Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Hatifungani za makazi zinavyoshambuliwa sokoni

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa First Housing Finance Tanzania, Charles Mugila.

Muktasari:

  • Hatifungani hiyo ya First Housing Finance (FHF) iliyoratibiwa na Stanbic Bank Tanzania, ilikusanya Sh33.08 bilioni kutoka kwa wawekezaji mbalimbali, ikilinganishwa na lengo la awali la Sh5 bilioni

Dar es Salaam. Imani ya Watanzania katika uwekezaji katika masoko ya mitaji Tanzania imeendelea kujidhihirisha baada Hati Fungani ya Makazi (FHF) kuvutia uwekezaji mara sita zaidi ya kiwango kilicholengwa.

Hatifungani hiyo inayoratibiwa na Stanbic Bank Tanzania, imekusanya Sh33.08 bilioni kutoka kwa wawekezaji mbalimbali ikilinganishwa na lengo la awali la Sh5 bilioni.

Kutokana na mwitikio huo, First Housing Finance ilipata kibali kutoka Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana Tanzania (CMSA) kukubali Sh28.15 bilioni kutumika kuongeza uwezo wa utoaji wa mikopo ya nyumba kwa Watanzania.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa First Housing Finance Tanzania, Charles Mugila amesema mafanikio hayo yanaonyesha kiwango kikubwa cha imani ambacho wawekezaji wanaendelea kuwa nacho kwa taasisi hiyo na mwelekeo chanya wa sekta ya fedha nchini.

Amesema fedha zilizopatikana zitatumika kupanua huduma za mikopo ya nyumba ili kuwafikia Watanzania wengi zaidi wanaohitaji makazi bora na nafuu.

“Huu ni ushahidi kwamba wawekezaji wana imani na taasisi yetu pamoja na fursa zilizopo katika sekta ya makazi. Fedha hizi zitasaidia kuongeza uwezo wetu wa kufadhili mikopo ya nyumba na kuchangia juhudi za kupunguza changamoto ya upatikanaji wa makazi,” amesema Mugila.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA), Nicodemus Mkama.

Mafanikio ya hati fungani hiyo, yamekuja wakati Tanzania ikiendelea kushuhudia ongezeko la mahitaji ya nyumba kutokana na ukuaji wa miji, ongezeko la watu na upanuzi wa shughuli za kiuchumi.

Kuorodheshwa kwa Hati Fungani ya Makazi katika Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) Juni 9, 2026 pia kumeongeza thamani ya uwekezaji katika hati fungani za kampuni kutoka Sh2.03 trilioni hadi Sh2.06 trilioni, hatua inayodhihirisha ukuaji wa masoko ya mitaji nchini.

Mtendaji Mkuu wa CMSA, Nicodemus Mkama amesema mafanikio ya mauzo ya hati hiyo yanaashiria kuimarika kwa mazingira ya uwekezaji na kuongezeka kwa uelewa wa wananchi, kuhusu fursa zinazotolewa na masoko ya mitaji.

Kwa mujibu wa takwimu za CMSA, wawekezaji binafsi walichangia asilimia 96.63 ya usajili wote huku wawekezaji wa taasisi wakichangia asilimia 3.37.

Mkama amesema ushiriki huo mkubwa wa wawekezaji binafsi unaonyesha kuwa Watanzania wengi zaidi wanaanza kuona masoko ya mitaji kama njia salama na yenye tija ya kukuza mitaji yao.

“Mafanikio haya yamechangiwa na mazingira mazuri ya sera na udhibiti yaliyowekwa na Serikali pamoja na hatua mbalimbali zilizochukuliwa kuhamasisha uwekezaji kupitia masoko ya mitaji,” amesema.

Alitaja baadhi ya hatua hizo kuwa ni pamoja na maboresho ya mifumo ya udhibiti na kuondolewa kwa kodi ya zuio kwenye mapato yatokanayo na hati fungani za kampuni, jambo ambalo limeongeza mvuto kwa wawekezaji.

Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Uwekezaji Benki wa Stanbic Bank Tanzania, Sarah Mkiramweni amesema mafanikio ya hati fungani hiyo yanaendelea kuimarisha nafasi ya Tanzania kama moja ya masoko muhimu ya mitaji katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Amesema mfumo wa udhibiti uliopo nchini pamoja na kuongezeka kwa idadi ya wawekezaji wa aina mbalimbali umeendelea kujenga mazingira mazuri ya mafanikio ya utoaji wa hati fungani na bidhaa nyingine za uwekezaji.

“Mafanikio haya yatasaidia pia juhudi za Serikali za kuongeza upatikanaji wa makazi kwa wananchi kupitia upanuzi wa mikopo ya nyumba na upatikanaji wa fedha nafuu kwa taasisi zinazotoa huduma hizo,” amesema.

Amesema Stanbic itaendelea kuwa mstari wa mbele katika kusaidia taasisi mbalimbali kupata mitaji kupitia masoko ya fedha na mitaji kwa kutumia zana mbalimbali za kifedha ikiwemo hati fungani.

“Tunajivunia kuwa sehemu ya mafanikio haya. Hii inaonesha uwezo wa soko la Tanzania kuvutia mitaji ya ndani na kutoa suluhisho la muda mrefu kwa taasisi zinazohitaji fedha za maendeleo,” amesema.