Tanzania yafungua rasmi soko la ndizi Afrika Kusini
Muktasari:
- Hatua hiyo inatarajiwa kuongeza mauzo ya mazao ya kilimo nje ya nchi, kupanua fursa za biashara kwa wakulima na wafanyabiashara, pamoja na kuimarisha mchango wa sekta ya kilimo katika ukuaji wa uchumi wa taifa.
Arusha. Tanzania imefungua rasmi soko la ndizi mbichi nchini Afrika Kusini baada ya kukamilika kwa majadiliano ya kitaalamu kuhusu matakwa ya afya ya mimea kati ya mamlaka husika za nchi hizo mbili.
Hatua hiyo imefikiwa kupitia mazungumzo kati ya Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA) na Mamlaka ya Afya ya Mimea ya Afrika Kusini (NAPOZA), yaliyolenga kuridhiana kuhusu masharti ya afya ya mimea yanayoruhusu ndizi kutoka Tanzania kuingia katika soko la nchi hiyo.
Aidha, mauzo ya nje ya mazao ya kilimo ya Tanzania kwa sasa yanakadiriwa kufikia thamani ya takribani dola za Marekani bilioni 3.54 (sawa na zaidi ya shilingi trilioni 9.3 za Tanzania) kwa mwaka.
Kwa upande wa ndizi pekee, mauzo yake ya nje yanakadiriwa kuwa na thamani ya takribani dola za Marekani milioni 3.67 (zaidi ya shilingi bilioni 9.6 za Tanzania) kwa mwaka, yakipelekwa katika masoko mbalimbali yakiwemo Zambia, Malawi, Uganda na nchi za Umoja wa Ulaya (EU).
Mkurugenzi Mkuu wa TPHPA, Profesa Joseph Ndunguru, akizungumza na waandishi wa habari kuhusu ufunguzi wa soko la ndizi nchini Afrika Kusini.
Ufunguzi wa soko hilo unatarajiwa kuongeza mauzo ya mazao ya kilimo nje ya nchi, kupanua fursa za biashara kwa wakulima na wafanyabiashara wa Tanzania, pamoja na kuchangia ukuaji wa uchumi wa taifa.
Akizungumza na waandishi wa habari, Mkurugenzi Mkuu wa TPHPA, Profesa Joseph Ndunguru, amesema hatua hiyo ni sehemu ya jitihada za Serikali za kutafuta masoko mapya ya mazao ya kilimo, kuongeza mapato ya wakulima na kuimarisha mchango wa sekta ya kilimo katika maendeleo ya uchumi.
Amesema mafanikio hayo yanaendana na utekelezaji wa Ajenda ya Kilimo ya mwaka 2030 inayolenga kukuza sekta ya kilimo kwa asilimia 10 na kuongeza thamani ya mauzo ya mazao ya kilimo nje ya nchi.
"Hatua hii pia inaunga mkono azma ya kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha uzalishaji wa chakula na mazao ya biashara kwa ajili ya soko la ndani na la kimataifa," amesema Profesa Ndunguru.
Amesema soko la Afrika Kusini linafungua fursa mpya kwa wazalishaji wa ndizi nchini kuingia katika moja ya masoko makubwa barani Afrika na kuimarisha nafasi ya Tanzania katika biashara ya kikanda na kimataifa ya mazao ya kilimo.
"Kwa sasa tunakamilisha utaratibu wa kuwaelimisha na kuwaandaa wadau kuhusu masharti, viwango na taratibu zinazotakiwa ili kuwezesha usafirishaji wa ndizi kwenda Afrika Kusini haraka iwezekanavyo," amesema.
Kwa mujibu wa Profesa Ndunguru, maandalizi hayo yanajumuisha maelekezo kuhusu mahitaji ya afya ya mimea, viwango vya ubora, ukaguzi wa mazao, uthibitishaji na masharti mengine yanayotakiwa na mamlaka za Afrika Kusini.
Amesema mbali na kufunguliwa kwa soko la ndizi, TPHPA pia imesajili makampuni 15 yanayojihusisha na uzalishaji, ufungashaji na usafirishaji wa parachichi kwa ajili ya kuuza zao hilo nchini Afrika Kusini.
"Hii ni baada ya kutimiza matakwa yote ya afya ya mimea na viwango vya biashara vinavyohitajika."
Naye Mkurugenzi wa Idara ya Usalama wa Afya ya Mimea wa TPHPA, Dk Ben Ngowi, amesema upatikanaji wa soko hilo utaongeza thamani ya zao la ndizi, kuhamasisha uwekezaji katika uzalishaji na usindikaji, pamoja na kuongeza ajira katika mnyororo mzima wa thamani wa zao hilo.
Amesema kufunguliwa kwa soko hilo kumechangiwa kwa kiasi kikubwa na kuimarika kwa mifumo ya afya ya mimea nchini, ikiwemo udhibiti wa visumbufu vya mimea, ufuatiliaji wa mazao kutoka shambani hadi sokoni, ukaguzi wa mashamba na vituo vya kufungashia mazao, pamoja na utoaji wa vyeti vya afya ya mimea vinavyotambulika kimataifa.
Dk Ngowi aliwataka wakulima, wasafirishaji na wadau wengine wa sekta ya kilimo kuendelea kuzingatia viwango vya kimataifa vya afya ya mimea ili kuongeza ushindani wa mazao ya Tanzania katika masoko ya kikanda na dunia.
Aidha, amesema TPHPA inaendelea kutoa elimu kwa wakulima kuhusu kilimo salama cha ndizi na mbinu za kudhibiti magonjwa yanayoliathiri zao hilo, ikiwemo ugonjwa wa mnyauko, ili kuhakikisha uzalishaji unaendana na mahitaji ya soko jipya la Afrika Kusini.