Bei ya kahawa ghafi yapaa, yafikia Sh10,000 kwa kilo moja
Muktasari:
- Bei hiyo ni kwa kahawa iliyochakatwa kwenye viwanda vidogo vilivyopo kwenye vyama vya ushirika(CPU), huku iliyochakatwa nyumbani (HP) ikitangazwa kuuzwa kwa Sh 8,500 kwa kilo.
Moshi. Wakati Serikali ikihamasisha wakulima wa kahawa nchini kulima kwa tija, Bodi ya Kahawa Tanzania (TCB) imetangaza kuwa bei ya kahawa ghafi ya Arabika ya maganda imepanda kutoka Sh7,500 Agosti hadi Sh10,000 kwa kilo Septemba mwaka huu.
Bei ya Sh10,000 kwa kilo ni kwa kahawa iliyochakatwa kwenye viwanda vidogo vya vyama vya ushirika (CPU), huku kahawa iliyochakatwa nyumbani (HP) ikifikia Sh8,500 kwa kilo.
Kahawa ya Robusta kwa sasa inauzwa Sh5,000 kwa kilo. Kwa mujibu wa taarifa ya Mkurugenzi Mkuu wa TCB, Primus Kimaryo aliyoitoa leo Jumatatu Septemba 9, 2024 mjini Moshi, bei hizo zinajumuisha michango, tozo na gharama nyingine za kibiashara.
"Bodi ya kahawa inapenda kutoa ufafanuzi kwa viongozi wa vyama vya ushirika kuwa bei ya mauzo ya kahawa ghafi ya Arabika ya CPU itakuwa Sh10,000 na kahawa iliyochakatwa majumbani (HP) itakuwa Sh8,500 kwa kilo Septemba, 2024," amesema Kimaryo.
Aidha, amesema bei hizo zitafanyiwa marejeo mara kwa mara kulingana na mwenendo wa soko la dunia na hawatarajii kusajili mkataba wowote wa mauzo chini ya bei hiyo.
Akizungumzia hilo, Mkurugenzi wa Ubora na Masoko wa TCB, Frank Nyarus amesema bei nzuri ya kahawa inatokana na mwenendo wa bei katika soko la dunia na kuongeza kuwa katika msimu uliopita, kahawa iliingiza Dola milioni 200 za Marekani.
Amesemja wakulima wamejitahidi kuboresha ubora wa kahawa yao na wanatarajia kupata bei nzuri inayoendana na jitihada hizo.
Kuhusu uzalishaji, amesema wanatarajia ongezeko kutoka tani 75,000 msimu uliopita hadi tani 85,000 msimu wa 2024/2025, kati ya hizo, tani 45,000 ni Robusta na tani 40,000 ni Arabika.
Nyarus amesema ongezeko la uzalishaji linatokana na jitihada za Bodi ya Kahawa kwa kushirikiana na wadau, ikiwemo kugawa bure miche bora ya kahawa kwa wakulima.
Amesema mwaka 2023, zaidi ya miche milioni 21 iligawiwa kwa wakulima.
Katibu wa Chama cha Ushirika cha Kinyamvuo, Glory Sam, amesema ongezeko la bei limekuja wakati mwafaka na ameiomba Serikali kuhakikisha wakulima wananufaika na kilimo cha kahawa.
"Tunafurahia kuona mkulima akipata manufaa, lakini tunapenda kuona wakulima wakibakiza Sh10,000 kama inavyotajwa, bila makato makubwa," amesema.
Mkulima Atanasi Joseph kutoka mkoani Kilimanjaro, amesema ongezeko la bei linaweza kuhamasisha zaidi watu kurudi kulima kahawa.
“Kwa mfano hapa kwetu, kilimo cha kahawa ndiyo ilikuwa kipaumbele hasa kwa mababu na kilileta mafanikio makubwa kwa familia, zilisomesha watoto na kujenga nyumba, kilipoyumba kila mtu akakiacha,” ameeleza mkazi huyo.
Hata hivyo, amesema kwa kuwa soko linarudi, watu watalima tena.