LHRC yabainisha mbinu mbadala kukabili bei ya mafuta
Muktasari:
- Yapendekeza Serikali ianzishe mradi wa kuwa na mkongo wa taifa wa gesi asilia katika mikoa yote nchini, hatua itakayosadia pale itakapokuwa inatokea changamoto ya uhaba wa mafuta.
Dar es Salaam. Wakati kukiwa na ongezeko la bei ya mafuta nchini, Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kimeishauri Serikali itanue na kuanzisha vituo vya uhifadhi wa gesi asilia katika mikoa yote nchini, ili kukabiliana na uhaba wa nishati ya mafuta.
Pia imeshauri Serikali ianzishe mradi wa kuwa na mkongo wa taifa wa gesi asilia katika mikoa yote nchini, hatua itakayosaidia pale itakapotokea changamoto ya uhaba wa mafuta.
LHRC inasema hayo ikiwa ni siku nane zimepita tangu Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura) itangaze ongezeko la bei za mafuta, ambapo kwa Jiji la Dar es Salaam, bei ya petroli imepanda kutoka Sh2,864 Machi hadi kufikia Sh3,820 Aprili 2026.
Ongezeko hilo linatajwa kuchangiwa kwa kiasi kikubwa na hali ya sintofahamu katika soko la kimataifa la mafuta, hususan kutokana na mvutano wa kijeshi Mashariki ya Kati unaohusisha Marekani, Israel na Iran.
Kwa kawaida, bei za mafuta nchini Tanzania hutegemea zaidi gharama za uagizaji kutoka soko la dunia pamoja na mabadiliko ya thamani ya fedha za kigeni, hali inayofanya bei kupanda au kushuka kulingana na mwenendo wa kimataifa.
Hata hivyo, ipo taarifa ya soko la kimataifa kupata ahueni baada ya bei ya mafuta kushuka kwa kasi na hisa kupanda, kutokana na tangazo la kusitishwa kwa mapigano kwa masharti kati ya Marekani na Iran lililotolewa na Rais wa Marekani, Donald Trump.
Baada ya Trump kuahirisha kufanya mashambulizi dhidi ya Iran kwa masharti kwamba Tehran ikubali kusitisha mapigano kwa wiki mbili na kufungua njia muhimu ya usafirishaji wa mafuta duniani, ya mlango wa bahari wa Hormuz.
Athari za tangazo hilo zilionekana haraka katika masoko ya nishati, ambapo bei ya mafuta ghafi aina ya Brent, kipimo cha kimataifa, ilishuka kwa karibu asilimia 15 hadi kufikia Dola 93 (Sh239,307) kutoka Dola 114 (Sh293,346) kwa pipa.
Akizungumza leo, Jumatano, Aprili 8, 2026, katika makao makuu ya LHRC, Kijitonyama, jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wake, Dk Anna Henga, amesema LHRC inaona hatari kubwa ya kuongezeka kwa ukali wa maisha katika jamii, ambayo ina athari ya moja kwa moja dhidi ya haki ya kuishi kama inavyoainishwa katika Ibara ya 14 ya Katiba ya Tanzania, pamoja na haki ya maendeleo ya ustawi.
"Ongezeko la bei ya mafuta lina athari kubwa katika sekta ya uzalishaji na usafirishaji, ambayo kwa kiwango kikubwa hutegemewa na sekta nyingine zote katika usambazaji wa bidhaa na ufikiwaji wa huduma za msingi kwa wananchi.
"Athari hii hugeuka na kwenda moja kwa moja kwa wananchi, ambao ndio walaji wa mwisho wa bidhaa na huduma hizo, athari ni kupanda kwa bei za bidhaa, hasa bidhaa za chakula, vinywaji, dawa, vifaa tiba, pembejeo za kilimo na ujenzi, kuongezeka kwa gharama za usafiri na kufikika kwa huduma za msingi kama vile shule, vyuo, huduma za afya na matibabu, sokoni na viwandani," amesema.
Akieleza zaidi, amesema kuna hatari ya kupungua kwa thamani ya fedha kutokana na kupungua kwa shughuli za kibiashara zinazosababishwa na hali ya ugumu wa maisha.
Henga pia amesema kuongezeka kwa ukatili wa kijinsia, hasa kwa wanawake na watoto, kutasababishwa na hali ya ugumu wa maisha katika jamii, pamoja na changamoto za afya ya akili.
"Hatari ya kuongezeka kwa vitendo vya uvunjifu wa sheria kwa kisingizio cha kukwepa masharti ya kikodi na kibiashara ili kupunguza ukali na gharama za maisha," ameongeza.
Akitoa mapendekezo mengine kwa Serikali, Henga amesema itoe taarifa rasmi ya ufafanuzi kuhusu ongezeko la bei ya mafuta, ikiwa nchi iliweka akiba ya mafuta ili kukabiliana na mtikisiko wa upatikanaji wa mafuta katika soko la dunia kwa takribani miezi mitatu, kama ilivyotolewa katika taarifa rasmi ya Serikali Februari 28, 2026.
Aidha, Serikali ipeleke mapendekezo ya mabadiliko ya Sheria ya Fedha kwa hati ya dharura katika Kikao cha 4 cha Mkutano wa 13 wa Bunge ili kufuta kwa asilimia 50 ya tozo zote zilizowekwa kwenye kila lita ya mafuta ili kukabiliana na ugumu wa maisha kwa wananchi kwa muda wa miezi sita.
"Kuimarisha na kutekeleza mikakati ya kuongeza akiba ya taifa ya mafuta angalau kwa miaka miwili mfululizo,” imesema.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Uwezeshaji na Ufuatiliaji wa Haki za Binadamu LHRC, Deogratius Bwire, amesema Serikali inapaswa kulinda haki za wananchi, ambazo ni kuishi, ustawi na maendeleo hivyo, kupaa kwa gharama za maisha kutaathiri haki hizo.
Hata hivyo, LHRC inasema hayo huku taasisi, wadau na vyama vya siasa vikitoa mapendekezo mbalimbali ya kutaka afueni. Chama cha Mapinduzi (CCM) kimeielekeza Serikali kuangalia uwezekano wa kutoa ruzuku na kuhamasisha kupunguzwa matumizi ya nishati hiyo katika ofisi za umma.
Pia, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimetoa pendekezo kwa Serikali ili kuleta unafuu wa gharama za nishati hiyo muhimu kwa kutoa ruzuku.