Tani 12,000 za korosho kusafirishwa bandari ya Mtwara

Muktasari:

Zaidi ya tani 12,000 za korosho ghafi zinatarajiwa kusafirishwa kupitia bandari ya Mtwara katika msimu huu wa mwaka 2022/23.

Mtwara. Zaidi ya tani 12,000 za korosho ghafi zinatarajiwa kusafirishwa kupitia bandari ya Mtwara katika msimu huu wa mwaka 2022/23 na tayari meli aina ya MV Lil Shama ya kampuni ya Hydro & Marine imeshatia nanga t kwakupokea shehena ya mzigo huo.

Akizungumza bandarini hapo leo Novemba 5, Kaimu Meneja wa Bandari ya Mtwara, Teddy Kololo amesema kuwa meli hiyo imefika tayari kwa ajili ya kusafirisha korosho na itakuwepo kwaajli ya kupakia mzigo huo.

 “Hii Meli itatumika katika usafirishaji wa korosho kwa msimu huu wa 2022/2023 na pia kampuni hiyo imeahidi kuwaletea meli nyingine itakayotumika katika usafirishaji wa bidhaa nyingine kupitia Badari yetu," amesema Kalolo.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Kanal Ahmed Abbas amesema kuwa ujio wa meli hiyo ni fursa kwa wafanyabishara kuanza kutumia bandari hiyo kwakusafirisha bihdaa mbalimbali hususani korosho, makaa ya mawe na saruji.

“Nimefarijika kuona uhitaji wa wafanyabiashara wa kuleta meli ni mkubwa, hivyo nawataka wadau na watumiaji wa bandari kuchangamkia fursa hii kwa kukusanya na kuwa na mzigo ya uhakika ambayo meli zikifika zikae kwa muda mfupi na kuondoka,” amesema.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Hydro Marine,   Ignasi Millanzi amewataka wafanyabiashara kushirikiana katika huduma ya meli kwani wao kama kampuni ya usafirishaji wa Baharini wapo tayari kutumia bandari hiyo.

Akizungumzia fursa hiyo, Mwenyekiti wa wafanyabiashara wa Mkoa wa Mtwara, Kizito Galinoma amesema kuwa kilikuwa kilio cha muda mrefu kwao kwa wafanya biashara wa Mtwara kupata meli ya kusafirisha bidhaa mbalimbali.