Mataifa 23 kushiriki Sabasaba, waoneshaji 3,891 wathibitishwa
Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk Judith Kapinga, akizungumza kuhusu maandalizi na umuhimu wa Maonesho ya 49 ya Kimataifa ya Biashara Dar es Salaam (Sabasaba).
Muktasari:
- Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba) yanayotarajiwa kuanza Juni 28, 2026, yatashirikisha mataifa 23 na waoneshaji 3,891, huku zaidi ya watembeleaji 590,000 wakitarajiwa kuhudhuria. Serikali imesema maandalizi yamekamilika, ikiboresha miundombinu na kuanzisha mfumo wa tiketi za kidijitali ili kuongeza ufanisi wa huduma.
Dar es Salaam. Mataifa 23 tayari yamethibitisha kushiriki katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (DITF), maarufu Sabasaba yanayotarajia kufanyika kuanzia Juni 28 hadi Julai 13, 2026.
Pia waoneshaji zaidi ya 3,891 wakitarajiwa kushiriki, wakiwemo zaidi ya 430 kutoka nje ya nchi. Idadi ya watembeleaji inatarajiwa kuzidi 590,000.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo, Juni 26, 2026, Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk Judith Kapinga, maonesho hayo pia yanatarajiwa kuzalisha ajira zaidi ya 12,800 za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja.
"Maandalizi yamekamilika kwa kiwango kikubwa. Tumekarabati kumbi za maonesho, ofisi, matenti, maeneo ya huduma za chakula, mifumo ya maji na vyoo, pamoja na kuboresha mandhari kwa ajili ya maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 50," amesema.
Amesema Serikali imeboresha matumizi ya teknolojia kwa kuanzisha mfumo utakaowawezesha watembeleaji kupata maelekezo ya mabanda kupitia simu zao za mkononi.
"Mwaka huu tiketi zote za kuingia viwanjani zitapatikana kidijitali kupitia TanTrade Biashara App. Hatutatumia tena tiketi za karatasi, hatua ambayo itaongeza ufanisi wa huduma," amesema.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade), Latifa Khamis, amesema maonesho ya mwaka huu yanatarajiwa kuwa miongoni mwa makubwa zaidi kuwahi kufanyika nchini.
"Maonesho haya yataendelea kuwa jukwaa muhimu la kutangaza bidhaa za Tanzania, kuvutia uwekezaji na kuongeza mauzo ya bidhaa zetu katika masoko ya kimataifa," amesema Latifa.
Amesema maonesho ya mwaka huu yanatarajiwa kukusanya washiriki kutoka mataifa 23 na kuendelea kuimarisha nafasi ya Tanzania kama kitovu cha biashara na uwekezaji katika ukanda wa Afrika Mashariki na kwingineko.