Prime
Baa 13 zilizofungiwa njiapanda, Kinondoni yafunga milango
Muktasari:
- Huku Manispaa hiyo ikisisitiza watekeleze kanuni na sheria kwanza, imeweka msimamo kwamba haitatoa leseni mpya kwa uwekezaji huo kwa kile ilichodai kuwa ina zaidi ya baa, Night Club na Glossary 350 zinazohitaji kuboreshwa ili kukidhi vigezo na kuondoa malalamiko yaliyopo kutoka kwa umma.
Dar es Salaam. Hatma ya baa 13 zilizofungwa na Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni Juni 22, 2026, imeendelea kuwa njia panda, licha ya kufanyika kwa kikao cha zaidi ya saa tano kati ya wafanyabiashara wa baa, vilabu vya usiku (Night Club), Glossary na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Kinondoni kujadili namna ya kumaliza mgogoro huo.
Badala ya kuagiza baa hizo zifunguliwe, uongozi wa wilaya umesisitiza kuwa zitaendelea kufungwa hadi wamiliki wake watakapotekeleza masharti yote ya kisheria na kuboresha miundombinu ya biashara zao ili kukidhi viwango vinavyotakiwa.
Aidha, Manispaa ya Kinondoni imesema haitatoa leseni mpya za baa, Night Club na Glossary, ikieleza kuwa tayari ina zaidi ya biashara 350 za aina hiyo na kinachohitajika kwa sasa ni kuboresha zilizopo ili zifuate sheria na kupunguza malalamiko kutoka kwa wananchi.
Kikao hicho kilichofanyika leo, Ijumaa, Juni 26, 2026, katika ofisi za Manispaa ya Kinondoni, kimehudhuriwa na Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Saad Mtambule, Mkurugenzi wa Manispaa pamoja na viongozi wa idara mbalimbali, likiwamo Jeshi la Polisi.
Kikao hiki kimefanyika zikiwa zimepita siku nne baada ya kufungwa kwa baa hizo kwa madai ya kukiuka Sheria ya Vileo ya mwaka 1968 na kanuni zake, ikiwemo kupiga muziki kwa sauti kubwa na kusababisha kero kwa wananchi.
Akisoma maazimio ya kikao hicho, Mtambule amesema baa zilizofungwa hazitafunguliwa hadi zitakapotekeleza masharti yote yaliyowekwa.
"Tunasisitiza kuheshimiwa kwa sheria na kanuni. Wamiliki wanapaswa kuboresha miundombinu ya biashara zao, ikiwemo ubora wa majengo, milango, madirisha na mazingira ya biashara. Serikali itaandaa mwongozo wa utekelezaji wa vigezo hivyo," amesema.
Amesema pande zote zimekubaliana kuimarisha ushirikishwaji kati ya Serikali na wawekezaji kupitia ukaguzi wa mara kwa mara utakaowapa nafasi wamiliki wa biashara kujirekebisha kabla ya hatua za kisheria kuchukuliwa, sambamba na ukaguzi wa kushtukiza.
Pia, amesema kutaimarishwa ulinzi na usalama katika maeneo ya biashara, huku matumizi ya walinzi binafsi maarufu kama mabaunsa yakifanyiwa tathmini upya.
"Tumekubaliana pia kufanya mapitio ya sheria zinazohusu biashara ya vileo ili kuishauri Serikali pale panapohitajika maboresho," amesema.
Kwa mujibu wa maazimio hayo, vifaa vyote vya muziki vitapaswa kupimwa na mamlaka husika kabla ya kuanza kutumika, huku ikipewa kipaumbele kuundwa kwa timu ya wataalamu kutoka kada mbalimbali itakayokuwa ikitoa ushauri kabla ya hatua za kufungia biashara kuchukuliwa.
Aidha, wamiliki wa baa wametakiwa kuhakikisha biashara zao hazitumiki kwa shughuli zinazokiuka maadili, ikiwemo biashara ya ngono na matumizi ya dawa za kulevya, ambazo viongozi wamesema zinaharibu taswira ya baadhi ya maeneo ya starehe.
Pia, kila baa itapaswa kuwa na msimamizi maalumu wa ma-DJ ili kuhakikisha muziki hauchezwi kwa kiwango kinachosababisha kelele kwa jamii inayozunguka maeneo hayo.
Kikao chazua vicheko
Kikao hicho kilishuhudia matukio mbalimbali, ikiwemo washiriki kuzungumza kwa uwazi kuhusu changamoto zinazoikabili sekta hiyo, huku baadhi wakikiri kuwapo kwa biashara ya ngono katika baadhi ya maeneo ya starehe.
Katika hali iliyozua kicheko, Katibu wa Wamiliki wa Baa na Night Club, Ramadhan Danda, maarufu Potipoti, alipiga magoti mbele ya viongozi wa wilaya akiwaomba wazifungulie baa zilizofungwa.
Akitoa hoja yake, Potipoti amesema kufungwa kwa biashara hizo kumesababisha hasara kubwa kwa wawekezaji na Serikali yenyewe kutokana na kupungua kwa mapato.
"Hata bajeti iliyopitishwa Bungeni hivi karibuni inategemea mchango wa sekta binafsi. Sisi ni sehemu ya wachangiaji wakuu wa mapato ya Serikali, hivyo tunaomba tupewe nafasi ya kuendelea kufanya biashara huku tukizingatia sheria," amesema.
Ameongeza kuwa vifaa vya muziki vilivyopo ndani ya baa hizo vinaendelea kuharibika wakati biashara zikiwa zimefungwa, ilhali vilinunuliwa kwa gharama kubwa.
Wamiliki walalamikia hasara
Kwa upande wake, mmiliki wa Joyce Bar iliyopo Mwananyamala, Joyce Cosmas amesema kikao hicho kimewapa fursa ya kuelewa maeneo wanayopaswa kuyaboresha ili biashara zao ziendeshwe kwa kuzingatia sheria.
Hata hivyo, amesema kufungwa kwa biashara hizo kumesababisha hasara kubwa. "Kumfungia mtu biashara si jambo dogo. Mbali na mwenye biashara kuathirika, hata familia zinazomtegemea zinapata shida."
Kuhusu agizo la kuondoa makahaba na kudhibiti biashara ya ngono katika baa, Joyce amesema utekelezaji wa sharti hilo ni mgumu kwa wamiliki wa baa peke yao.
"Biashara ya ngono ni tatizo la muda mrefu. Si rahisi kwa mmiliki wa baa kuikomesha peke yake. Serikali na mamlaka nyingine zinapaswa kushirikiana nasi kwa sababu wahusika wanajipatia kipato kikubwa na wateja wao ni watu wa kada mbalimbali," amesema.
Ameshauri Serikali kutafuta utaratibu wa kudhibiti shughuli hizo kupitia vyombo husika badala ya kuwaachia jukumu hilo wamiliki wa baa pekee, akisema hatua hiyo itasaidia kupunguza migogoro kati ya wafanyabiashara na mamlaka za usimamizi.