Mpango mzima mabasi ya mwendokasi majijini

Mataifa mengi yanayoendelea yanakabiliwa na changamoto ya uwiano sawa kati ya idadi ya miundombinu na huduma za kijamii zinazohitajika.


Changamoto hii wakati mwingine huwa mzigo mzito unaopunguza kasi ya maendeleo ya taifa husika katika nyanja tofauti.

Miongoni mwa miundombinu muhimu ni ya uchukuzi, ambayo hurahisisha usafiri wa watu na bidhaa kutoka sehemu moja kwenda nyingine kwa ajili ya shughuli mbalimbali.

Mataifa mengi yanayoendelea bado yanapambana kuimarisha miundombinu yake ya uchukuzi ili kurahisisha usafiri na usafirishaji ambayo ni nyanja muhimu katika kukuza uchumi.

Tanzania ikiwa miongoni mwa mataifa yanayoendelea kiuchumi ilibuni mradi wa kurahisisha usafiri wa umma maarufu kama mwendokasi (BRT) kwa ajili ya usafiri wa abiria ndani ya Jiji la Dar es Salaam.

Licha ya changamoto zilizopo, kupitia mradi huu unaosimamiwa na Wakala wa Mabasi yaendayo Haraka (Dart), wananchi wamepata nafuu ya usafiri kutokana na uharaka wa mabasi na uwezo wa basi moja kupakia watu wengi kwa wakati mmoja.

Kutokana na ongezeko la watu katika majiji mengine nchini, Dart unakusudia kupeleka huduma katika majiji hayo ifikapo 2030 ili kurahisisha usafiri wa umma.

Novemba mwaka jana Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-Tamisemi), Angellah Kairuki aliitaka Bodi ya Ushauri ya Dart kubuni mikakati ya kuboresha huduma ya usafiri ndani ya Jiji la Dar es Salaam na kupanua wigo wa huduma hiyo katika majiji mengine yanayokidhi vigezo yakiwamo Arusha, Mbeya, Tanga, Mwanza na Dodoma.

Alisema wakati wa uanzishwaji wa Wakala huo ulikuwa ni kwa ajili ya Jiji la Dar es Salaam lakini kuna majiji mengine yanatamani kupata huduma ya mabasi yaendayo kwa haraka, hivyo kuwataka kuweka nguvu kulifanikisha hilo.

Katika mahojiano na Mwananchi Kaimu Meneja wa Mipango ya Usafirishaji wa Dart, Mohamed Kuganda anaeleza namna mradi wa BRT, utakavyotekelezwa kwenye majiji hayo na njia zitakavyokuwa.

Mhandisi Kuganda anasema mwaka 2021, Dart ilifanya tathimini katika majiji nchini na matokeo yalionyesha uhitaji wa mradi huo kwa asilimia 85 Dar es Salaam Arusha (70%), Dodoma (80%), Tanga (88%), Mbeya (95%) na Mwanza (90%).

Pamoja na uhitaji huo, alisema mradi utatekelezwa katika maeneo hayo endapo sheria ya usafiri wa mijini itapitishwa. Hatua iliyofikiwa sasa ni andiko la sheria hiyo kuwasilishwa kwa mara nyingine katika baraza la mawaziri kwa ajili ya hatua zaidi.

Akizungumza na waandishi wa habari hivi karibuni Kaimu Ofisa Mtendaji Mkuu wa Dart, Dk Eliphas Mollel, anasema huenda rasimu ya sheria hiyo ikatua bungeni Desemba mwaka huu.

Licha ya sheria, Dk Mollel anasema jambo lingine litakalofanikisha utekelezaji wa mradi huo kwa haraka ni utayari wa Serikali na upatikanaji wa fedha za miundombinu.

Dodoma

Kwa mujibu wa Dart, Dodoma ndilo litakalokuwa jiji la kwanza kuwa na huduma ya usafiri wa mabasi yaendayo haraka baada ya Dar es Salaam.
Kuganda anasema licha ya kuwa tathimini haionyeshi kuwa Dodoma inauhitaji mkubwa na mradi huo kuliko majiji mengine lakini litaanza kutokana na umaalumu wake wa kuwa makao makuu ya nchi.
Anasema njia katika Jiji la Dodoma zitakazohusika baadhi tayari barabara zake zimejengwa kwa namna inayoruhusu mradi huo kutekelezwa kwa urahisi.

Njia hizo ni zile za Ihumwa na Zuguni, Nanenane kwenda Sabasaba ambazo zote zitatumia barabara ya Dar es Salaam.

Njia nyingine ni inayokwenda Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), yenye kilomita 12 ambayo itatokea eneo la Nong’ona ndani ya Chuo hicho, kupitia barabara ya Udom kwenda Sabasaba.

“Korido nyingine ni barabara upande wa kwenda Singida itakayotokea Nkuhungu kwenda mpaka Sabasaba nyingine ni ya kwenda Arusha itakayokuwa na safari tatu tatu,” anasema.

Katika sarafi hizo ipo itakayoanzia Veyula kwenda mjini Sabasaba yenye kilomita 20, nyingine itaanzia St. Gema yenye kilomita 11 na ile ya Mkonze kwenda Majengo yenye kilomita 9.5.
 

Mwanza

Jiji la Mwanza barabara zilizopewa vipaumbele katika hatua za awali ni Igoma kwenda katikati ya jiji kupitia barabara ya Nyerere itakayokuwa na urefu wa kilomita 10.

Awamu ya pili itahusisha Buhongwa kwenye kituo kikuu cha daladala kupitia barabara ya Kenyatta kwenda mjini, ambayo itakuwa na urefu wa kilomita 13.

Katika awamu ya tatu barabara ya Uwanja wa Ndege kupitia Makongo kwenda mjini yenye urefu wa kilomita nane itahusika ikiwa ni maalumu kwa ajili ya abiria wanaotumia uwanja wa ndege.

“Tumechagua barabara hizo kwakuwa ndizo zenye idadi kubwa ya abiria, endapo baadaye itatokea kukawa na mahitaji kwa barabara zingine hatutaacha kupeleka miundombinu yetu huko,” anasema Kuganda.

Karakana ya mabasi hayo mkoani Mwanza inatarajiwa kuwepo katika maeneo matatu ya Nyegezi lenye ukubwa wa mita za mraba 65,000, Nyegezi Kona (mita za mraba 70,000) na Nyakato Tanesco (mita za mraba 68,000).
 

Arusha

Tathimini ya Dart inaonyesha kwa Jiji la Arusha, BRT inaweza kuwekwa katika barabara ya Kwa Mromboo kwenda Mbauda kupitia barabara ya Nyerere kwenda mjini.

Nyingine ni ya Old Moshi itakayoanzia Suye kwenda mjini na itaishia eneo la Burca kwenye viwanja vya Tanapa. Barabara hizo za Arusha zina urefu wa kilomita 14.4.

Karakana inapendekezwa kuwapo maeneo ya Burca lenye mita za mraba 104,000 na Kwa Mromboo eneo linalomilikiwa na Polisi kikosi cha FFU lenye ukubwa wa mita za mraba 108,000.

“Tutajitahidi tuombe uongozi wa mkoa maeneo hayo yahifadhiwe kwa ajili ya kuweka karakana yetu,” anasema Kuganda.
 

Mbeya

Kuganda anasema BRT inapendekezwa Igawilo kwenda kituo kikuu cha mabasi barabara ikiwa na urefu wa kilomita 20. Mbalizi kwenda kituo kikuu cha mabasi yenye kilomita 18 na Nsalaga kwenda kituo kikuu cha mabasi yenye kilomita 18.

Deogratius Mwakisisile, mkazi wa Mbeya anasema ujio wa mabasi hayo utawaondolea adha ya usafiri.
 

Tanga

Mkoani Tanga baada ya bandari kufufuliwa, Kuganda anasema barabara zinazopewa kipaumbele katika mradi huo ni Ngamiani kwenda Sahare (kilomita 9.7), Raskazone kwenda Mikanjuni (kilomita 7.27), Donge kwenda Sahare (kilomita tisa) na Magomeni kupitia Sahare kwenda Raskazone (kiliometa tisa).

“Utekelezaji wa mradi huu kwa barabara za Tanga nao unaweza kutekelezwa kwa awamu kulingana na namna fedha zitakapopatikana,”anasema Kuganda.

Mmoja wa wakazi wa Tanga, Abdul Ramadhani, akitoa maoni yake kuhusu barabara tajwa hapo, anasema Dart wala hajakosea kwa kuwa ndio barabara kubwa zinazotumiwa kwa wingi sio tu kwa wafanyakazi kwenda makazini bali hata wafanyabiashara.

Ramadhani anasema ujio wa mabasi hayo, utazidi kulipendezesha jiji hilo la Tangaambalo lina historia katika biashara kwa nchi hii.
 

Mchumi afunguka

Oscar Mkude, ambaye ni mchambuzi wa masuala ya uchumi na kijamii, anasema wazo la kupeleka huduma za mabasi yaendayo haraka katika majiji mengine ni zuri japo huenda ikachukua muda mrefu kurejesha gharama za uwekezaji.

“Kwa Jiji la Dodoma mradi huo kwenda ni sawa, kwa kuwa uleni mji wa Kiserikali, lakini kwa majiji mengine nina wasiwasi kama Dart itaweza kurudisha fedha ambazo itakuwa imewekeza katika miundombinu ukizingatia kuwa ni fedha ambazo zinakopwa na zinatakiwa kurudishwa,”anasema Mkude.

Hata hivyo anashauri ni uwekezaji huo ukafanywa kwenye kupananua barabara za majiji hayo ili ili wananchi wasafiri kwa urahisi.

“Huko mikoani ni tofauti na Dares Salaam, ambapo wengi shughuli zao ni za kuajiriwa na mara nyingi viwandani, kwani huko wengi wamejiajiri na pia hakuna msongamano mkubwa wa magari hivyo huwezi kupalinganisha na Dar ambapo watu asubuhi wanaelekea sehemu moja na jioni kurudi,” anasema.

Anasema katika majiji mengine hata kama kuna msongamano wa watu ni muda mfupi hivyo ni vyema wakatafakari vizuri ili mabasi hayo yakipelekwa yasijeyakajikuta yanakaa vituoni kusubiria abiria.