Matumizi ya intaneti yapaa, simu janja bado changamoto

Dar es Salaam. Pamoja na kuongezeka kwa idadi ya watumiaji wa intaneti hadi kufikia milioni 35.8, matumizi ya simu janja kwa Watanzania bado ni changamoto, huku gharama kubwa zikitajwa kuwa kikwazo.

Kwa jumla watumiaji wa huduma za simu waliongezeka kwa asilimia 4.7 hadi Desemba 2023 na kufikia milioni 70.3 ikilinganishwa na miezi mitatu nyuma. Kampuni ya Tigo iliongoza kwa kuongeza wateja wengi zaidi ndani ya miezi mitatu kutoka wateja milioni 18.5 hadi milioni 19.6.

Ripoti ya robo mwaka unaoishia Desemba 2023, inayotolewa na Mamlaka ya Mawasiliano Nchini (TCRA) inaonyesha watumiaji wa simu za kawaida (vitochi) idadi imeongezeka hadi kufikia asilimia 85.62 nchini kote, ikitoka asilimia 83.66.

Hata hivyo, wapo wanaotumia simu janja na vitochi kwa wakati mmoja, kwani matumizi ya simu jaja kwa ajili ya intaneti nayo yaliongezeka na kufikia asilimia 32.1 kutoka asilimia 30.7 iliyoripotiwa miaka mitatu iliyopita.

Hata hivyo, watoa huduma wa intaneti wameongeza usambazaji mtandao wa 3G, 4G kwa asilimia 3 hadi 4 katika maeneo mbalimbali, huku ubora na kasi navyo vikiongezeka, hususani kasi ya kupakua ambayo ilifikia wastani wa Mb 11.03 kwa sekunde kwa kifaa cha simu.

Mtandao wa simu wa Tigo ulitajwa kuongoza kwa ubora wa mtandao nchini na hata taasisi ya Kimataifa ya Ookla ambayo hufuatilia ubora wa huduma za mtandao iliupatia tuzo kwa kuwa mtandao wenye kasi zaidi Tanzania mwaka 2023.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Moses Ismail alisema ni wakati muafaka kwa serikali na watoa huduma kutoa ruzuku ya vifaa (CPEs) kwa wasio na uwezo wa kuvimudu.

Alisema kuna mafanikio makubwa katika kuwawezesha wananchi kupata intaneti yenye kasi, lakini wanaofikiwa hawana vifaa vya kupata huduma hiyo.

"Ipo haja kwa Serikali kuangalia upya kampeni ya kuondoa ushuru kwenye (gudgets), inaonekana haikuwa na matarajio husika, ndiyo maana vifaa vimeendelea kuuzwa kwa bei kubwa," alisema.

Aliongeza kuwa Serikali inapaswa kuendelea kupunguza na kuondoa kodi na kuweka utaratibu wa kuhakikisha waagizaji wa simu za mkononi wanauza kwa bei ya chini kwa sababu ya msamaha huo wa kodi.

Kuhusu matumizi ya simu janja kuwa chini, Mkurugenzi wa Masuala ya Kisekta wa TCRA, Felician Mwesiga alisema mipango inaendelea kati ya mamlaka na watoa huduma ili kuchunguza njia za kuboresha ufikiaji wa simu janja za gharama nafuu, lengo kuu likiwa ni kuongeza matumizi ya intaneti.