Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kilolo yageukia ufuta kuukabili ukame

Wakulima wilayani Kilolo wakiwa wamebeba mbegu ya ufuta aina ya Lindi 02  tayari kuanza msimu wa kilimo na kukabiliana na ukame.

Muktasari:

  • Utekelezaji wa mkakati huo wa kuongeza uzalishaji wa zao la ufuta umeanza kwa kusambaza mbegu bora kwa wakulima, hatua inayolenga kukabiliana na athari za ukame na kuongeza kipato cha kaya.

Iringa. Serikali ya Wilaya ya Kilolo mkoani Iringa imejipanga kuongeza uzalishaji wa zao la ufuta kwa wingi katika msimu huu wa kilimo 2025/2026, kufuatia wakulima wa kata tatu kupokea mbegu bora zinazolenga kuimarisha uzalishaji wa zao hilo linalostahimili ukame.

Hatua hiyo imechukuliwa wakati maeneo ya kata za Nyanzwa, Ruaha Mbuyuni na Mahenge yakikabiliwa na changamoto ya ukame, hali inayolazimisha serikali ya wilaya kuelekeza nguvu kwenye mazao yanayoweza kustahimili mabadiliko ya tabianchi.

Wakizungumza na Mwananchi kwa njia ya simu, leo Januari 26, 2026, wakulima kutoka maeneo hayo wamesema mpango wa ugawaji wa mbegu bora umeongeza imani yao ya kuendelea kulima ufuta kama zao la kibiashara lenye soko la uhakika.

Mkulima wa Kata ya Nyanzwa, Kijiji cha Mgowelo, Samwel Kambatini amesema kwa muda mrefu wakulima wamekuwa wakikumbwa na changamoto ya upatikanaji wa mbegu bora, hali iliyokuwa ikisababisha mavuno madogo na kukatisha tamaa.

“Kupatikana kwa mbegu za ufuta aina ya Lindi 02 kunatarajiwa kuongeza uzalishaji endapo wakulima tutazingatia kanuni bora za kilimo tulizoelekezwa na wataalamu wa kilimo wa halmashauri,” amesema Kambatini.

Kwa mujibu wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilolo, jumla ya kilo 230 za mbegu bora za ufuta zimegawiwa kwa wakulima 117 Januari 23, 2026, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuhamasisha kilimo cha zao hilo.

Imeelezwa kuwa mpango huo unalenga kutatua changamoto ya upatikanaji wa mbegu bora, kuongeza uzalishaji wa ufuta na kuinua kipato cha mkulima.

Ofisa Kilimo wa Halmashauri ya Kilolo, Michael Mwaisondola amesema mazao ya wakulima yatakusanywa na kuuzwa kwa mfumo wa stakabadhi ghalani ili kuhakikisha mkulima anapata bei inayostahili.

“Ongezeko la uzalishaji, halmashauri inanufaika kwa kuongeza mapato ya ndani kupitia ushuru wa mazao, hatua itakayosaidia kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi,” amesema Mwaisondola.

Ameongeza kuwa amesema mfumo huo utaondoa walanguzi waliokuwa wakinufaika na jasho la wakulima kwa kununua mazao kwa bei ya chini wakati wa mavuno.

Kwa upande wake, diwani wa Kata ya Mahenge, Baraka Kidenya amesema mpango wa kugawa mbegu bora umeongeza hamasa kwa wakulima na kuonyesha dhamira ya Serikali kuboresha maisha ya wananchi wa vijijini.

“Niseme tu kuwa Serikali itaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa wakulima ili kilimo cha ufuta kiwe chanzo endelevu cha kipato na maendeleo ya Wilaya ya Kilolo,” amesema Kidenya.