NMB yatajwa kinara ithibati usawa wa kijinsia Afrika

Muktasari:
- Cheti hicho kimetolewa na The Edge Certified Foundation ya Uswisi, taasisi inayoongoza duniani kwa mbinu bora za tathmini na udhibiti wa viwango vya biashara katika suala zima la usawa wa kijinsia, ambapo mwaka 2022, NMB ilikuwa benki ya kwanza Kusini mwa Jangwa la Sahara Afrika kutunukiwa cheti hicho.
Kwa mara ya pili katika kipindi cha miaka minne, Benki ya NMB imetunukiwa Cheti cha Ithibati ya kutambuliwa kuwa Kinara Katika Mgawanyo wa Kiuchumi Kwenye Suala la Usawa wa Kijinsia Mahali pa Kazi (EDGE Assess), miongoni mwa taasisi za fedha barani Afrika.
Cheti hicho kimetolewa na The Edge Certified Foundation ya Uswisi, taasisi inayoongoza duniani kwa mbinu bora za tathmini na udhibiti wa viwango vya biashara katika suala zima la usawa wa kijinsia, ambapo mwaka 2022, NMB ilikuwa benki ya kwanza Kusini mwa Jangwa la Sahara Afrika kutunukiwa cheti hicho.
Akizungumza wakati wa kupokea cheti hicho leo Jumanne, Julai mosi, 2025, Kaimu Ofisa Mtendaji Mkuu wa NMB, Filbert Mponzi amesema cheti hicho kinachoitangaza taasisi yake kimataifa ni cha kujivunia na kwamba usawa wa kijinsia kwa benki yake hauishii katika utendaji kazi wa ndani tu, bali pia katika bunifu za masuluhisho yao kwa wateja.
“Cheti cha EDGE Certified Foundation kinaakisi na kuthibitisha uwepo wa jitihada kubwa za kuzingatia usawa wa kijinsi mahali pa kazi.
“Kwetu NMB, usawa wa kijinsia hatuuangalii tu katika utendaji kazi ndani ya taasisi yetu, bali pia katika aina ya bunifu za masuluhisho yetu yanayozingatia mpango mkakati, uthibitisho ukiwa ni pamoja na Hatifungani ya Jasiri tuliyoingiza sokoni na kuuza kwa zaidi ya Sh70 bilioni , ambazo zilielekezwa katika mikopo ya riba nafuu kwenye biashara zinazoongozwa ama kugusa maisha ya wanawake, ambako mikopo zaidi ya 3,200 ilitolewa.
“Kwa ujumla, katika miaka michache tumeendelea kuongeza uwiano miongoni mwa wafanyakazi, kufikia Desemba 31, 2024, NMB ilikuwa na jumla ya waajiriwa 5,204 kutoka waajiriwa 3,544 tuliokuwa nao Desemba, 2022.
“Mgawanyo wa kijinsia miongoni mwa wafanyakazi wetu kwa sasa ni waajiriwa wanaume ni 2,564 sawa na asilimia 49.26 na waajiriwa wanawake wapo 2,640 sawa na asilimia 50.74,” alibainisha Mponzi katika hotuba yake wakati wa hafla hiyo na kuongeza:
“Utafiti unaonesha kuwa taasisi zenye usawa wa kijinsia, ndizo zinazopata mafanikio makubwa zaidi, NMB chini ya Ofisa Mtendaji Mkuu, Ruth Zaipuna ni uthibitisho na kielelezo cha hilo, mafanikio ya benki ni makubwa pale idadi ya wafanyakazi inapoelekea kulingana,” amesema Mponzi.
Akikabidhi cheti hicho, Meneja wa Shirika la Fedha la Kimataifa (IFC) Kanda ya Afrika Mashariki, Samuel Ng’ang’a, ameipongeza NMB kwa kuendelea kuamini katika usawa wa kijinsia na mgawanyo huo una faida nyingi kibiashara na kiuchumi kwa ukuaji wa taasisi kitaifa na kimataifa.
Akiunga mkono kauli ya Mponzi, Ng’ang’a alibainisha kuwa usawa wa kijinsia mahali pa kazi unachochea ubunifu, ukuaji wa kiuchumi na utulivu wa kifedha, na kwamba kinachofanywa na NMB katika hilo ni alama ya kudumu na mbegu bora ya mafanikio kwa taasisi.
Kwa upande wake, Ofisa Mkuu wa Rasirimali Watu wa Benki ya NMB, Emmanuiel Akonaay, ameishukuru EDGE Certisified Foundation kwa cheti hicho.
Akonaay amesisitiza kuwa wataendelea kushirikiana na wadau mbalimbali, ikiwa ni pamoja na wateja wao katika kufikia malengo ya jamii ya usawa kijinsia katika kila nyanja, huku akiwashukuru wafanyakazi, wateja pamoja na wadau wa NMB kwa kuwa sehemu ya utambuzi huo.