Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

BoT: Mikopo ya kobe, nyoka haina leseni

Muktasari:

  • Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imeendelea kuzionya taasisi zinazotoa mikopo bila ya kuwa na leseni huku ikisema adhabu kwa watakaobainika ni Sh20 milioni au kifungo cha miaka miwili jela au vyote kwa pamoja

Dar es Salaam. Siku chache baada ya kusambaa mitandaoni mahojiano ya mmoja wa wanawake akizungumzia uwepo wa mikopo aina ya kobe na nyoka, Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imewataka wananchi kutokopo kwa kuwa haijakatiwa leseni.

Taarifa ya BoT iliyotolewa jana inaeleza kuwa, kuna taarifa katika mitandao ya kijamii zinazohusisha alama za wanyama kama vile kobe na nyoka katika utoaji wa mikopo, jambo ambalo ni kinyume cha sheria na maadili ya utoaji wa huduma za kifedha.

“Hivyo, wananchi wanashauriwa kupuuza taarifa hizo na kutokujihusisha nazo kwa kuwa hazijapewa leseni hapa nchini,” inasema sehemu ya taarifa hiyo.

Katika mahojiano ya mama huyo na kituo kimoja cha habari nchini, anasikika akisema kuna mkopo mpya aina ya kobe na nyoka imeingia huku akielezea kuwa, ikiwa mtu atashindwa kuulipa atalazimika kumnyonyesha kobe.

“Kwa mkopo wa nyoka unaongea na nyoka kwenye nyumba ya mtu, nyoka anakuwa juu humuoni ila unajua huyu ni nyoka, anafugwa na mtu, unachukua mkopo kuanzia Sh100,000. Unapewa hela, ila ulipe kwa wakati na hii haihitaji barua ya Serikali za mitaa wala mjumbe,” anasimulia mama huyo.

Katika taarifa ya BoT iliyotolewa inasema kwa mujibu wa Kifungu cha 16(1) cha Sheria ya Huduma Ndogo za Fedha ya mwaka 2018, ni kosa kwa taasisi, kampuni na watu binafsi kujihusisha na biashara ya kutoa mikopo bila kuwa na leseni kutoka Benki Kuu ya Tanzania.

“Pia, kifungu cha 16(2) (a) cha sheria hiyo kimeainisha adhabu inayopaswa kutolewa kwa kuendesha biashara ya kukopesha bila kuwa na leseni ikiwa ni pamoja na kutozwa faini isiyopungua Sh20 milioni au kifungo cha muda usiopungua miaka miwili au vyote viwili kwa pamoja,” inaeleza taarifa hiyo.

Kutokana na hilo, BoT  inausisitiza umma kuepuka kukopa au kufanya biashara na taasisi, kampuni au mtu binafsi ambaye hana leseni.

“Endapo taasisi au mtu binafsi anataka kufanya biashara ya ukopeshaji, anatakiwa kufuata taratibu husika za kuomba leseni kutoka Benki Kuu ili apewe kwa mujibu wa sheria. Ni muhimu mtu anapotaka kukopa, atumie taasisi zenye leseni ya Benki Kuu ili kuhakikisha huduma anayopata ni salama na inayozingatia sheria za nchi,” inaeleza taarifa.

Kufuatia hilo, wachambuzi wa masuala ya fedha wamesema Watanzania wengi hasa wale wa kipato cha chini wanakimbilia kwa wakopeshaji wasio na leseni kwa sababu hawawezi kupata mikopo kwenye taasisi rasmi za fedha.

Hiyo ni kwa sababu taasisi nyingi za fedha huwa na mahitaji kama dhamana ambayo wengi hawawezi kutimiza, hivyo huwalazimu kutafuta wakopeshaji ambao hutoa mikopo ya haraka lakini mara nyingi huwa na viwango vya juu vya riba.

Akizungumza na Mwananchi leo Jumatano Januari mosi, 2025, Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu Cha Elimu Dar es Salaam (DUCE), Abel Kinyondo amesema  Watanzania wengi wanalazimika kukopa kutoka kwa wakopeshaji wasio na leseni kwa sababu hawawezi kupata mikopo kutoka kwa vyanzo rasmi.

“Na hii ni kwa sababu wanakabiliwa na changamoto nyingi za kifedha kama vile ada za shule na chakula. Suluhisho bora la muda mrefu ni Serikali kujikita katika kukuza uchumi na kutengeneza ajira zenye staha ili wananchi waweze kujikimu bila kutegemea mikopo,” amesema Kinyondo.

Mchumi kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Dk Mwinuka Lutengano amesema

mikopo kwenye taasisi ambazo hazijasajiliwa hutolewa kwa haraka na kwa muda mfupi zaidi ikilinganishwa na taasisi rasmi za kifedha.

Amesema urahisi wa taratibu na mchakato wake, ndiyo unaovutia wengi kwa sababu wakopaji wengi bado hawana uelewa wa kutosha wa gharama za mkopo kupitia riba zake.

“Pia, vigezo vya kupata mkopo mfano benki kwao ni vigumu zaidi. Ni vyema elimu iendelee kutolewa kwa wananchi na taarifa sahihi za vyanzo tofauti vya mikopo. Kwa sababu, nje ya taasisi za fedha ipo pia mikopo ya Serikali mfano ofisi za mikoa, halmashauri na mfuko wa vijana, ofisi ya Waziri Mkuu,” amesema Lutengano.