Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Tanzania yajipanga kuwa kinara wa graphite duniani

Muktasari:

  • Tanzania kwa sasa ina kampuni 30 zinazomiliki leseni za kati na kubwa za uchimbaji wa madini kinywe, jambo linalotarajiwa kuongeza ushindani wa uzalishaji wa madini hayo duniani, huku China ikiendelea kuongoza kwa kuzalisha tani milioni 1.2 kwa mwaka

Dar es Salaam. Serikali imesema Tanzania inajiandaa kuwa miongoni mwa wazalishaji wakubwa wa madini ya kinywe duniani yanayotumika katika utengenezaji wa betri za magari ya umeme.

Waziri wa Madini, Anthony Mavunde amesema Tanzania kwa sasa ina kampuni 30 zinazomiliki leseni za kati na kubwa za uchimbaji wa madini kinywe, jambo linalotarajiwa kuongeza ushindani wa uzalishaji wa madini hayo duniani, huku China ikiendelea kuongoza kwa kuzalisha tani milioni 1.2 kwa mwaka.

Mavunde amesema hayo leo Mei 28, 2026 wilayani Ruangwa mkoani Lindi katika hafla ya utiaji saini wa mikataba ya ubia kati ya Serikali na Kampuni ya Lindi Jumbo Limited kwa ajili ya mradi mkubwa wa uchimbaji wa graphite.

Hafla ya utiaji saini wa mikataba ya ubia kati ya Serikali na Kampuni ya Lindi Jumbo Limited kwa ajili ya mradi mkubwa wa uchimbaji wa graphite.

Amesema kuanza kwa uzalishaji mkubwa wa madini hayo kunaiweka Tanzania katika ramani ya dunia kama nchi yenye nafasi ya kimkakati katika uzalishaji wa madini muhimu kwa teknolojia za nishati safi.

“Madini ya kinywe ndiyo msingi wa teknolojia ya kesho kutokana na umuhimu wake katika utengenezaji wa betri za magari ya umeme. Tanzania sasa ina nafasi kubwa ya kuwa miongoni mwa wazalishaji muhimu duniani,” amesema.

Amesema kwa sasa Tanzania ipo katika nafasi ya sita duniani kwa uzalishaji wa graphite, ikiwa na uzalishaji wa tani 25,000 kwa mwaka kupitia kampuni mbili za Lindi Jumbo na God Mwanga-Tanga ambazo tayari zimeanza uzalishaji mkubwa.

Pia kampuni nyingine 28 zipo katika hatua mbalimbali za maandalizi ya kuanza uzalishaji, huku Serikali ikizitaka kuharakisha utekelezaji wa miradi yao kwa mujibu wa masharti ya leseni.

“Wenye leseni wanapaswa kuhakikisha wanaanza uzalishaji kwa wakati kama sheria inavyoelekeza ili kuepuka hatua za kufutiwa leseni,” amesema.

Wananchi wa Lindi wakiwa katika hafla ya utiaji saini wa mikataba ya ubia kati ya Serikali na Kampuni ya Lindi Jumbo Limited kwa ajili ya mradi mkubwa wa uchimbaji wa graphite.

Mavunde amesema mafanikio hayo yanatokana na mazingira mazuri ya uwekezaji yaliyowekwa na Serikali.

“Rais ameendelea kuifanya Tanzania kuwa Taifa lenye dira wazi ya kiuchumi, mazingira rafiki ya uwekezaji na usimamizi mzuri wa rasilimali zake,” amesema.

Ameyasema hayo wakati ambao mradi wa Lindi Jumbo wenye thamani ya zaidi ya dola za Marekani milioni 82 unatarajiwa kuzalisha tani 40,000 za kinywe kwa mwaka kwa kipindi cha miaka 24 ya uhai wa mgodi huo.

Amesema tayari zaidi ya ajira 300 zimezalishwa kupitia mradi huo huku ukitarajiwa kuongeza mapato ya Serikali pamoja na kuchochea shughuli za kiuchumi mkoani Lindi.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Timu ya Majadiliano ya Serikali katika Sekta ya Madini, Profesa Sifuni Mchome amesema kupitia makubaliano hayo Serikali itanufaika kupitia mapato, udhibiti wa fedha na fursa za ajira kwa Watanzania.

Amesema Serikali itamiliki asilimia 16 ya hisa huru zisizohafifishwa thamani katika kampuni ya ubia, huku Kampuni ya Lindi Jumbo Limited ikimiliki asilimia 84.

“Makubaliano haya yanaihakikishia Serikali ushiriki wa moja kwa moja katika manufaa ya mradi pamoja na uhakika wa mapato yatokanayo na uwekezaji huo,” amesema.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Lindi Jumbo Limited, Andrew Cunningham amesema kampuni itaendelea kufanya utafiti zaidi wa mashapo ya graphite ili kuongeza uzalishaji na kurefusha maisha ya mgodi.

Amesema hatua hiyo itasaidia kuongeza mchango wa mradi huo katika uchumi wa Tanzania pamoja na kuimarisha nafasi ya nchi katika soko la kimataifa la madini mkakati.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Nachingwea ambaye pia ni Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Ruangwa, Mohamed Moyo amesema Serikali ya Mkoa wa Lindi itaendelea kushirikiana na wawekezaji ili kuhakikisha miradi hiyo inaleta manufaa kwa wananchi na Taifa kwa ujumla.