanya kuwa mawakala wa bodi za mazao, kwa maana ya kukusanya mazao na baadaye kuyapeleka kwenye bodi ili yakatafutiwe masoko,” anasema.

“Kilichotokea na ukiangalia taarifa ya Tume ya Rais ya Kuchunguza Bodi za Mazao na Ushirika ya mwaka 1966 ilionekana wazi kwamba mfumo huo umewaongezea wakulima mzigo.

“Kwa sababu kwa bei waliyokuwa wanapata, na kama kungekuwa na ziada inabaki kwenye ushirika kwa ajili ya maendeleo mengine, ziada ile lazima igawanywe tena iende kuhudumia tena warasimu katika bodi za mazao,” anasema.

Dk Kamata anasema lengo la Serikali lilikuwa ni kutafuta namna ya kudhibiti ushirika.

“Walikuwa na dhana moja kwamba ushirika kwa kweli ulikuwa umeshamiri sana na ulikuwa unajitegemea, kwa hiyo walikuwa na pesa. Wale warasimu kwenye ushirika walikuwa wanaajiri watu kwenye majineri. Kwa hiyo ushirika ulikuwa umeshamiri.

“Kwa hiyo kwa upande mmoja hiyo iliwatisha wanasiasa ambao hata nguvu za kiuchumi hawakuwa nazo. Hawakutaka watu wenye nguvu ya pesa na ushawishi nje ya tabaka la kisiasa,” anasema.

Kadhalika anataja kuwepo kwa hisia kwamba, viongozi wa vyama vya ushirika walikuwa wanafaidi fedha za ushirika, hivyo wanasiasa wakaanza kuibua tuhuma za ubadhirifu wa fedha.

“Kwa kipindi hiki wakaanza kusema ndani ya ushirika kuna ubadhirifu, lakini wakitafuta njia ya kuingilia ushirika. Kwa hiyo walipokuwa wameunda hizi bodi za mazao na kuanza kutoa hizo tuhuma mbalimbali za ubadhirifu na rushwa kwenye ushirika, wakawa wanapata nafasi ya kupenyeza watu wao kwenda kuendesha ushirika,” anasema.

Kutokana na hali hiyo, Dk Kamata anasema uendeshaji wa bodi za mazao ukawa na gharama kubwa na gharama hizo zilibebwa na wakulima, hivyo zikaanza kudhoofisha ushirika.

“Wananchi, wakulima, wakawa hawapati bei nzuri na wakati mwingine wakawa hawapati malipo kwa wakati. Ndipo katika kudorora huko na tuhuma zilizotolewa, mwaka 1966 ikaundwa hiyo Tume ya Rais ya kuchunguza ushirika na bodi za mazao.”

Sababu nyingine inayotajwa ni Serikali kuanzisha ushirika holela. “Serikali ikaanzisha ushirika kwenye maeneo ambapo ilidhani haupo, kwa sababu inasema ushirika ni kitu kizuri sana, kwa hiyo ikaanza kuanzisha ushirika tu usiokuwa na wanachama.

“Matokeo yalikuwa kuchochea migogoro mikubwa katika ushirika na kuudhoofisha ushirika.

Kutokana na hilo, ikaundwa Tume ya Ushirika na Mamlaka za Mazao ya 1966 ambayo ilitoa mapendekezo mengi ambayo shabaha yake ilikuwa ni kuangalia namna bora ya kuboresha na kuhuisha vyama vya ushirika.

Hata hivyo, ilibainika kuwa wakulima walikuwa wanapewa bei ndogo na bodi na hawakulipwa malipo ya pili na bodi.

Pia ilibainika kuwepo kwa makato kwenye kilo za mkulima wa kuongeza uzito wa gunia na kulikuwa na ucheleweshaji mkubwa wa malipo.

“Kiutawala baada ya bodi kuwa zimeanzishwa, ushirikishwaji wa wanachama ukawa umekufa. Kwa sababu halmashauri za ushirika zikawa hazina kazi zilizokuwa zinafanya mwanzo, Tume ilibainisha kuingia kwa chama na viongozi wa kisiasa katika vyama vya ushirika,” anasema.

Ushirika baada ya Azimio la Arusha

Dk Kamata anasema kutokana na changamoto zilizobainishwa na Tume ya Rais ya kuchunguza ushirika na bodi za mazao, Serikali ikaanza juhudi za kuboresha kwa kurekebisha sheria mwaka 1968.

Hata hivyo, sheria hiyo haikudumu kutokana na mabadiliko ya kisiasa yaliyotokea.

Mbali na tume hiyo, Dk Kamata pia anataja tume ya Masomo iliyoanzisha sheria mpya ya mwaka 1975 ya ujamaa vijijini, ambayo ilisababisha ushirika kufutwa na kuanzishwa kwa vijiji vya ujamaa.

“Chini ya utaratibu huu mpya, vijiji vya ujamaa viliandikishwa kama vyama na moja ya shughuli yake ni kununua mazao ya wakulima.

Anasema pia kilichochangia kufutwa kwa vyama hivyo ni Tume ya Masomo iliyopendekeza pamoja na mambo mengine kufutwa kwa baadhi ya vyama vikuu vya ushirika.

“Kwa hiyo mashirika kadhaa yakafutwa na maelekezo yakawa ni kwamba mali zao zitapelekwa katika mashirika ya maendeleo ya wilaya, halmashauri za wilaya, DDC, na hizi zinazoitwa Regional Trading Corporation (RTC).

“Haya ndiyo mabadiliko makubwa yalitotokea mwaka 1975, ushirika ukawa umevunjwa na kwa hiyo bodi zikashamiri.”


Tume ya Ushirika ya mwaka 1981

Dk Kamata anabainisha kuwepo kwa Tume ya Ushirika iliyoundwa mwaka 1981 ambayo pamoja na mengine, ilipendekeza kuanzishwa kwa Benki ya Ushirika na Maendeleo Vijijini (CRDB).

Mbali na hilo, tume hiyo ilipendekeza kuundwa kwa Jumuiya ya Vyama vya Ushirika na ikaweka sharti kwamba lazima kwanza uwe mwanachama wa CCM na siyo tu mwanachama, ni lazima uthibitishwe na chama.