Namna ya kulinda namba ya simu

“Laini yangu ilifungwa, baada ya muda nikawa nikipigiwa simu anapokea mtu mwingine, nilienda kwa mtoa huduma wangu lakini nikaambiwa amepewa mtu mwingine.”

Ndivyo alivyoanza kusimulia John Julius, mkazi wa Tabata ambaye mbali na kufungiwa laini, hakuweza kupata zaidi ya Sh30,000 zilizokuwa katika laini hiyo.

“Sasa sijui huwa kinatokea nini, nilienda makao makuu ya ofisi hiyo na kukuta jina la mtu mwingine ndiyo linasomeka katika namba yangu, sikuweza hata kuhudumiwa zaidi ya kuambiwa nikamchukue huyo mtu niende naye, namtoa wapi,” alimaliza kwa kuhoji.

Julius anawakilisha kundi kubwa la watumiaji wa mitandao nchini ambao baadhi pasipo kujua kuwa laini zao zisipotumika ndani ya miezi mitatu zitafungiwa kwa mujibu wa sheria na kwa taratibu za kila kampuni baada ya muda maalumu namba hiyo huweza kuuzwa kwa mteja mwingine.

Visa vya watu laini zao kupewa watu wengine vinawakuta zaidi watu ambao hufanya safari za kwenda nje ya nchi na kukaa kwa muda mrefu.

Hata hivyo, laini hizo hazifungwi bila taarifa, watoa huduma za simu wamekuwa na tabia ya kuwakumbusha wateja wake ambao hawajatumia laini zao kwa muda mrefu kuwataka waongeze salio ili namba zao zisifungwe kwa mujibu wa sheria.

"Si mitandao yote inayotoa taarifa, unaweza kukuta laini yako imefungwa na hakuna hata ujumbe mmoja uliokukumbusha kufanya nini ili usifungiwe, ni vyema watuambie," anasema Leina Kipeta.

Umuhimu wa kulinda laini yako unatokana na umuhimu wa simu katika shughuli za kila siku za binadamu na ukuaji wa teknolojia ya dijitali na fursa zake kama uchumi wa kidijitali.

Laini au namba ya simu inatumika kama utambulisho wa mtu katika ulimwengu wa kidijitali, hivyo laini imefungamanishwa kwa sehemu kubwa na uchumi wa kidijitali ambao ndiyo msingi wa uchumi endelevu katika zama hizi.

Kwa mujibu wa kanuni ya 25 (1) ya Kanuni za Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta kuhusu usajili wa laini za simu ya mwaka 2023, inaelekeza kwamba laini ya simu ya mkononi au kifaa cha mawasiliano kinachotumia laini ya simu kitasitishwa matumizi endapo laini hiyo haijatumika kwa siku 90 mfululizo.

Wakati huohuo, Kanuni ya 25 (2) inamuelekeza mtoa huduma kuwa hapaswi kusitisha matumizi ya laini hiyo endapo mteja atakuwa ametoa taarifa kwa maandishi kuwa laini hiyo haitatumika kipindi cha mfululizo kisichozidi miezi 12.

Mkurugenzi wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Dk Jabir Bakari anasema mbali ya uwepo wa sheria hiyo, kila kampuni ina kanuni zake ndogondogo za utekelezaji.

“Kama hatakuwa na uwezo wa kutumia laini yake kwa miezi mitatu, anatakiwa kutoa taarifa kwa mtoa huduma wake,” amesema Dk Jabir.
Kwa mujibu wa kampuni za simu Tanzania, utoaji wa taarifa hizo huweza kufanya mtumiaji kulinda laini yake isifungwe kwa kipindi ambacho haitatumika.

Mkurugenzi wa huduma kwa wateja wa kampuni ya huduma za simu ya Vodacom Tanzania, Harriet Lwakatare alisema: “Kanuni ya 25(2) inatuelekeza kuwa hatupaswi kusitisha matumizi ya laini hiyo endapo mteja atakuwa ametoa taarifa kwa maandishi kuwa laini hiyo haitatumika kipindi cha mfululizo kisichozidi miezi 12”.

Mkurugenzi wa Biashara kutoka Halotel, Abdallah Salum anasema kwao, baada ya miezi mitatu iliyopo kwa mujibu wa sheria mteja huongezewa siku 30 ambazo anaweza kuomba laini hiyo.

“Ikiwa hakutokea ndani ya siku hizo (90 za mwanzo na 30 za nyongeza), namba itawekwa na kuwa tayari kwa ajili ya kurejelezwa katika matumizi kupitia mtu mwingine,” anasema Salum.

Akizungumzia taratibu za utoaji wa taarifa, anasema mteja huweza kutoa taarifa katika maduka ya Halotel na huko atapewa utaratibu wa kufanya.
Kwa upande wa Mkuu wa kitengo cha bidhaa wa Tigo, Ndevonakieli Eliaki anasema ili mteja aweze kulinda namba yake isifungwe ikiwa hataitumia ndani ya kipindi fulani, anatakiwa kutembelea vituo vya kutolea huduma vya mtandao huo kutoa taarifa.

“Hii inaweza kufanyika kwa mteja kutembelea duka la Tigo lililo jirani yake ambapo watamuelekeza kuandika barua ya kuomba namba yake isifungwe,” anasema Eliaki.

Njia nyingine inayoweza kulinda laini isifungwe hata kama haikutumika kwa muda mrefu ni kuiwekea muda wa maongezi kila baada ya muda.

Kuhusu fedha ambazo zilikuwa katika laini ya mtumiaji, Lwakatare kutoka Vodacom anasema mteja ambaye laini yake imefungwa na anahitaji fedha zake, atatakiwa kufika katika duka la mtandao huo akiwa na namba ya utambulisho wa Taifa (NIDA) au kitambulisho kwa ajili ya kuomba kurejeshewa fedha hizo.

“Vodashop itafanya uhakiki wa umiliki wa awali wa laini hiyo na tukishajiridhisha tutaendelea na utaratibu wa kumrejeshea mteja huyo fedha zake,” anasema.

Kwa wateja wa Halotel, Salum anasema hata kama namba hiyo atapewa mtu mwingine, fedha za mtumiaji wa awali zitakuwa salama.

“Akihitaji kupewa fedha zake atapewa kwa sababu ile ni namba tu iliyotumika kufungua akaunti, lakini akaunti yake itatunzwa kwenye mfumo. Ila hela ikikaa kwa muda mrefu kwetu tutaipeleka Benki Kuu,” anasema Salum.

Kauli hiyo iliungwa mkono na Mkuu wa Kitengo cha Uendeshaji kutoka Tigopesa, Arnold Ngarashi ambaye anasema baada ya miaka mitano kama mteja hakudai fedha yake, basi itawasilishwa BoT lakini bado mteja huyo atakuwa na uwezo wa kuipata.

Ikiwa atahitaji fedha zake kabla ya muda huo, atalazimika kutembelea maduka ya Tigo yaliyo karibu yake akiwa na kitambulisho chake ambacho kinabeba taarifa za mteja zilizopo katika akaunti husika.

“Akaunti ya Tigopesa itaendelea kuwa salama hata kama namba yake ilifungiwa na kupewa mtu mwingine,” anasema.

Akizungumzia suala la fedha kupelekwa BoT, Dk Jabir anasema BoT wanao utaratibu wa kusimamia fedha hizo kwa sababu akaunti ya fedha katika simu ni sawa na ile ya benki ya CRDB, NMB.

Kwa mujibu wa Kifungu cha 31 cha Kanuni za Mifumo ya Malipo ya Kidijitali za mwaka 2015, kikisomwa pamoja na kifungu cha 56 (3) cha Sheria ya mifumo ya Taifa ya Malipo ya mwaka 2015, kinazitaka kampuni za simu kuzitambua akiba zilizomo kwenda akaunti za wateja wao ambazo hazijatumika kwa miaka mitano kama mali iliyotelekezwa.

Ikiwa kipindi hicho kitapita, akaunti hiyo huhesabika kama mfu (dormant account), hivyo fedha zilizopo katika akaunti husika zitawasilishwa BoT, lakini mhusika atakapozihitaji ataweza kuzipata.

Akizungumzia suala hilo, Gavana wa BoT, Emmanuel Tutuba amesema upo utaratibu ambao mtu huweza kuutumia kupata fedha zake, ikiwa ni pamoja na kuwasiliana na watoa huduma wake wa awali.

Fedha hizo pia hazitolewi kwa mmiliki pekee, bali hata kwa warithi ikiwa watafuata taratibu hata ikiwa imekaa zaidi ya miaka 10.

“Akiwasiliana na taasisi husika, akawapatia vielelezo vyote, wataviwasilisha kwetu, vikifanana watapewa hela hiyo,” anasema Tutuba.
Anasema kila kampuni ya simu, inao utaratibu wa kushughulikia suala hili ambao baadhi huangalia ikiwa laini inatumika au haitumiki, kuna wengine miezi mitatu, wengine hadi sita wakichukua laini kumpa mtu mwingine.

“Huwezi kusema laini zikae milele, ni sawa na kupanua wigo wakati kuna laini zisizotumika, sasa wakimpa mtu mwingine laini wataendelea kukaa na fedha kama baada ya miaka mitano watarejesha kama hazijatumika,” anasema Tutuba.

Anasema kampuni za simu nazo hupewa leseni ya uendeshaji huduma za kifedha kama za benki.

 

Idadi ya watumiaji wa huduma za simu nchini

Kwa mujibu wa TCRA, watumiaji wa mtandao wamekuwa wakiongezeka kila mwaka na sasa wamefikia milioni 67.11 Septemba mwaka jana, ikiwa ni ongezeko kutoka milioni 64.08 waliokuwapo Juni mwaka huo.

Ripoti hiyo inaonyesha kuwa mkoa wa Dar es Salaam unaongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya laini za simu (milioni 12.3), ukifuatiwa na Mwanza milioni 4.4, Arusha milioni 4.0 na Mbeya milioni 3.8.

Mikoa yenye idadi ndogo zaidi ya laini za simu zilizohai ni Kasini Unguja 92,336 na Kaskazini Unguja laini 61.360.