Benki ya Standard Chartered kuuza jengo lake Nairobi
Muktasari:
- Standard Chartered yauza jengo la Nairobi kupunguza utegemezi wa ofisi kubwa na kuhamia kidijitali. Imeuza pia mali Kenya, ikisisitiza haijiondoi sokoni, huku ikiendelea na mageuzi ya kimataifa tangu 2022.
Dar es Salaam. Benki ya Standard Chartered imeanza mchakato wa kuuza makao makuu yake ya Afrika Mashariki yaliyopo Nairobi nchini Kenya, hatua inayotajwa kuwa sehemu ya mkakati wa benki hiyo wa kurahisisha shughuli zake na kutumia mtaji kwa ufanisi zaidi.
Taarifa iliyoandika na gazeti dada la The Citizen, Benki hiyo yenye asili ya Uingereza ilithibitisha kuwa uuzaji wa ofisi yake iliyopo Chiromo Road ni sehemu ya juhudi pana za kupanga upya mali zake za majengo duniani, ikiwa na lengo la kuongeza ufanisi na kupunguza utegemezi wa maeneo makubwa ya ofisi.
Jengo hilo la Nairobi lenye ghorofa saba, lililopo eneo la Westlands, tayari limewekwa rasmi kwenye orodha ya mali zinazouzwa wakati ambao Benki hiyo inalenga kupata thamani kutoka kwenye mali zake muhimu huku ikielekea zaidi kwenye mfumo wa kidijitali na biashara isiyohitaji mali nyingi za kudumu.
Standard Chartered pia imeuza angalau mali nyingine mbili nchini Kenya katika miaka ya hivi karibuni. Hata hivyo, benki hiyo imesisitiza kuwa hatua hiyo haimaanishi kujiondoa katika soko la Kenya.
Uuzaji huo unafuatia mpango mpana wa mageuzi ya kimataifa ulioanzishwa Aprili 2022, ambapo benki hiyo ilijiondoa katika masoko kadhaa barani Afrika na Mashariki ya Kati. Hatua hizo za kujiondoa, zikiwemo shughuli zake nchini Cameroon na Gambia, wakati mwingine zilisababisha hasara za kifedha.
Nchini Tanzania, benki hiyo iliuza huduma zake za wateja binafsi na biashara ndogo ili kujikita zaidi katika huduma za benki kwa makampuni na huduma za benki kwenye uwekezaji.