Michango ya harusi inavyowaumiza Watanzania kiuchumi

Watanzania ni watu wenye desturi ya kujitoa katika kusaidia na kushiriki kwa namna mbalimbali katika mambo ya kijamii na moja kati ya mambo hayo ni matukio ya sherehe za harusi, wengi hushiriki kwa namna ya kuchangia fedha ili kufanikisha sherehe hiyo.

Changamoto inaibuka pale jambo hilo sasa linapogeuka kuwa  mwiba unaochoma ustawi wa kimaisha na hali za kifedha kwa wenye harusi na wanaochangia, na wengine baada ya tukio la harusi kupita, wanajikuta hoi kifedha na pengine na wao wangehitaji kuchangiwa.

Upande wa kwanza, wenye sherehe hiyo bajeti wanazifanya kubwa sana, mfano gharama kununua mavazi, kukodi ukumbi, vyakula, muziki mkubwa, magari, kuwalipa washereheshaji na mengine.

Tukilinganisha gharama hizo na uwezo wa kifedha wa familia inayoandaa sherehe ni kama mlima na kichuguu, ni msukumo tu wa kuonesha ufahari na usasa ndio unaofanya familia kujitwika zigo hilo.

Matokeo yake ni kuweka kiasi kikubwa cha michango kwa wengine, kuuza au kuweka rehani vitu vya thamani ili kupata fedha, au ngoma inapokuwa nzito, familia nyingine zinalazimika kukopa fedha na vitu kwa ajili ya kutimiza mahitaji ya sherehe hiyo.

Hatima yake familia nyingi na hata kwa wanandoa wapya wanapitia wakati mgumu kiuchumi baada ya harusi, hali hiyo inaathiri vipato binafsi, kujikosesha baadhi ya mahitaji muhimu kwa kipindi fulani ili kupata fedha kulipia madeni.

Si ajabu katika jamii ya Kitanzania na ukweli ni kuwa harusi nyingine zinaacha madeni ya kuogofya kwa familia baada ya sherehe hizo kupita.

Upande wa pili, wachangiaji changamoto inaanzia pale michango inapokutana, mathalan michango ya harusi zaidi ya tatu inakutana kwa pamoja, uzoefu wa kimazingira unaonesha kwa Mtanzania wa kawaida anayefanya kazi ya mshahara kutoa mchango wa laki 2 au 3 kwa mkupuo mmoja inampunguzia matumizi yake ya msingi, wengine ikiwemo mahitaji ya familia, ili tu aweze kuchangia harusi.

Hali inaweza kuwa ngumu zaidi kwa anayetakiwa kutoa mchango na hana chanzo cha kipato cha kuaminika na ndio wengi kwa mujibu wa matokeo ya ripoti ya utafiti wa watumiaji wa huduma za kifedha nchini (Finscope 2023).

Kwa wakina mama wajasiriamali, michango ya harusi ni mithili ya gunia la mawe, linaelemea na kuumiza.

Mama Nusaiba ameeleza makala haya kuwa mauzo na faida ya biashara yake ya kuuza mihogo ya kukaanga mwezi huu yote atatoa mchango wa harusi.

“Mtoto wa kiume wa ndugu yangu anaoa mwezi ujao, na mimi ndiyo mama mkubwa,” ameeleza mama huyo akiashiria kuwa hana budi kuchangia harusi hata kama inamuumiza katika biashara yake.

Kwa jumla wakina mama wengi harusi zinawakaba zaidi kwa sababu zinatanguliwa na matukio mengine yanayoongeza gharama, mfano usiku wa vyombo, kukata sare ya kitambaa kwa ajili ya siku ya harusi na mengine.

Sherehe za harusi zifanyike kulingana na uwezo wa familia, ufahari wa harusi haumaanishi kuwa ndio ndoa bora, na upangaji wa michango uzingatie hali za watu kifedha na kimaisha.

Pia, mwamko huu wa kuchangiana harusi ufanyike hivyo katika mambo mengine muhimu kijamii na ya dharura, kwa mfano matibabu. Watanzania wengi ni wepesi kuchangia harusi ya bajeti hata ya milioni 20, lakini inaweza kuwa ngumu kuchangia matibabu ya mtu ya shilingi milioni 3.