Bei ya petroli, dizeli yashuka Julai

Muktasari:
- Kwa bei za Juni 2025, wastani wa gharama za kubadilisha fedha za kigeni umepungua kwa asilimia 4.98.
Dar es Salaam. Bei ya mafuta ya petroli, dizeli na ya taa katika Bandari ya Dar es Salaam imeshuka ikilinganishwa na Juni 2025.
Taarifa iliyotolewa leo Julai Mosi, 2025 na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura), imeonyesha bei ya kikomo ya petroli katika Bandari ya Dar es Salaam ni Sh2,877 tofauti na mwezi uliopita bei ya kikomo ilikuwa Sh2,885.
Pia bei ya dizeli nayo imeshuka kutoka Sh2,826 hadi Sh2,767 huku mafuta ya taa nayo ikishuka kutoka Sh2,877 hadi bei ya sasa ya Sh2,629.
Kwa Bandari ya Tanga, bei ya petroli ni Sh2,938 tofauti na Juni ambapo iliuzwa Sh2,946, dizeli Sh2,828 bei ya sasa ikilinganishwa na Sh2,887 na mafuta ya taa Sh2,690 kutoka Sh2, 938.
Hali ni tofauti katika Bandari ya Mtwara kwani Petroli huuzwa kwa bei ya juu zaidi ya Sh2,969 kwa lita moja, dizeli Sh2,859 na mafuta ya taa Sh2,722.
”Kwa Julai 2025, gharama za kuagiza mafuta katika Bandari ya Dar es Salaam zimeongezeka kwa wastani wa asilimia 27.98 kwa mafuta ya petroli, asilimia 8.04 kwa mafuta ya dizeli na kupungua kwa asilimia 5.64 kwa mafuta ya taa, hakuna mabadiliko kwa Bandari ya Tanga na Mtwara,” imeeleza taarifa ya Ewura.
Kwa mujibu wa mamlaka hiyo, bei za mafuta hapa nchini zinazingatia gharama za mafuta yaliyosafishwa kutoka soko la Uarabuni.
Ewura imebainisha katika bei kikomo kwa Julai 2025, bei za mafuta kwa soko la dunia zimeongezeka kwa asilimia 6.8 kwa mafuta ya petroli, asilimia 9.3 kwa mafuta ya dizeli na asilimia 8.1 kwa mafuta ya taa,”taarifa ya Ewura imeeleza.
Kufuatia mabadiliko hayo ya bei, Ewura imewataka wafanyabiashara wa bidhaa za mafuta kwa jumla na rejareja pamoja na jamii kuzingatia bei kikomo za bidhaa za mafuta ya petroli kwa eneo husika.
“Kwa mujibu wa Sheria ya Mafuta ya mwaka 2015, kifungu namba 166, bei za bidhaa za mafuta ya petroli zitaendelea kupangwa na soko, Ewura itaendelea kuhamasisha ushindani kwa kutoa taarifa za bei kikomo za bidhaa za mafuta.
“Kampuni za mafuta ziko huru kuuza bidhaa za mafuta ya petroli kwa bei ya ushindani isipokuwa bei hizo zisizidi bei kikomo au kuwa chini ya bei iliyoruhusiwa kama zilivyokokotolewa kwa mujibu wa Kanuni za Ewura za Kupanga Bei za Mafuta za Mwaka 2022,” imeeleza taarifa hiyo.
Kwa mujibu wa Ewura, vituo vyote vya mafuta vinatakiwa kuchapisha bei za bidhaa za mafuta katika mabango yanayoonekana bayana yakionesha bei za mafuta, punguzo, vivutio vya kibiashara vinavyotolewa na kituo husika.
“Pale ambapo inawezekana kuchagua, wateja wanashauriwa kununua bidhaa za mafuta katika vituo vinavyouza mafuta kwa bei nafuu zaidi ili kushamirisha ushindani.
Ni kosa kuuza mafuta bila kuweka mabango ya bei inayoonekana vizuri kwa wateja, adhabu kali itatolewa kwa kituo husika kwa kutotekeleza matakwa ya kisheria kwa mujibu wa kanuni husika,” imeeleza taarifa hiyo.