RC Mbeya atoa maagizo utoroshaji madini

Wachimbaji wa madini ya dhahabu mkoa wa kimadini Chunya wakiwa kwenye mkutano mkuu uliowakutanisha taasisi mbalimbali za Serikali ili kuwasilisha kero zao. Picha na Mary Mwaisenye Chunya.

Chunya. Mkuu wa Mkoa wa Mbeya (RC), Juma Homera amekemea tabia ya wachimbaji wa madini ya dhahabu mkoa wa Mbeya kutorosha na kuuza madini yao nje ya nchi, akidai hali hiyo inapoteza mapato ya Serikali.

Homera ametoa kauli hiyo leo Jumanne, Novemba 22, 2022 katika mkutano mkuu wa wachimbaji wa madini uliofanyika katika mkoa wa  kimadini Chunya ambapo amesisitza wachimbaji wawe wanauza madini yao kwenye masoko yaliyoanishwa.

Amesema Serikali inatambua changamoto za wachimbaji wa madini wanazokutanazo katika utendaji wao wa kazi hivyo watahakikisha changamoto hizo ambazo ni za kisera wanazifikisha mahali husika ili ziweze kufanyiwa kazi.

Awali, akiwasilisha risala kwa mkuu wa mkoa wa Mbeya Mwenyekiti wa chama Cha wachimbaji madini mkoa wa Mbeya Leonard Manyesha amesema wachimbaji wanakabiliwa na utitiri wa Kodi kutoka kwenye taasisi mbalimbali za Serikali ambazo TRA, OSHA, Zimamoto, TFS pamoja na Halmshauri.

Ambapo ameomba Serikali kuangalia namna bora ya ukusanyaji wa kodi kwa wachimbaji wa madini ya dhahabu ili kumpunguzia mchimbaji utitiri wa Kodi.

Kwa upande wake, Mbunge wa Lupa, Masache Kasaka akizungumzia utitiri wa kodi amesema hilo linawaumiza wachimbaji kwani kama mkoa wa kimadini ambao unazalisha madini kwa wingi na kufanikiwa kushika nafasi ya pili kitaifa kwa uzalishaji wa madini wanapaswa kutengenezewa mazingira ambayo ni rafiki kwao.

Ambapo amefafanua yeye kama mwakilishi wa wananchi na muwakilishi wao bungeni atahakikisha yale yote yanayowahusu Sheria atawasemea bungeni ili kuhakikisha yale yanayohusu marekebisho ya  Sheria yanafanyiwa kazi na wao kufanya kazi kwa Uhuru.

Akijibu risala ya wachimbaji mkuu wa mkoa wa Mbeya amesema pamoja na malalamiko ya wachimbaji, Homera amesisitiza kuwa hakuna nchi inayoendeshwa bila kodi hivyo wachimbaji wahakikishe wanalipa Kodi zilizo halali kwa maendeleo yao wenyewe.

Aidha, mkuu huyo wa mkoa amemwagiza mkuu wa Wilaya ya Chunya (DC), Mayeka Mayeka kuunda kamati maalumu ambayo itasaidia kuunganisha taasisi zilizolalamikiwa ili ziangalie changamoto zote zinazowakabili wachimbaji wa madini mkoa wa kimadini Chunya ili uzalishaji wa madini uweze kuwa na tija kwa wananchi.