Tanzania, Burundi kutumia madini kukuza uchumi

Tuesday February 16 2021
madini pic

Serikali ya Tanzania na Burundi wakutana katika kikao cha siku mbili kujadili namna nchi hizo mbili zitakavyoweza kushirikiana kutumia fursa ya madini kukuza uchumi baina ya nchi hizo mbili.

By Happiness Tesha

Kigoma. Serikali ya Tanzania na Burundi zimejadiliana namna zitakavyoweza kushirikiana kutumia fursa ya madini kukuza uchumi.

Kikao hicho kimefanyika leo Jumanne Februari 16, 2021 mjini Kigoma kati ya Balozi wa Tanzania nchini Burundi,  Jilly Maleko na  Balozi mdogo wa Burundi nchini Tanzania, Kabura Cyriaque na wataalamu wa madini kutoka nchi zote mbili.

Akizungumza katika kikao hicho Balozi Maleko amesema wanatarajia kuja na makubaliano yatakayotumika kwenye ushirikiano wa biashara ya madini.

Amebainisha kuwa kikao hicho ni maandalizi ya mkutano mkubwa wa ushirikiano wa tume ya pamoja kati ya Tanzania na Burundi unaotarajia kufanyika Machi 3 hadi 4, 2021 ikiw ani utekelezaji wa  marais wa nchi hizo mbili waliokutana Septemba 2020.

"Tanzania ina madini mengi ambayo nchi ya Burundi haina na pia kuna baadhi ya madini Tanzania haina, kwa ushirikiano huo tutaweza kunufaika na fursa ya madini hayo yanayopatika katika nchi hizo," amesema Maleko.

Akifungua  kikao hicho kwa niaba ya Mkuu wa mkoa wa Kigoma, Thobias Andengenye, katibu tawala msaidizi mipango na uratibu, Samweli Tenga amesema kuna chokaa na chumvi na kwamba kutaibua fursa za biashara.

Advertisement

Kamishna wa madini Wizara ya Madini,  David Malabwa amesema kutokana na uwepo wa changamoto ya tozo na kodi katika usafirishaji wa madini baina ya nchi hizo mbili, katika kikao hicho watajadili masuala hayo kwa kina na kutoka na makubaliano.

Naye Cyriaque amesema anaamini katika kikao hicho watakayojadili, watatoka na maazimio ambayo yatakuwa na manufaa kwa wananchi wa nchi hizo mbili.


Advertisement