Mfumuko wa bei wazidi kushuka Aprili

What you need to know:

  • Ofisi ya Taifa ya Takwimu imetoa ripoti ya mfumuko wa bei ikionyesha imezidi kuleta ahueni kwa mwezi Aprili ikilinganishwa na Machi.

Dar es Salaam. Ripoti ya mfumuko wa bei inaonyesha mwezi Aprili umezidi kushuka huku bei za bidhaa zikiendelea kuwa himilivu sokoni.

Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) ripoti yake inaonyesha mfumuko huo umeshuka hadi asilimia 4.3 Aprili ikilinganishwa na asilimia 4.7 Machi mwaka huu.

“Mwenendo huu unamaanisha kasi ya kubadilika kwa bei za bidhaa Aprili kulipungua ikilinganishwa na Machi ambapo kasi ya kubadilika kwa bei hizo ilikuwa juu,” imesema sehemu ya taarifa hiyo.

Kiwango hicho ni kidogo ikilinganishwa na miezi kumi na moja iliyopita ambayo mfumuko wa bei ulikuwa juu.

Mara ya mwisho Tanzania kurekodi mfumuko mdogo wa bei ikilinganishwa na wa Apeili 2023 ilikuwa Mei 2022 ambapo mfumuko wa bei ulikuwa asilimia nne.

Hata hivyo kwa upande wa vyakula na vinywaji visivyo na vilevi Aprili 2023 mfumuko ulipungua hadi asilimia 9.1 kutoka asilimia 9.7 iliyorekodiwa Machi 2023 na kwa upande wa bidhaa nyingine zisizokuwa za chakula, mfumuko pia ulishuka kutoka asilimia 2.3 kutoka asilimia 2.7 Aprili.