Ripoti yaainisha maeneo muhimu kuinua wachimbaji wadogo
Wachimbaji wadogo wa madini ya dhahabu katika Kijiji cha Itumbi Wilayani chunya Mkoani Mbeya wakiendelea na zoezi la uchenjuaji wa madini hayo. Picha naMaktaba
Muktasari:
- Ripoti hiyo, iliyozinduliwa leo Juni 13, 2026 inapendekeza hatua za mageuzi zinazolenga kuwawezesha wachimbaji, kuongeza uzalishaji, kuharakisha urasimishaji wa shughuli zao na kuongeza mchango wa sekta hiyo katika ukuaji wa uchumi wa taifa.
Dar es Salaam. Wachimbaji wadogo wa madini nchini wanaweza kunufaika na upatikanaji mkubwa wa mitaji, taarifa za kijiolojia, teknolojia za kisasa na masoko ya uhakika iwapo mapendekezo yaliyomo katika ripoti mpya iliyoagizwa na Serikali yatatekelezwa.
Ripoti hiyo, iliyozinduliwa leo Juni 13, 2026 inapendekeza hatua za mageuzi zinazolenga kuwawezesha wachimbaji, kuongeza uzalishaji, kuharakisha urasimishaji wa shughuli zao na kuongeza mchango wa sekta hiyo katika ukuaji wa uchumi wa taifa.
Mwenyekiti wa kamati iliyoandaa mapendekezo hayo, Victor Tesha amesema mapendekezo hayo yanalenga kutatua changamoto za muda mrefu zinazowakabili wachimbaji wadogo wa madini ikiwemo mitaji.
“Mapendekezo yetu yanalenga kuwawezesha wachimbaji wadogo kuongeza uzalishaji, kuimarisha urasimishaji wa shughuli za uchimbaji na kuongeza mchango wa sekta ya madini katika ukuaji wa uchumi wa nchi,” amesema Tesha.
Miongoni mwa mapendekezo muhimu yaliyotolewa ni kuanzishwa kwa benki maalumu ya wachimbaji pamoja na kuboresha upatikanaji wa mikopo nafuu, taarifa za kijiolojia, teknolojia za kisasa za uchimbaji, viwango vya usalama kazini na masoko ya uhakika ya madini.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, wachimbaji wadogo wanachangia takribani asilimia 40 ya mapato ya sekta ya madini nchini lakini bado wanakabiliwa na vikwazo vikubwa vinavyozuia ukuaji na kuongeza uzalishaji.
Changamoto hizo ni pamoja na ukosefu wa mitaji kutoka taasisi rasmi za fedha, upatikanaji hafifu wa taarifa za kijiolojia, matumizi ya vifaa vya kizamani, udhaifu wa mifumo ya usaidizi wa taasisi, pamoja na hatari za mazingira na usalama.
Ripoti hiyo inaonyesha kuwa takribani asilimia 72 ya wachimbaji wadogo bado wanatumia mbinu za jadi katika uchimbaji na uchenjuaji wa madini hali inayosababisha uzalishaji mdogo, gharama kubwa za uendeshaji, ufanisi mdogo na kuongezeka kwa hatari kwa wachimbaji na mazingira.
Ripoti hiyo inaeleza kuwa hadi Mei 2025, Tanzania ilikuwa imetoa leseni nyingi za uchimbaji mdogo, jambo linaloonyesha kuongezeka kwa ushiriki wa Watanzania katika sekta hiyo.
“Hata hivyo, umiliki wa leseni pekee hautoshi kwa kuwa wachimbaji wengi bado hawana mtaji, ujuzi wa kiufundi, vifaa na masoko yanayohitajika kuendesha shughuli endelevu za uchimbaji,” amesema.
Ili kukabiliana na changamoto hizo, timu ya wataalamu iliyoteuliwa na Waziri wa Madini imependekeza kuanzishwa kwa Mfuko wa Maendeleo ya Uchimbaji Madini Tanzania (Tanzania Mining Development Fund) wenye mtaji wa awali wa dola za Marekani milioni 100 (Sh2.6 bilioni) kutoka serikalini.
“Mfuko huu utasaidia upatikanaji wa fedha, kugharamia tafiti za kijiolojia, kupunguza hatari za uwekezaji na kusaidia wachimbaji kuandaa miradi yenye mvuto kwa wawekezaji na taasisi za fedha,” amesema.
Ripoti hiyo inakadiria kuwa takribani dola milioni 97 (Sh2.54 bilioni) zitahitajika kusaidia miradi 20 ya uchimbaji iliyo katika hatua za juu za maendeleo.
Mapendekezo mengine ni pamoja na kuimarisha mfumo wa usajili wa wachimbaji, kupanua huduma za taarifa za kijiolojia, kuongeza upatikanaji wa teknolojia za kisasa za uchimbaji, kuwaainisha wachimbaji kulingana na uwezo wao wa uwekezaji na kuimarisha uratibu kati ya taasisi zinazohudumia sekta hiyo.
Amesema kuimarishwa kwa msaada kwa wachimbaji wadogo kutachochea uzalishaji wa madini, kuongeza ajira, kukuza mapato ya Serikali na kuongeza ushiriki wa Watanzania katika mnyororo mzima wa thamani wa sekta ya madini.
“Mapendekezo tunayowasilisha leo yanaashiria mwanzo wa awamu mpya ya maendeleo ya uchimbaji mdogo wa madini nchini. Kwa kuweka mifumo sahihi ya usaidizi, rasilimali kubwa za madini zilizopo Tanzania zinaweza kuchangia zaidi katika maendeleo ya taifa,” amesema Tesha.
Akizungumza katika hafla hiyo, Waziri wa Madini, Antony Mavunde amesema Serikali inaendelea kuimarisha juhudi za kuibadilisha sekta ya madini kwa kuweka mkazo zaidi katika kuwawezesha wachimbaji wadogo ambao kwa sasa wanachangia takribani asilimia 40 ya uzalishaji wa madini nchini.
Amesema mageuzi yaliyofanyika tangu mwaka 2017 yameimarisha usimamizi wa biashara ya madini na kuongeza makusanyo ya mapato kupitia kuanzishwa kwa masoko na vituo rasmi vya ununuzi wa madini nchini kote.
“Sekta ya madini imepitia mabadiliko makubwa katika miaka ya karibuni, ambapo mapato yameongezeka kwa kiwango kikubwa na manufaa mengi zaidi kubaki nchini,” amesema.
Amesema sehemu ya mafanikio hayo imetokana na mchango unaoongezeka wa wachimbaji wadogo huku akitaja hatua mbalimbali zinazolenga kuharakisha maendeleo ya sekta hiyo.
Miongoni mwa hatua hizo ni kuanzishwa kwa taasisi itakayotoa dhamana ya hadi asilimia 50 ya mikopo inayotolewa kwa wachimbaji, hatua inayotarajiwa kurahisisha upatikanaji wa fedha kutoka benki za biashara.
“Tunataka wachimbaji wetu wapate mtaji kwa urahisi zaidi bila kutegemea kwa kiasi kikubwa wafadhili au wawekezaji wa nje. Kupitia mageuzi haya, tunafungua fursa zaidi kwa Watanzania kushiriki kikamilifu katika uchimbaji na biashara ya madini,” amesema.
Amesema Serikali pia inaendelea kuimarisha mifumo ya biashara ya dhahabu ndani ya nchi na kuongeza upatikanaji wa vyanzo vya fedha vya ndani ili kuwawezesha wachimbaji kuuza dhahabu yao kupitia masoko ya ndani huku ikiiimarisha Tanzania katika soko la kimataifa la dhahabu.
Mavunde alieleza imani yake kuwa utekelezaji wa mapendekezo ya ripoti hiyo utafungua uwezo mkubwa uliopo katika uchimbaji mdogo wa madini na kuongeza mchango wa sekta hiyo katika ukuaji wa uchumi na maendeleo ya viwanda.
Kwa upande wake, Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wachimbaji Tanzania (Femata), John Bina amesema ili kufikia matokeo yanayotarajiwa ni lazima wachimbaji wadogo wawezeshwe ili waweze kushindana na wawekezaji wakubwa na kampuni zenye nguvu kubwa za kifedha.
“Hakuna namna ya kupata madini bila kuwekeza mtaji. Uchimbaji wa madini unahitaji teknolojia na uwekezaji mkubwa si jambo la kufanyika kwa mazoea. Ni muhimu sekta ya benki ikawa sehemu ya suluhisho kwa kuwawezesha wachimbaji kupata mitaji,” amesema.
Bina amesema Femata ipo katika mkakati wa kuanzisha Benki ya Wachimbaji Tanzania na kuiomba Serikali kuunga mkono mpango huo kwa kuwa unaweza kuleta manufaa makubwa kwa sekta hiyo.
“Kwa mfano, leo hii Benki Kuu ya Tanzania inanunua dhahabu, jambo ambalo limeongeza uhakika wa soko la madini hayo nchini. Kama isingekuwa hivyo, bei za dhahabu nchini zingeweza kubaki chini hata wakati bei katika soko la dunia zimepanda. Uwepo wa Benki Kuu umesaidia kuleta utulivu na kudhibiti soko,” amesema.