Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Dk Mwigulu: Tanzania yazidi kuvutia uwekezaji viwanda vya dawa

Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba alipokutana na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD), Christophe Lecourtier, kando ya Mkutano wa Ushirikiano kati ya Afrika na Ufaransa (Africa Forward Summit) hayo jana Mei 12, 2026 jijini Nairobi, Kenya.

Muktasari:

  • Hatua hiyo inalenga kuimarisha uhakika wa upatikanaji wa dawa, kupunguza gharama za uagizaji, kuvutia uwekezaji wa viwanda, na kuongeza ajira pamoja na thamani ya bidhaa zinazozalishwa nchini.

Dar es Salaam. Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba amesema Tanzania imeweka kipaumbele katika uwekezaji wa viwanda vya dawa ili kupunguza utegemezi wa kuagiza dawa kutoka nje ya nchi.

Dk Mwigulu ameyasema hayo jana Mei 12, 2026 jijini Nairobi, Kenya alipokutana na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD), Christophe Lecourtier, kando ya Mkutano wa Ushirikiano kati ya Afrika na Ufaransa (Africa Forward Summit).

Dk Mwigulu alimuwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk Samia Suluhu Hassan katika Mkutano wa Ushirikiano kati ya Afrika na Ufaransa uliofanyika Mei 11 hadi 12, 2026 jijini Nairobi, Kenya.

“Tunaagiza kiasi kikubwa cha dawa kutoka nje ya nchi, lakini sasa tumeweka kipaumbele kuona jinsi tunavyoweza kuwekeza kwenye viwanda vya dawa ili tuzalishe nchini mwetu,” alisema Dk Mwigulu.

Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba (wa kwanza kulia) alipokutana na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD), Christophe Lecourtier, kando ya Mkutano wa Ushirikiano kati ya Afrika na Ufaransa (Africa Forward Summit) hayo jana Mei 12, 2026 jijini Nairobi, Kenya.

Aliongeza kuwa fursa hiyo inapaswa kuvutia wawekezaji wa ndani na nje, akibainisha kuwa Tanzania ni lango muhimu la masoko ya kikanda kupitia Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).

“Kupitia ofisi yako pamoja na wadau wengine, wanaweza kutumia fursa hii kubwa iliyopo kuja kuwekeza kwenye eneo hilo. Kuwekeza Tanzania ni kuingia katika lango la EAC pamoja na SADC,” amesema.

Katika mazungumzo hayo, Dk Mwigulu pia amepongeza dhamira ya AFD katika kusaidia utekelezaji wa Mradi wa Maji wa Ziwa Victoria Awamu ya Pili, akisema ni wa kimkakati katika kuboresha upatikanaji wa maji safi na salama kwa wananchi.

Aidha, amesema Serikali inaendelea kuweka kipaumbele katika miradi mikubwa ya maendeleo ikiwemo Reli ya Kisasa (SGR), nishati, kilimo hususan umwagiliaji pamoja na sekta ya afya kupitia uwekezaji katika uzalishaji wa dawa nchini.

Katika hatua nyingine, Dk Mwigulu amesisitiza kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na AFD katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD), Christophe Lecourtier, wakati akizungumza alipokutana na Waziri Mkuu wa Tanzania, Dk Mwigulu Nchemba kando ya Mkutano wa Ushirikiano kati ya Afrika na Ufaransa (Africa Forward Summit) hayo jana Mei 12, 2026 jijini Nairobi, Kenya.

“Tunathibitisha tena dhamira ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuendelea kufanya kazi kwa karibu na AFD kwa manufaa ya maendeleo ya wananchi wetu,” amesema.

Akizungumzia sekta ya kilimo, Dk Mwigulu alitoa wito kwa wadau wa maendeleo kuoanisha malengo ya Bara la Afrika ili kuhakikisha maendeleo endelevu yanapatikana.

“Tumekaa muda mrefu tukizungumzia kujenga uwezo badala ya kujenga miundombinu itakayowezesha bara letu na nchi zetu kuendesha ajenda zao ipasavyo,” alisema.

Aidha, alisisitiza umuhimu wa uhamishaji wa teknolojia na matumizi ya mifumo ya kisasa ya kilimo, akisema Afrika inapaswa kuacha kusafirisha malighafi ghafi na badala yake kuongeza thamani ya mazao yake.