Sare, vifaa vya hamasa vya Chadema dili Mwanza

Wafanyabiashara wakichangamkia biashara ya sare na vifaa vya hamasa vya Chadema viwanja vya Furahisha jijini Mwanza. Picha Doreen Parkshard.

Muktasari:

  • Hamasa ya kununua na kuvaa sare na vifaa vingine vya hamasa vya Chadema ni kati ya mambo yanayoendelea katika viwanja vya Furahisha jijini Mwanza ambako mkutano wa hadhara wa chama hicho unafanyika leo.

Mwanza. Biashara wa sare na vifaa vya uhamasishaji vya Chadema ni miongoni mwa fursa inayoambatana na uwepo wa mkutano wa hadhara wa chama hicho unaofanyika katika viwanja vya Furahisha jijini Mwanza leo.

Wafanyabiashara wa sare na vifaa hivyo tayari wametandaza bidhaa zao katika eneo lote la viwanja hivyo vilivyoko jirani na eneo la kibiashara la Rock City Mall.

Yoramu Sethy, mmoja wa makada wa Chadema na mfanyabiashara wa sare na vifaa vya hamasa vya chama hicho kikuu cha upinzani nchini ameiambia Mwananchi kuwa biashara imenoga tangu alipowasili jijini Mwanza juzi ambapo kwa siku anauza zaidi ya sare 100 na vifaa vingine vya hamasa.

"Tunamshukuru Mungu kwa mikutano ya hadhara kuruhusiwa kwa sababu tumepata fursa ya biashara ya sare na vifaa vingine vya hamasa vya Chadema. Leo tuko hapa Mwanza na kesho tunaelekea Musoma na baadaye maeneo mengine kulingana na ratiba itakayotangazwa na chama," amesema Yoram.

Amesema biashara ya sare na vifaa vya hamasa iliyumba wakati mikutano ilipozuiwa kiasi cha baadhi yao kujikuta wana mzigo waliouagizia tangu mwaka 2015.

"Sehemu ya huu mzigo mwingine wangu ni wa tangu mwaka 2015 na bado unauzika. Tunatarajia biashara itakuwa nzuri zaidi kuanzia sasa baada ya mikutano kurejea," amesema Yoram.

Mfanyabiashara mwingine, Paulina Augustine, mkazi wa Mwanza naye ameonyesha imani kuwa kipato chake kitaimarika kutokana na kurejea kwa mikutano ya hadhara.

"Biashara ilidorora miaka saba iliyopita kwa sababu baadhi ya wana Chadema walihofia kuvaa sare kutokana na hali ya kisiasa iliyokuwepo. Hofu hiyo sasa imeondoka na tunaamini tutauza sare na vifaa vingine vya hamasa vya Chadema," amesema Paulina