Prime
Tanzania inaweza kudhibiti hivi utegemezi wa fedha za kigeni
Muktasari:
- Kwa mujibu wa Kanuni za Matumizi ya Fedha za Kigeni za mwaka 2025, bidhaa na huduma zote zinazotolewa nchini zinapaswa kuuzwa na kulipiwa kwa shilingi ya Tanzania.
Dar es Salaam. Wataalamu wa uchumi wamesema hatua za mara kwa mara za Serikali kupiga marufuku matumizi ya fedha za kigeni kwa malipo ya bidhaa na huduma ndani ya nchi hazitakuwa na matokeo ya kudumu endapo Benki Kuu ya Tanzania (BoT) haitaimarisha thamani ya shilingi na kuhakikisha sheria zilizopo zinatekelezwa kikamilifu.
Wamesema pamoja na kuwapo kwa Kanuni za Matumizi ya Fedha za Kigeni za mwaka 2025, bado baadhi ya wafanyabiashara wanaendelea kunukuu bei na kufanya malipo kwa dola kutokana na udhaifu wa usimamizi wa sheria na kuyumba kwa thamani ya shilingi.
Maoni hayo yametolewa siku moja baada ya Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba, kupiga marufuku matumizi ya sarafu za kigeni katika malipo ya bidhaa na huduma ndani ya nchi, akisema tabia hiyo ni miongoni mwa njia zinazoweza kuchochea utakatishaji fedha.
Dk Mwigulu alifikia hatua hiyo wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Suma Fyandoma ambaye alihoji kauli ya Serikali kuhusu baadhi ya wafanyabiashara wenye hoteli, wauzaji wa viwanja na wanaopingisha nyumba ambao wanaendelea kutoza gharama kwa kutumia Dola.
Waziri Mkuu akijibu swali hilo, amesema tabia ya kutoza kwa sarafu za kigeni ni "ulimbukeni wa kujificha kwenye ukoloni" usioendana na wakati, huku akisisitiza kuwa katazo hilo halihusu shughuli za biashara ya kimataifa, ikiwemo mauzo na manunuzi ya nje pamoja na zabuni kubwa za kimataifa.
Hata hivyo, si mara ya kwanza Serikali kutoa msimamo huo. Mei 2025, Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Emmanuel Tutuba, alitangaza ni kosa kisheria kunukuu bei, kutangaza au kufanya malipo kwa fedha za kigeni kwa bidhaa na huduma zinazotolewa ndani ya Tanzania.
Katika taarifa hiyo, BoT ilieleza kuwa miamala ya kimataifa pekee ndiyo inayoruhusiwa kufanyika kwa fedha za kigeni, huku watalii wakitakiwa kubadilisha fedha kupitia benki au maduka ya kubadilisha fedha yaliyosajiliwa au kutumia kadi za benki.
Akizungumza na Mwananchi, Profesa wa Uchumi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Abel Kinyondo, amesema tatizo kubwa si ukosefu wa sheria bali utekelezaji wake.
"Watu wanapoona udhibiti ni hafifu wataendelea kufanya jambo hilo hata kama wanajua wanavunja sheria. Swali ni ukimkuta mtu ametumia dola kinyume cha sheria, hatua gani zinachukuliwa? Kama hakuna uwajibikaji, makatazo yataendelea kutolewa lakini tabia haitabadilika," amesema.
Profesa Kinyondo amesema Serikali pia inapaswa kuwa mfano katika utekelezaji wa sheria hizo, akieleza kuwa baadhi ya taasisi za umma bado zinatangaza ada au gharama kwa kutumia dola.
Ametoa mfano wa sekta ya utalii, ambapo baadhi ya huduma bado hunukuliwa kwa fedha za kigeni, hali inayotuma ujumbe unaokinzana na sera ya matumizi ya shilingi.
"Sekta za Serikali zikifanya jambo lililopigwa marufuku, inakuwa vigumu kuwashawishi wafanyabiashara binafsi kuacha kufanya hivyo," amesema.
Mbali na usimamizi wa sheria, Profesa Kinyondo amesema suluhu ya muda mrefu ni BoT kuhakikisha shilingi ya Tanzania inabaki kuwa sarafu yenye utulivu.
"Wafanyabiashara wengi wanakimbilia dola kwa sababu thamani yake haitetereki kwa haraka. Akitaja huduma kwa dola anajihakikishia kuwa hata kiwango cha ubadilishaji kikibadilika hatapata hasara. Ndiyo maana BoT inapaswa kuendelea kulinda uthabiti wa shilingi," amesema.
Kwa upande wake, mchambuzi wa masuala ya uchumi, Oscar Mkude, amesema matumizi ya dola katika miamala ya ndani yanaathiri uwezo wa Benki Kuu kusimamia sera za fedha.
"Dola inapokuwa sehemu ya miamala ya ndani, BoT inapunguza uwezo wake wa kudhibiti mfumuko wa bei kwa sababu sehemu ya uchumi inaanza kutegemea sarafu ambayo haiidhibiti," amesema.
Mkude amesema pamoja na kusimamia sheria, Serikali inapaswa kuongeza elimu kwa wafanyabiashara na wananchi kuhusu umuhimu wa kutumia shilingi katika miamala ya ndani.
Naye mchambuzi wa uchumi, Magabilo Masambu, amesema BoT inapaswa kuendelea kusimamia sera za fedha zitakazodhibiti mfumuko wa bei na kupunguza kuyumba kwa thamani ya shilingi dhidi ya sarafu za kimataifa.
"Kadiri shilingi inavyokuwa imara na kutabirika, ndivyo wafanyabiashara watakavyopunguza matumizi ya dola katika kupanga bei za bidhaa na huduma," amesema.
Masambu amesema Serikali pia inapaswa kuhakikisha Kanuni za Matumizi ya Fedha za Kigeni za mwaka 2025 zinatekelezwa kwa usawa katika sekta zote bila ubaguzi.
Amesema baadhi ya taasisi za umma na sekta kama utalii bado zinanukuu gharama kwa dola, jambo linalopunguza ufanisi wa utekelezaji wa sheria.
Aidha, ameshauri BoT na mamlaka nyingine kuongeza ukaguzi wa biashara zinazokiuka kanuni hizo na kuhakikisha adhabu zilizowekwa zinatekelezwa kwa uwazi.
Kanuni zinasemaje?
Kwa mujibu wa Kanuni za Matumizi ya Fedha za Kigeni nchini Tanzania za mwaka 2025, bidhaa na huduma zote zinazotolewa nchini zinapaswa kuuzwa na kulipiwa kwa shilingi ya Tanzania.
Kanuni hizo zinakataza kupanga bei, kutangaza, kunukuu au kulazimisha malipo kwa fedha za kigeni, pamoja na kukataa kupokea shilingi kama njia halali ya malipo ndani ya nchi.
Hata hivyo, kanuni hiyo inatoa ruhusa kwa baadhi ya miamala maalumu kufanyika kwa fedha za kigeni, ikiwemo michango ya Serikali kwa taasisi za kikanda, miamala ya balozi na mashirika ya kimataifa, mikopo ya fedha za kigeni inayotolewa na benki za biashara na taasisi za fedha, pamoja na malipo ya bidhaa katika maduka yasiyotoza ushuru.