Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Tozo mpya usafirishaji wa bidhaa nje ya Tanzania

Muonekano wa Bandari ya Dar es Salaam. Picha na Maktaba

Muktasari:

  • Kwa ujumla, lengo ni kuongeza mapato ya Serikali.

Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania inapendekeza kufanya marekebisho kwenye Sheria ya Usafirishaji wa Bidhaa Nje ya Nchi, Sura ya 196.

Lengo ni kutoza tozo ya usafirishaji wa bidhaa kwenda nje ya nchi kwa kiwango cha asilimia 30 ya thamani ya mzigo (FOB) au Sh200 kwa kila kilo moja, kutegemeana na kiwango kitakachokuwa kikubwa, kwenye taka za karatasi (waste paper) zinazotambulika kwa HS Code 4707.00.00.

Lengo la hatua hiyo ni kuchochea uongezaji wa thamani nchini na kuhakikisha upatikanaji wa malighafi hiyo kwa wazalishaji wa karatasi na maboksi nchini. Hatua hii inatarajia kuongeza mapato ya Serikali kwa kiasi cha Sh415 milioni.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Fedha, Balozi Khamis Mussa Omari, wakati akiwasilisha bajeti ya Serikali ya mwaka 2026/2027 ya Sh62.3 trilioni leo Alhamisi, Juni 11, 2026, Bungeni jijini Dodoma.

“Kutoza tozo ya usafirishaji wa bidhaa kwenda nje ya nchi kwa kiwango cha asilimia 10 au Sh200 kwa kila kilo, kutegemeana na kiwango kitakachokuwa kikubwa, kwenye madini ya quartz yanayotambulika kwa HS Heading 25.06 na feldspar zinazotambulika kwa HS Code 2529.10.00.

“Lengo la hatua hii ni kuhakikisha uwepo wa malighafi za kutosha kwa wazalishaji wa marumaru na vioo nchini. Hatua hii inatarajia kuongeza mapato ya Serikali kwa kiasi cha Sh6 bilioni,” amesema.

Pia, kutoza tozo ya usafirishaji wa bidhaa kwenda nje ya nchi kwa kiwango cha Sh50 kwa kila kilo ya pumba za ngano (wheat bran) zinazotambulika kwa HS Code 2302.30.00; mashudu ya pamba (cotton cake) yanayotambulika kwa HS Code 2306.10.00.

“Pumba za mpunga (rice bran) zinazotambulika kwa HS Code 2302.40.00; pumba za mahindi (maize bran) zinazotambulika kwa HS Code 2302.10.00; na mashudu ya alizeti (sunflower cake) yanayotambulika kwa HS Code 2306.30.00,” amesema.

Amesema lengo la hatua hii ni kuhakikisha upatikanaji wa kutosha wa bidhaa husika ambazo ni malighafi muhimu katika uzalishaji wa vyakula vya mifugo. Hatua hii inatarajia kuongeza mapato ya Serikali kwa kiasi cha Sh17.95 bilioni.

Waziri huyo wa Fedha amesema hatua hizi kwa ujumla wake zinatarajiwa kuongeza mapato ya Serikali kwa kiasi cha Sh24.44 bilioni.