Elimu ya fedha kuwainua vijana kwenye kilimo biashara
Mkuu wa Chuo cha Benki Kuu ya Tanzania (BoT Academy), Dk Nicas Yabu,akizungumza leo Ijumaa Juni 26,2026 jijini Arusha baada ya kumalizika kwa mafunzo kwa vijana wanaojishughulisha na kilimo biashara waliotunukiwa vyeti vya kuwa Wakufunzi Waliothibitishwa wa Elimu ya Fedha (CFE). Picha na Janeth Mushi
Muktasari:
- Vijana 79 wanaojishughulisha na kilimo biashara kutoka mikoa mitano wamepata mafunzo ya wiki mbili ya elimu ya fedha na kutunukiwa vyeti vya kuwa Wakufunzi Waliothibitishwa wa Elimu ya Fedha (CFE), wakitarajiwa kuwafundisha wakulima, wafugaji na wajasiriamali wenzao ili kuboresha usimamizi wa fedha, kuongeza tija ya uzalishaji na kuimarisha usalama wa chakula.
Arusha. Vijana 79 wanaojishughulisha na kilimo biashara kutoka mikoa mitano wamepata mafunzo ya wiki mbili ya elimu ya fedha, yatakayowawezesha kuwa wakufunzi wa jamii katika masuala ya usimamizi wa fedha, uwekezaji na ujasiriamali kwa lengo la kuongeza tija katika kilimo na kuimarisha usalama wa chakula nchini.
Mafunzo hayo yametolewa kupitia programu ya Vijana Kilimo Biashara (VKB) inayotekelezwa na Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) kwa ufadhili wa Mastercard Foundation, kwa kushirikiana na Chuo cha Benki Kuu ya Tanzania (BoT Academy).
Akizungumza kwenye mafunzo hayo leo Ijumaa Juni 26, 2026 jijini Arusha, Mkuu wa Chuo cha BoT, Dk Nicas Yabu amesema vijana hao kutoka mikoa ya Arusha, Dodoma, Singida, Morogoro na Manyara, baada ya mafunzo hayo kwa sasa ni Wakufunzi Waliothibitishwa wa Elimu ya Fedha (Certified Financial Educators - CFE).
Amesema lengo la mafunzo hayo yamelenga kuwawezesha vijana kuwa walimu wa elimu ya fedha watakaorejea katika jamii zao kuwafundisha wakulima, wafugaji na wafanyabiashara wadogo namna bora ya kusimamia fedha.
Amesema washiriki hao waliosoma kwa muda wa wiki mbili, wamejengewa uwezo na uelewa kuhusu matumizi sahihi ya huduma za kifedha,umuhimu wa kuweka fedha mahali salama,fursa za uwekezaji,pamoja na namna ya kupata mikopo kwa ajili ya kukuza shughuli zao za kilimo na biashara ili kuongeza tija ya shughuli zao za uzalishaji na kujenga ustawi wa kiuchumi wa muda mrefu.
“Tumewafundisha namna ya kutafuta kipato halali, kubana matumizi, kuweka akiba na kuwekeza. Lengo ni kuhakikisha wanakwenda kuwawezesha wananchi katika maeneo yao kutumia fedha kwa ufanisi na kujenga uchumi imara kupitia shughuli za kilimo na biashara,” amesema.
Ameongeza kuwa mafunzo hayo yalihusisha wataalamu kutoka Benki Kuu ya Tanzania, UTT AMIS, sekta ya bima na mabenki mbalimbali ili kuwajengea washiriki uelewa kuhusu uwekezaji, matumizi ya bima za mazao na mifugo pamoja na matumizi sahihi ya mikopo.
Amesema baada ya kurejea katika maeneo yao, wahitimu watafuatiliwa ili kubaini idadi ya wananchi watakaowafundisha, hatua inayolenga kupanua wigo wa elimu ya fedha na kuongeza ushiriki wa wananchi katika shughuli za kiuchumi.
Mmoja wa washiriki hao kutoka mkoani Manyara, Shedrack Minja, amesema mafunzo hayo yamewajengea uwezo wa kuwekeza mapema hata kwa kipato kidogo na kutumia mifumo rasmi ya uwekezaji.
Amesema wao kama wakufunzi watawahamasisha vijana na wananchi kuanza kuweka akiba na kuwekeza kabla ya kutumia mapato yao ili kujenga ustawi wa kifedha.
“Tutapeleka elimu hii kwa jamii ili watu watambue kuwa hata kipato kidogo kinaweza kuwa mwanzo wa uwekezaji. Tunataka kujenga utamaduni wa kuwekeza kwanza kabla ya kutumia fedha,” amesema.
Naye, mshiriki kutoka Wilaya ya Kilosa mkoani Morogoro, Mzizi Rashid, amesema mafunzo hayo yamebadili mtazamo wake kuhusu kilimo, akisema sasa anakiona kama biashara inayoweza kuongeza kipato na kuchangia ukuaji wa uchumi.
Amesema pia wamejifunza umuhimu wa kufanya kazi kwa vikundi ili kuongeza nafasi ya kupata mitaji na fursa nyingine za kifedha, badala ya kila kijana kufanya kazi peke yake.
Kaimu Mkurugenzi Mkazi wa WFP nchini, Christine Mendes amesema mafunzo hayo ni sehemu ya utekelezaji wa programu ya VKB inayofadhiliwa na Mastercard Foundation, yenye lengo la kuwawezesha vijana kupata ajira zenye staha, ujuzi wa ujasiriamali na kukuza biashara kupitia sekta ya kilimo.
Amesema pamoja na kutengeneza ajira, programu hiyo inalenga kuwajengea vijana uwezo wa kusimamia fedha kwa kuwafundisha kupanga bajeti na kufanya maamuzi sahihi ya kifedha ili kuimarisha biashara zao na kuongeza kipato kwa muda mrefu.
Mendes amesema wahitimu 79 waliotunukiwa vyeti jijini Arusha wameongeza idadi ya Wakufunzi Waliothibitishwa wa Elimu ya Fedha kufikia 150, baada ya kundi la kwanza kuhitimu mkoani Mwanza.
Amesema tangu kuanza kwa programu ya VKB mwaka 2023, zaidi ya vijana 77,000 katika mikoa minane wamefikiwa na programu hiyo, huku akisisitiza kuwa ushirikiano kati ya WFP na Chuo hicho chini ya BoT, unaendelea kujenga kizazi cha vijana wenye uwezo wa kujiajiri, kuwekeza na kuchangia maendeleo ya uchumi wa nchi.
Julai 31, 2025, chuo hicho na WFP walisaini hati ya makubaliano (MoU) kwa lengo la kuwajengea uwezo wa elimu ya fedha vijana kupitia mradi wa VKB ili wapate maarifa ya kifedha yanayowawezesha kuboresha maisha yao kupitia kilimo biashara.